Charles Hilary atakumbukwa kwa haya….

Dar es Salaam. Nguli wa tasnia ya habari nchini, Charles Hilary amefariki dunia, huku wadau waliowahi kufanya kazi naye, wakimkumbuka kwa weledi, umahiri wa kitaaluma, ucheshi na sauti yake ya kipekee waliyoifananisha na dhahabu.

Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa walioguswa na msiba huo, akimtaja kuwa nguli aliyekuwa na mchango wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari nchini, tangu akiwa mtangazaji wa redio hadi televisheni.

Ukiacha kutangaza katika vituo vya redio na luninga za ndani ya nchi, Charles ameitumikia taaluma ya habari katika mashirika ya kimataifa ikiwemo Deutsche Welle (DW) na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Mwanahabari huyo, amefariki dunia akiwa na wadhifa wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, tangu alipoteuliwa Desemba 30, mwaka 2021 na Februari 6, 2023 kuteuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali visiwani humo.
Taarifa ya kifo chake iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Zena Said, inaeleza Charles alifariki alfajiri ya jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila alikokuwa akipatiwa matibabu.

Sambamba na taarifa hiyo, Mwananchi jana ilizungumza na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed ameyasema Charles alifariki dunia saa 9:20 usiku akiwa hospitalini Mloganzila alikopelekwa kwa matibabu. 

Amesema mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Ijumaa saa 2 usiku licha ya kuwa alikuwa anaumwa, hali haikuonekana kuwa mbaya kiasi hicho.

“Tulikuwa na matukio mawili ya kazi ya Rais Jumamosi. Nilijaribu kuwasiliana naye lakini haikuwezekana, tukalazimika kuendelea na shughuli kama kawaida,” amesema Raqey.
Rais Samia amlilia

Katika salamu zake za pole, Rais Samia kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii aliandika, “natoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wote wa sekta ya habari kwa msiba huu mkubwa.”

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, atamkumbuka Charles kwa mchango wake wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari, tangu akiwa mtangazaji wa redio hadi televisheni, pia kama mshauri kwa waandishi chipukizi.

“Namuomba Mwenyezi Mungu aijaze familia yake subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, na aiweke roho ya mpendwa wetu mahali pema peponi. Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea,” ameandika Rais Samia.

Wanavyomzungumza

Ivona Kamuntu ni amewahi kuwa mtangazaji mwenza wa Charles alipokuwa katika Kituo cha Luninga cha Azam, amesema atamkumbuka kwa sifa ya utu na furaha mara zote na mwadilifu kazini.

“Wakati nikiwa Chief Anka na yeye akiwa Mkurugenzi wa Redio, mara nyingi alikuwa anatoka redioni na kuja TV, akanichukulia kama bosi wake licha ya cheo chake. Hii inaonesha jinsi alivyokuwa na maadili ya hali ya juu,” amesema Ivona.

Umakini katika kazi ni sifa nyingine aliyokuwa nayo Charles kwa mujibu wa Ivona, akisisitiza hakuacha habari iende hewani bila kuipitia.

“Kama tukitaka kurusha habari ya dharura, alikuwa anasisitiza ifanyiwe marekebisho kwanza. Hakuwa tayari kufanya kosa akiwa hewani. Alikuwa ni mtu wa viwango vya juu sana kitaaluma,” amesema.

Charles amewahi kufanya kazi katika Redio Tanzania na mwaka 1991, alimpokea na kumfundisha utangazaji wa mpira, Abubakar Liongo kama anavyosimulia.

Liongo amesema sio kutangaza mpira pekee, Charles alimfundisha kusoma hata taarifa ya habari na baadaye akahamia Redio One naye akashawishika kwenda huko.

“Baadaye, Charles alinishawishi nihamie Redio One baada ya kuniombea kwa baba yake. Alikuwa kaimu Mkurugenzi kipindi hicho kabla ya kwenda Sauti ya Ujerumani (DW), na mimi nikaanzisha Redio Uhuru,” almesema Liongo.

Liongo amesema Charles alipoondoka DW kwenda BBC, yeye ndiye aliyerithi nafasi yake katika kituo hicho na kwa miaka yote wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu.

“Alibarikiwa kipaji kikubwa cha kutangaza, sauti yake ilikuwa na mvuto kwa kila kipindi, asingeweza kufanya kipindi iwe kwenye michezo au habari za kawaida ukashindwa kufurahia, au ukasikia kipindi kinapwaya,” amesema mtangazaji mkongwe wa ndani na nje ya Tanzania, Abdallah Majura.

Amesema akiwa Radio One, Charles alianzisha kipindi cha charanga, licha ya muziki huo kutokuwa maarufu Tanzania, lakini kwa kipaji chake na uwezo wa kukiandaa, kilikuwa kizuri na maarufu nchini.

Amesema kupitia kipindi hicho, aliyekuwa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi alipokuwa akisafiri kwenda nje ya nchi alikuwa anarudi na CD nyingi za muziki huo anampa Charles.

“Alikuwa na ulimi, lafudhi Kiswahili kizuri, alikuwa mtaalamu wa Kiswahili, kwa hiyo alipokuwa akichanganya vyote hivyo kilikuwa kinavutia sana,” amesema Mjura.

…alinitoa mavumbini

Wakati Majura akisema hivyo, Mtangazaji mwingine, Regina Mziwanda alisema Charles alimtoa kwenye dimbwi la kilio na kusaga meno lakini akamshika mkono akitamani afike mbali.

