
Kama alivyosema Kocha wa Simba, Fadlu Davids kwamba watahakikisha wanaimaliza mechi dhidi ya Al Masry hukohuko Misri, ndicho walichoamua kukifanya mabosi wa timu hiyo kwa kukiweka kikosi sehemu salama zaidi ili kuepuka fitna zozote za wapinzani wao ambazo zinaweza kukwamisha mipango waliyoiweka.
Kikosi cha Simba ambacho kilitua Misri Ijumaa, wiki hii tayari kwa mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika mkondo wa kwanza dhidi ya Al Masry hatua ya robo fainali, unaambiwa kambini walipofikia wameweka ulinzi unaowafanya wapinzani wao kushindwa kufika kirahisi.
Jambo la kwanza ambalo Simba walilifanya baada ya kutua Misri kikosi hicho kilisafiri umbali wa kilomita 125.2 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo na kuweka kambi sehemu ambayo Al Masry hawatathubutu kukanyaga kirahisi huku wakiweka ulinzi wa watu 10.
Simba imeweka kambi ya siku nne jijini Ismailia inapotokea Klabu ya Ismailia ambao ni wapinzani wa Al Masry katika Ligi Kuu ya nchi hiyo huku wakifikia kwenye hoteli moja kubwa iitwayo Tolip Resort El Forsan Ismailia yenye kila kitu mpaka uwanja wa kufanyia mazoezi.
Taarifa kutoka katika kambi hiyo, zimeifikia Mwanaspoti zikibainisha kuwa walinzi hao 10 wanaowalinda mastaa wa Simba, watano kazi yao kubwa ni kusimamia usalama wa ndani ya hoteli huku waliobaki wakishughulikia usalama wa nje kuhakikisha hakuna ambaye anaweza kufanya jambo lolote litakaloathiri mipango yao.
“Hapa ulinzi mkubwa ni wetu, tumehakikisha walinzi wote wanakuwa wa kwetu, wale wa hoteli wanaishia pale getini ambako nako kuna watu wetu.
“Kati ya watu watano waliopo nje baadhi wako getini wakihakikisha kila anayeingia akionekana anataka kuja eneo tulilopo anatakiwa kujieleza sawasawa, jambo zuri ni kwamba tuna vijana ambao wanasoma hapa Misri wanajua lugha ya hapa (Kiarabu) nao wamejitolea kuhakikisha tunakuwa salama,” alisema bosi mmoja wa juu wa Simba ambaye ameambatana na timu hiyo nchini Misri.
Mbali na kuweka ulinzi wa watu 10, mtoa taarifa huyo amesema pia wamehakikisha masuala ya chakula wanaandaa wenyewe kufuatia kusafiri na mpishi wao ambaye amekabidhiwa jiko hotelini hapo huku wakibeba vyakula vyao vya kupika kutoka Tanzania ambavyo benchi la ufundi limependekeza kuvitumia nchini humo.
DAKIKA 26 ZA MOTO
Muda mfupi baada ya kufika Misri, Kocha Fadlu alifanya kikao na wachezaji kilichochukua dakika 26 hadi kumalizika, huku jambo la tofauti ni kwamba, tangu waanze kucheza mechi za kimataifa msimu huu hakuwahi kufanya kama hivyo.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba katika kikao hicho, Fadlu amewataka wachezaji wote kuzichukulia kwa uzito mkubwa mechi mbili za hatua ya robo fainali ugenini na nyumbani kwani zimebeba heshima ya klabu yao.
“Fadlu amewataka wachezaji wote kuamsha akili zao kuwa mechi hizi mbili zimebeba heshima ya klabu, huku akiwaambia mastaa wake kwamba hakuna ambacho wanawadai viongozi wao.
“Kila bonasi zao zimelipwa na bado watakuwa nazo katika mchezo huu lakini wachezaji ndio wana deni kwa viongozi na mashabiki kwa kushinda ugenini.
“Pia amewaambia hii ni robo fainali, wanatakiwa kucheza kikubwa, hataki kuona yanafanyika makosa ambayo yanaepukika, amemtaka kila mchezaji kuzingatia maandalizi wanayoyafanya kuwakabili Al Masry wakiwa kwao, anataka mechi imalizikie Misri na sio kusubiri kumalizia nyumbani,” alisema bosi huyo.
RATIBA YA MAZOEZI
Timu ilipofika Misri Ijumaa, ilifanya mazoezi usiku kwenye uwanja uliopo hotelini hapo huku siku zingine wakiwa hapo kuanzia Jumamosi ratiba itaendelea kwa kufanya mazoezi mchana katika uwanja ambao tayari wameuandaa kabla ya baadaye kuhamia uwanja wa mechi siku moja kabla.
Ikumbukwe kuwa, mchezo huo utafanyika kwenye Uwanja wa New Suez uliopo Mji wa Suez ambapo Simba imeshajua ubora wa uwanja huo wakibaini hauna tofauti kubwa na ule wanaoutumia hivi sasa jijini Ismailia.
Umbali kutoka ilipo kambi ya Simba katika Mji wa Ismailia hadi Suez ambapo watakwenda kucheza mechi hiyo Jumatano saa 1 usiku ni takribani kilometa 91, kwa mwendo wa gari unatumia saa 1 na dakika 20.
HOTELI WALIYOFIKIA
Simba imefikia Tolip Resort El Forsan Ismailia, hoteli ambayo ina kila kitu ikiwemo sehemu ya kufanyia mazoezi kukiwa na gym yenye vifaa vya kisasa sambamba na bwawa la kuogelea la viwango vya Olimpiki. Hoteli hiyo ina vyumba 305, vyote vikiwa na mandhari ya kipekee inayoangalia Ziwa Al Temsah, njia ya meli ya Mfereji wa Suez.
MSIKIE AHMED ALLY
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Tumeamua kukaa Ismailia ambapo ni mji wa timu pinzani na Al Masry, ukiwa hapa hakuna anayetaka kuisikia Al Ahly wala hao Al Masry, huku sio kama huko kwetu kwamba ukienda Kigoma unakutana na Wanasimba kama ilivyokuwa Dar es Salaam, hapa wanataka kujua Ismailia tu, ukitaja Al Masry wanachukia na hao Al Masry hawaji hapa,” alisema Ally.