
LIGI ya Championship inaendelea tena kurindima wikiendi hii, ambapo baada ya jana kuchezwa mchezo mmoja, leo mingine miwili itapigwa kwenye viwanja mbalimbali, huku raundi ya 23 ikitarajiwa kuhitimishwa keshokutwa Jumatatu ya Machi 17, 2025.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, mjini Musoma wenyeji Biashara United wanaoburuza mkiani huku wakitoka pia kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Stand United, watapambana na African Sports yenye kumbukumbu ya kucharazwa mabao 4-1 na Mtibwa Sugar.
Cosmopolitan iliyotoka kuichapa Green Warriors mabao 3-2, itaendelea kusalia kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kucheza dhidi ya Mbuni, yenye kumbukumbu ya kuchapwa mechi ya mwisho kwa bao 1-0 na wapinzani wao kutoka Arusha TMA Stars.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili kupigwa ambapo Songea United iliyochapwa mabao 3-0 na Mbeya City, itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma kucheza na Transit Camp, iliyonyukwa mechi ya mwisho bao 1-0 na Kiluvya United.
Maafande wa Polisi Tanzania walioichapa Geita Gold kwa bao 1-0, watakuwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati kucheza dhidi ya Bigman kutoka Lindi iliyolazimishwa sare ya bao 1-1, nyumbani katika mechi yake ya mwisho na Mbeya Kwanza.
Raundi ya 23, itahitimishwa keshokutwa Jumatatu kwa michezo mitatu kupigwa ambapo Mbeya City itakuwa kwenye uwanja wake wa Sokoine jijini Mbeya kucheza na Kiluvya United, huku Geita Gold ikiwa Nyankumbu mkoani Geita kucheza na Mbeya Kwanza. ‘Chama la Wana’ Stand United yenye morali baada ya kuichapa Biashara United mabao 3-0 katika mechi ya mwisho, itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kucheza dhidi ya vinara wa ligi, Mtibwa iliyoichapa African Sports 4-1.
Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi alisema kwa michezo iliyobakia hakuna timu yenye uhakika wa moja kwa moja wa kupanda Ligi Kuu Bara, kushuka daraja au kusalia hivyo, ugumu huongezeka zaidi kutokana na mahitaji ya kila mmoja wao.