
Dar es Salaam. Ugumu wa kupatikana kwa mitaji, ukosefu wa ujuzi wa masoko na gharama za juu za usajili wa biashara vimetajwa kuwa baadhi ya sababu zinazowakwamisha wajasiriamali wanawake kufikia mafanikio kamili katika biashara zao.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 14, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Her Initiative, Lydia Moyo wakati akiwasilisha ripoti ya Uchunguzi wa Hali ya Biashara kwa Wanawake Vijana Wajasiriamali katika mkutano uliowakutanisha wajasiriamali, serikali pamoja kupitia jukwaa la Panda Event 2024.
Moyo amesema uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo umebaini kuwa baadhi ya wajasiriamali wanashindwa kufikia malengo yao kibishara kutokana na kutokuwa na ujuzi juu ya mbinu sahihi za kuzitumia ili kulifikia soko kikamilifu.
“Kwa mujibu wa uchunguzi huo asilimia 75 ya wanawake wajasiriamali wanahitaji mafunzo na ushauri wa kitaalamu juu ya mbinu bora za kuendesha kampeni za masoko mtandaoni kwa ufanisi, ili waweze kufikia wateja wengi zaidi na kuongeza mapato ya biashara zao,” amesema.
Amesema zaidi ya asilimia 60 ya wanawake vijana wajasiriamali wanatumia mitandao ya kijamii, kama Instagram na Facebook, kutangaza bidhaa zao.
Ameeleza kuwa licha ya mitandao hiyo kuwa na msaada katika utangazaji wa bidhaa kwa wajasiriamali bado baadhi yao hawanufaiki kutokana na changamoto, ikiwemo ukosefu wa vifaa vinavyofaa kama simu bora au kompyuta, ujuzi mdogo wa masoko ya kidigitali.
Pia ametaja ya gharama za matangazo pamoja vifurushi vya intaneti zinaathiri uwezo wao wa kuyatumia majukwaa hayo kwa ufanisi.
Vilevile amegusia changamoto katika urasimishaji wa biashara kwa wajasiriamali, ambapo kwa mujibu wa uchunguzi huo zaidi ya asilimia 50 ya wajasiriamali hawa hawajasajili biashara zao rasmi, kutokana na changamoto kama gharama za usajili, ukosefu wa taarifa juu ya mchakato wa usajili, na ukosefu wa muda.
Amesema Hali hiyo inawazuia kupata manufaa muhimu, kwani bila usajili rasmi wanakosa fursa ya kushiriki katika kupata masoko rasmi na kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara zao.
“Urasimishaji wa biashara ungeweza kuboresha uwezekano wa upanuzi wa biashara na kuwapa wajasiriamali hawa upatikanaji wa fursa kama mikopo, ambayo ni muhimu kwa maendeleo endelevu.
“Ili kuwasaidia kushinda changamoto hizi, kuna haja ya kuanzisha programu za kutoa elimu na msaada wa kiufundi juu ya usajili kwa wanawake wajasiriamali,” anasema.
Akihutubia katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha wajasiriamali wanawezeshwa ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kuwawezesha wajasiriamali kupata mikopo rafiki ili kuwawezesha wao kukua kibiashara akitolea mfano mikopo inayotolewa na halmashauri mbalimbali nchini.
Pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakiwapatia elimu wajasiriamali hao ili waweze kufikia malengo yao kibiashara.
“Kuwawezesha wasichana kiuchumi ni msingi wa maendeleo ya Tanzania. Kwa kushirikiana na mashiriko kama TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) na TBS (Shirika la Viwango Tanzania), tunahakikisha kuwa wajasiriamali hawa wanapata elimu ya masuala ya kodi, usajili wa biashara,” anasema.
Amina Mazengo ambaye ni mjasiriamali anasema kuwa kutolewa kwa mafunzo juu ya soko la kidigitali kwa wajasiriamali itawasaidia Mafunzo haya yatasaidia wajasiriamali hawa kujenga ujuzi wa masoko mtandaoni na kutumia majukwaa ya kidigitali kama vile mitandao ya kijamii kwa ufanisi zaidi ili kufikia wateja wengi zaidi.