“Charles Hilary alinitoa kwenye dimbwi la simanzi, kilio na kusaga meno wakati nilipopigwa zengwe nikiwa Redio Uhuru bila kujali mizengwe hiyo alisimama kuhakikisha naingia Redio One na kutokea hapo dunia ikanifahamu,” amesema.
Mtangazaji huyo wa BBC, alisema,

“kwa kweli Mbuyu umeanguka, tasnia ya habari tutamkumbuka, mcheshi, mbunifu na mtu mwenye utu wake, na mtu mwenye kauli, mtu anayejua utu, Mwenyezi Mungu amrehemu, ampe kauli thabiti na ampokee, pumzika salama Charles Hilary.”
Charles katika familia

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ni miongoni mwa waombolezaji waliofika nyumbani kwa Charles Kibamba jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia msiba wa baba yake, mtoto wa mwisho wa Charles, Faith Hilary amesema baba yake alianza kuumwa miezi kadhaa iliyopita na alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Alfajiri ya leo Mei 11, 2025 hali yake ilibadilika tukamuwahisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila ndipo tulipopewa taarifa kuwa amefariki dunia,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Faith, ratiba ya sasa inaonyesha Charles atazikwa Jumatano Mei 14, 2025 katika makaburi ya Anglikana huko Mwanakwerekwe visiwani Zanzibar.

Amesema ibada ya kumuaga inatarajiwa kufanyika Jumanne Mei 13 katika kanisa la Anglikana lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam kisha kusafirishwa kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya maziko.
Amesimulia enzi za uhai wa baba yake, akimtaja kuwa mzazi aliyekuwa mcheshi na alipenda kufanya kazi kwa bidii.

“Kufanya kazi kwa bidii kilikuwa ni kipaumbele cha baba, hata katika nyakati zake za mwisho alikuwa anahakikisha kazi zake zinaenda vizuri,” amesema.

Katika uhai wake, Faith amesema baba yao amekuwa akiwasisitiza kuwa na nidhamu, kupenda kuwa na furaha, kufanya kazi kwa bidii na kuweka akiba kwa ajili ya baadaye.

Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu amesema Charles alikuwa mmoja kati ya washauri wake wa karibu katika masuala mbalimbali ya maendeleo katika eneo la Kibamba.

“Kwangu alikuwa ni kaka na mshauri tangu nikiwa diwani hata kabla ya kuwa mbunge hakika tumepoteza mtu mpenda maendeleo,” alieleza.

Alikuwa mcheshi, lakini haya yaliondoa tabasamu la Charles Hilary

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Hassan Mhelela amesema alikutana na Charles mwaka 1996 alipomaliza kidato cha sita, alipokuwa  anataka kuanza uandishi wa habari.

Amesema katika muda wote ambao amefanya naye kazi tangu Redio One, BBC kisha Azam, alikuwa ni mtu wa kuzingatia taaluma na maadili ya kazi.

“Alikuwa mkali sana watu anaofanya nao kazi akitaka wafuate taratibu za kitaaluma zilizowekwa kwa mfano matumizi ya lugha ni mwalimu wa Kiswahili, alikuwa anafoka sana akikuta mtangazaji kijana au mkongwe anashindwa kuzingatia misingi ya lugha,” amesema Mhelela.

Pamoja na kufoka kwake, amesema Charles alikuwa mcheshi, mwenye vichekesho, utani, mzaha, lakini ni mtu mwenye kukasirika pale ukiharibu kazi.

“Unapokiuka maadili au kanuni za kazi alikasirika na unamuona kabisa tabasamu limeondoka, hayo yote ni kwa sababu alizingatia sana maadili ya kazi,” amesema.

Naye, Varelie Msoka amesema alimfahamu alipojiunga na Redio Tanzania akiwa miongoni mwa watangazaji waliokuwa na uwezo wa kutangaza taarifa za habari, utayarishaji wa vipindi na kutangaza mpira mubashara.

Amesema sio kawaida mtu kuwa na uwezo wa kumudu vyote hivyo kwa ustadi na ufasaha, lakini Charles alifanikiwa.

Amefafanua kuwa  mtangazaji  huyo alijaaliwa kuwa na sauti yenye mvuto kwa msikilizaji wa redio au mtazamaji kwenye televisheni, akisema alikuwa na kipaji kikubwa cha kutangaza mpira redioni. 

“Wasikilizaji wengi wakati huo kabla TV hazijaingia walikuwa wakifurahi sana kama siku hiyo mtangazaji anakuwa Charles Hilary,” amesema Msoka. 

Amesema Charles alikuwa na ujasiri wa aina yake akirejea jinsi alivyoondoka RTD na wenzake kwenda kuanzisha Redio One.

“Huu ni ujasiri na uthubutu maana enzi hizo unakaa mahali mpaka unastaafu.”

Amesema licha ya kwamba hakuwapo alipoenda DW na BBC London Idhaa ya Kiswahili, mbwembwe zake za RTD hakuziacha, alivutia wasikilizaji na watazamaji wengi.

Mtoto wa mwisho wa marehemu, Faith Hillary

“Kwa hakika tasnia imepoteza mtu aliyeipenda, kuheshimu na kuifurahia kazi yake. Kwa ufanisi, heshima na uthubutu, aliweza, hatua kwa hatua, kutoka mtangazaji wa RTD hadi Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema.

Charles aliwahi kuwa mtumishi mwandamizi wa kituo cha Azam Media Limited kati ya mwaka 2015 na 2023. Alihitimisha muda wake akiwa Mkuu wa Idara ya Redio ya UFM, baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.

Hilary pia amewahi kuvitumikia vituo mbalimbali vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wakati huo likiitwa Redio Tanzania na Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) na DW Idhaa ya Kiswahili.

Kwa mujibu wa familia hadi anafikwa na umauti nguli huyo wa habari, ameacha mke na watoto wawili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *