
Mmoja wa marafiki zangu wa nje walionitembelea hivi karibuni aliniambia “Dar es Salaam is beautiful, but it’s quite dark at night. Is it safe?” (Dar es Salaam ni mji mzuri, lakini una giza. Je, ni salama kuishi hapa?”)
Elijah (rafiki huyo Mjerumani) aliniambia tulipofika Coco Beach Masaki tukitokea Mwenge, hapo tulifuata mishikaki, juisi ya muwa pamoja na upepo wa bahari.
Pengine yeye alitaka kuifananisha Dar es Salaam na mji wake wa Cologne au mji mkubwa ya nchini yake (Berlin), sifahamu lakini anafikirisha. Nilichomjibu mimi ni kuwa Dar ni salama sana asijali kuhusu giza.
Wakati tukiendelea na kilichotupeleka Coco ambacho yeye alikifurahia sana nikawa nawaza na kuwazua, mwishoni nikasema angekuja miaka 10 iliyopita angestaajabu mengi, kidogo sasa jiji letu namba moja nchini limebadilika sana.
Kutokana na ongezeko la watu na kukua kwake, Dar es salaam linatajwa kuwa jiji kuu (Megacity) ifikapo mwaka 2030. Kwa sasa majiji yenye hadhi hiyo Barani Afrika ni Lagos, Cairo na Kinshasa. Luanda la Angola nayo inatarajiwa kama ilivyo kwa Dar es Salaam.
Hata hivyo, pamoja na maendeleo makubwa katika ujenzi na upanuzi wa miundombinu katika Jiji hili, Suala la giza limebaki kuwa changamoto kwa wakazi wake na tena si kwa sababu ya kukatika kwa umeme.
Giza linalotawala barabara kuu na za mitaa ndani ya Jiji la Dar es Salaam si tu tishio kwa usalama wa watu binafsi, bali pia ni kikwazo kwa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya mji.
Kukosekana kwa taa za barabarani si tu kwamba kunahatarisha usalama wa maisha na mali za wakazi, bali pia kunazidisha vikwazo vya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.
Barabara ambazo zilitarajiwa kuwa nguzo za maendeleo ya kisasa baadhi zimegeuka kuwa vichaka vya uhalifu, ajali na hofu kwa waendesha bodaboda, madereva wa magari, na hata wapita njia wa kawaida.
Hii ni licha ya juhudi za serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ambao ndio wasimamizi wakuu wa miundombinu hiyo.
Katika baadhi ya barabara kuu kama Morogoro, Nyerere, Mandela, Sam Nujoma na zile za pembezoni kama Goba, Malamba Mawili, Buza, Kinyerezi, na Mbezi Beach ukosefu wa taa za barabarani umesababisha hali ndogo ya usalama hata kutopendeza kwa mji.
Maeneo mengine ni Tabata, Kinyerezi-Mbezi, Kinondoni Makaburini, baadhi ya mitaa ya Masaki, Ununio, Mikochen, Malamba Mawili, Pugu, Tandika-Buza, Majohe, na hata baadhi ya mitaa ya katikati mwa jiji kama Posta na Kariakoo.
George Mbezi, dereva wa bodaboda maeneo ya Mwenge, anasimulia namna giza lilivyogeuza baadhi ya njia kuwa maeneo hatari ya maisha.
“Ukifika saa mbili usiku, hata mtu akisema atakulipa Sh30,000 ili nimpeleke Madale, siendi. Huko ni vichaka tupu. Mteja humjui, unaweza kukabwa saa yoyote,” anasema Mbezi.
Mbezi anasema maeneo mengi wanayopeleka abiria hayana taa, yanategemea mwanga wa nyumba za watu au maduka ya jirani. Hatari inakuwa kubwa zaidi hasa kwa wageni ambao hawajui miinuko na mashimo yaliyofichwa na giza.
Katika Jiji la Dar es Salaam, Tanroads inasimamia barabara kuu zenye umuhimu wa kiuchumi na kimkakati zenye urefu wa kilomita 494.3, wakati Tarura inasimamia barabara za ndani ya jiji zenye urefu wa kilomita 1,600.
Halmashauri za Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke kwa pamoja zinahusika na zaidi ya kilomita 1,600 ya barabara hizo.
Latifa Hussein, mkazi wa Malamba Mawili anasema giza limesababisha ajali nyingi pamoja na matukio ya wizi na uporaji katika eneo la barabara inayounganisha maeneo ya Mbezi kupitia kona ya Ndodi.
“Mtu anaona ni karibu kutoka kwa Ndodi kwenda kona, lakini kwa hofu ya usalama wake barabarani, anachagua kupanda bodaboda,” anasema na kuongeza kuwa wengine hulazimika kushuka vituo vya mbali vyenye mwanga kwa kuhofia usalama wao.
Latifa anaongeza: “Eneo letu lina mashimo mengi, mtu akipita usiku bila kujua anaweza kujikuta kwenye shimo na kuharibu chombo chake. Barabara zetu pia hazina taa, nyumba zipo chache na nyingine zipo mbali na barabara, giza ni kubwa mno.”
