Championship vita imehamia huku

WAKATI Mtibwa Sugar ikizidi kupepea kileleni, kibarua kipo kwa miamba minne kusaka nafasi mbili za juu kwenye Championship kuitafuta Ligi Kuu msimu ujao.

Hii ni baada ya Geita Gold kupoteza mechi yake dhidi ya Polisi Tazania 1-0, huku Mbeya City ikiinyuka mabao 3-0 Songea United na Stand United kutakata ugenini 3-0 dhidi ya Biashara United.

Matokeo hayo yaliifanya Mtibwa Sugar kubaki katika usukani kwa pointi 54 baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya African Sports, Mbeya City nafasi ya pili kwa alama 46 sawa na Stand United, huku Geita Gold akifunga ‘Top Four’ kwa pointi 45 baada ya timu zote kucheza mechi 22.

Katika mechi zijazo, Geita Gold itakuwa nyumbani dhidi ya Mbeya Kwanza, Mbeya City ikiikaribisha Kiluvya United, huku Stand United ikiwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar na TMA walio nafasi ya tano kwa alama 41 wakiifuata Green Warriors.

Katibu Mtendaji wa Stand United, Fred Masai alisema wanafahamu vita ilivyo ngumu, lakini hesabu zao ni kukata ukame wa Ligi Kuu waliyoikosa kwa misimu mitano.

‘Kati ya mechi nane zilizobaki, tuna nne nyumbani na nne ugenini, ambapo ngumu zaidi ni Mtibwa na Geita hapa Shinyanga na Mbeya City na Songea tunaowafuata na tumejipanga kushinda”  alisema Masai.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga alisema bado kazi ni ngumu licha ya mwelekeo kuwa mzuri akiwapongeza vijana kwa kupambana kila mechi.

“Tuwashukuru menejimenti na mashabiki kwa sapoti, kila mmoja anatimiza wajibu wake na kiu yetu ni kuona tunashinda kila mechi ili kurejesha timu Ligi Kuu, ushindani ni mkubwa,”  alisema Mayanga.

Ofisa Habari wa Geita Gold, Samuel Dida alisema licha ya kushuka nafasi ya nne, lakini hawajashuka kimalengo akieleza kuwa mechi nane zilizobaki wanao uwezo wa kushinda.

“Zaidi walio juu yetu wanaenda kukutana ambapo matokeo ya namna yoyote yanaweza kutupa faida sisi, kimsingi tunahitaji michezo ya nyumbani tupate alama tatu,” alisema Dida.

Mtibwa, Mbeya Kwanza na Mbeya City zilikuwa uwanjani jana katika miji mitatu tofauti katika mechi za hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), huku Bigman, Stand United na Songea United zilizopo pia Championship zikisubiri kucheza na Yanga, Simba na Girrafe Academy kukamilisha hatua hiyo ili kuwania kutinga robo fainali ya michuano hiyo inayotoa tiketi ya CAF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *