Dodoma. Mambo manne yametajwa kutishia uendelevu wa sekta ya nyuki nchini Tanzania, ikiwemo matumizi ya dawa za kuua wadudu katika kilimo yasiyozingatia kiwango kinachotakiwa.
Mambo mengine ni ubadilishaji wa matumizi ya misitu kwa ajili ya shughuli nyingine, uchomaji wa misitu na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 18, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati akizindua maonyesho ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani.
Senyamule amesema sekta ya nyuki inakabiliwa na changamoto zinazotishia uendelevu wake na hivyo kuhatarisha uvunaji wa mazao ya nyuki kwa siku zijazo.
Amesema uendelevu wa sekta hiyo unatishiwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kuua wadudu katika kilimo bila kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule (kulia), alipotembelea mabanda ya maonyesho ya maadhimisho ya siku ya nyuki duniani katika viwanja vya Chinangali Ii jijini Dodoma.
“Mtu kwenye nyanya anaambiwa atumie nusu lita ya dawa, yeye anasema ‘ili wadudu wafe haraka natumia lita moja.’ Pale unapoteza ile dawa, haitaharibu nyanya tu bali na nyuki akija pale atakufa. Kwa hiyo ni muhimu tuzingatie matumizi sahihi ya viwango vya dawa,” amesema.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni uchomaji wa misitu, unaofanya nyuki kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine na wakati mwingine husababisha kuwapoteza iwapo wataungua kwenye moto.
“Kubadilisha maeneo ya misitu kwa matumizi mengine nayo ni changamoto. Na hili ni jambo ambalo linaelekea kuibuka kwa kasi kubwa nchini. Kila mahali watu wanatamani kumegewa msitu wajenge nyumba au waweke shughuli nyingine za kibinadamu,” amesema.
Senyamule amesema ulinzi wa maeneo ya misitu unapaswa kuzingatiwa ili kulinda viumbe hai, ikiwemo nyuki kwa sababu wana manufaa makubwa katika maisha ya binadamu.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaambatana na mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira rafiki kwa nyuki kuzalisha mazao yao.
“Pamoja na changamoto hizo bado tuna nafasi kubwa ya kukuza na kuendeleza sekta hii. Ni wazi bado tuna nafasi ya kuhifadhi misitu katika ardhi za vijiji, halmashauri, Serikali Kuu na hifadhi za wanyamapori,” amesema.
Aidha, Senyamule amesema Dodoma una zaidi ya mizinga 18,000 ya nyuki yenye uwezo wa kuzalisha lita 135,000 za asali.
Hata hivyo, amesema kiwango hicho ni kidogo ukilinganisha na fursa zilizopo Dodoma ambapo kuna zaidi ya hekta milioni moja za misitu iliyohifadhiwa inayoweza kutumika kwa shughuli za ufugaji nyuki.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesema maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya sita nchini.
“Pamoja na kutambua umuhimu wa nyuki, maadhimisho haya yanatoa nafasi kwa wananchi kutoka mikoa mbalimbali kujumuika kwa pamoja na kutambua fursa mbalimbali zilizomo kwenye sekta hii,” amesema.
Amesema pia maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kupata uelewa wa mafanikio mbalimbali yanayotokana na sekta ya nyuki.
Maadhimisho hayo yalianza Mei 17, 2025, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika kilele kitakachofanyika Mei 20, 2025, katika viwanja vya Chinangali II jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mwaka 2021, wastani wa pato linalotokana na asali nchini lilikuwa Sh818.4 milioni na nta ilikuwa ikiingiza wastani wa Sh2.6 bilioni.
Baadhi ya masoko makubwa ya asali inayozalishwa Tanzania ni pamoja na Afrika Kusini, India, Botswana, Namibia, Canada, Dubai, Kuwait, Iraq, Iran, Japan, China na Lebanon.