Naye Aboubakar Njovu, dereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi na Makumbusho kupitia Goba anasema barabara ina giza, ikitokea taa yake ikaungua au ikapunguza mwanga anatumia uzoefu tu.
Serikali inasemaje
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, tayari alishaelekeza kwamba kila mradi wa ujenzi wa barabara jijini Dar es Salaam uende sambamba na ufungaji wa taa.
“Nisingependa kuona katika miji barabara zinakuwa na giza, kasi ya ujenzi wa barabara iendane na ufungwaji taa za barabarani,” alisema Ulega Desemba 15, mwaka jana wakati akikagua ujenzi wa mradi wa BRT awamu ya pili.
Akizungumza na Mwananchi Machi 12, 2025 Mhandisi wa Umeme Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Juma Omar anasema watafunga taa 213 ambazo zitagharimu Sh800 milioni kwa mitaa ya Mafia, Pemba, Tandamti, Stesheni na Pugu Mnadani.
“Sisi mitaa ambayo tunaweka taa hizo ni ile ambayo barabara zilikuwepo tangu zamani kabla ya kuanzishwa kwa Tarura, tunatumia vyanzo vya mapato ya ndani kuzinunua,” anasema.
Anasema taasisi nyingine zinasaidia katika hilo, wakiwamo Tarura ambapo katika moja ya masharti kila wanapojenga barabara zao lazima wafunge na taa.
Kwa tathmini ya mwaka 2022 kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Wilaya ya Ilala pekee inahitaji takriban taa 38,000, huku zilizopo ni 4,000 tu. Gharama ya taa moja ni kati ya Sh3 milioni hadi Sh10 milioni kulingana na aina ya taa.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Alinanuswe Kyamba, anasema maeneo ambayo tayari yana taa lakini hazifanyi kazi, wameingia mikataba ya marekebisho na makandarasi.
“Maeneo ambayo yana taa lakini hazifanyi kazi kuna mkandarasi anafanyia marekebisho na katika kuhakikisha hali hiyo inaendelea vizuri kwa sasa tumeweka taa barabara ya Sam Nujoma kwa ajili ya kuongeza usalama zaidi,” anasema Kyamba.
Anasema barabara nyingine zinaendelea kujengwa kupitia mradi wa mabasi ya mwendokasi, hivyo haiwezekani kufunga taa mpya wakati mradi unaendelea, hivyo wanaendelea kufanyia matengenezo zilizopo.
Kwa upande wa Tarura, Meneja wake, Geofrey Mkinga anasema kuwa katika miradi mipya ya barabara, wanatarajia kufunga taa 3,580.
“Tunaongeza taa zenye nafasi nzuri kuondoa vivuli na kuongeza usalama kwa biashara za saa 24,” anasema Mkinga.
Aidha, ameongeza kuwa wapo katika mpango wa kubaini aina bora ya taa zitakazodumu muda mrefu bila kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Kuhusu usalama wa watu katika maeneo yenye giza, Machi 4, 2025, Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele alisema jeshi hilo limeongeza askari na magari katika maeneo yenye giza ili kuhakikisha usalama wa wakazi na watumiaji wa barabara katika jiji hilo.
“Vyote hivi vinafanyika kuhakikisha hali ya usalama unaimarika na watu kuwa huru kutembea, maeneo korofi tunaongeza nguvu ya ziada huku tukiendelea kutoa elimu kwa wananchi wa eneo husika,” anasema Mafwele.
Mafwele amewasisitiza wananchi kuweka taa kubwa na kamera za CCTV nje kwenye mitaa yao ili kuimarisha ulinzi.
Nini kifanyike?
Mkurugenzi wa taasisi ya utoaji wa elimu ya usalama barabarani (TARSI), Maliki Mwarongo anasema ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali na mashirika ya kijamii wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya ufungaji wa taa za barabara za kisasa na za nishati endelevu (nishati ya jua) katika maeneo muhimu.
“Serikali imejitahidi kutengeneza barabara nyingi kubwa na ndogo, lakini tatizo lililopo ni taa ambapo kuna maeneo yamewekewa taa lakini hazifanyiwi marekebisho ya mara kwa mara na mamlaka hata zinapoungua au kugongwa,” anasema.
Anasema ushirikiano na ufungwaji wa taa za sola itasaidia kuangamiza giza na kufanya mitaa kuwa salama zaidi.
Hata hivyo, katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Kiwanda cha Sky Zone kilichopo chini ya Suma JKT, walieleza kuwa wameanza kuzalisha taa za barabarani zinazotumia umeme wa jua (sola) na umeme wa kawaida kwa ajili ya kupunguza changamoto ya giza mitaani.
“Tunalenga kuwasaidia taasisi za serikali na sekta binafsi kukabiliana na changamoto ya giza katika barabara za mijini na vijijini,” alisema Mhandisi Salome Lwanteze.