Chanongo aziwaza dakika 270

KIUNGO wa Tanzania Prisons, Haruna Chanongo amesema wana dakika 270 ngumu za maamuzi ya timu hiyo kusalia Ligi Kuu au la, kutokana na kile ambacho watakivuna katika mechi tatu zilizosalia.

Prisons ipo nafasi ya 14 katika mechi 27 ilizocheza imeshinda saba, sare sita na imepoteza 15, ikifunga mabao 21 na kufungwa 36 ikikusanya pointi 27, jambo analoliona Chanongo wanahitaji kuvuja jasho ili kusalia salama kwa msimu ujao kwani pointi walizonazo ni mtihani mzito kwa sasa.

Maafande hao walioshinda mechi tatu mfululizo ukiwamo wa juzi dhidi ya JKT Tanzania walioilaza mabao 3-2, sasa imesaliwa mechi dhidi ya Coastal Union, Yanga na Singida Black Stars na kama itashinda zote itakusanya pointi tisa, huku Yanga ikipambana kutetea ubingwa na Singida ikiwani Nne Bora.

“Kazi iliyopo mbele yetu ni ngumu, tunahitaji kujitoa na kupambana kwa jasho hivyo dakika 270 ndizo zimebeba maamuzi ya Prisons kusalia Ligi Kuu au la,” alisema Chanongo ambaye katika mechi 11 alizocheza akiwa na timu hiyo amefunga mabao matatu na asisti mbili.

Nyota huyo wa zambi wa Simba, alisema wakati anajiunga na Prisons msimu huu alitokea Pamba ilipokuwa Ligi ya Championship na alifunga mabao 15, ila kitendo cha kucheza Ligi Kuu kwake alikichukulia ni hatua moja mbele licha ya kukiri kuuona ugumu na ushindani mkali kwa msimu huu.

“Wachezaji tuna vipindi tofauti katika kazi yetu ya mpira wa miguu,mfano ukisema nikutajie msimu bora kwangu ulikuwa wa 2013/14 nikiwa Simba nilifunga mabao manane na 2016/17 nikiichezea Mtibwa Sugar nilimaliza na mabao manane,” alisema Chanongo anayemkubali winga Elie Mpanzu anayekipiga katika timu ya Simba namna anavyoonyesha bidii na kiwango chake kubadilika siku hadi siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *