
Unguja. Wakati mwili wa Padri Anselmo Mwang’amba (77), ukitarajiwa kuzikwa Machi 4, 2025 katika Kanisa la Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar umetaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
Padri Mwang’amba alifariki dunia asubuhi ya Februari 27, 2025 akiwa kanisani hapo akitoa huduma.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi Mosi, Katibu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo la Zanzibar, Padri Cosmas Shayo amesema kiongozi huyo wa kiroho alikuwa akisumbuliwa na mgongo kwa muda na ndiyo sababu ya kifo chake.
“Alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mgongo, kanisa litamkumbuka kwa mengi mazuri, alifanya kazi akiwa kijana mpaka umauti unamkuta,” amesema.
Amesema Padri Mwang’amba aliyezaliwa Juni 4, 1948 wilayani Mbozi mkoani Mbeya, alipata daraja takatifu la upadri Juni 14, 1981 akiwa na umri wa miaka 33.
Mpaka alipofariki dunia, amesema Mwang’amba alikuwa amelitumikia kanisa kwa kipindi cha miaka 44 akifanya kazi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Amesema kanisa limepata pigo kwa kifo cha padre huyo aliyefanya kazi yake kwa weledi na ufanisi.
“Kanisa limepata pigo kwa sababu tumeondokewa na padri mwenye weledi na aliyefanya kazi kwa ufanisi zaidi, ila Mungu ameamua kumchukua na hilo ni pigo kubwa kwetu,” amesema.
Septemba 2013, Mwang’amba alimwagiwa tindikali na kulazwa katika Hospitali ya Mnazimmoja Zanzibar kisha kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Tukio hilo lilitokea katika Mtaa wa Mlandege, Mkoa wa Mjini Magharibi. Alijeruhiwa usoni, kifuani na mkononi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana wakati huo, kiongozi huyo wa kiroho alikuwa akitokea katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao wa simu saa 10:15 jioni.
Watuhumiwa wa tukio hilo ilielezwa walimtega mlangoni kabla ya kufanya uhalifu huo na kutokomea kwenye vichochoro vya mitaa ya Mtendeni na Mchangani.
Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Padri Stanley Lichinga amesema japo kifo ni mipango ya Mungu lakini pengo lake haliwezi kufutika.
“Ametumika na amefikia wakati wa kutuaga roho yake ilazwe pema, hatuwezi kukataa kwamba asiondoke wapo wanaondoka Mungu ameshawatumia lakini umefika wakati wa kuondoka tusimkufuru Mungu,” amesema.