PAMEANZA kuchangamka! ndivyo unavyoweza kusema katika Ligi ya Championship baada ya kubakisha michezo tisa kwa kila timu kuhitimisha msimu huu, huku vita kubwa ikitanda maeneo yote, hususani ile ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao wa 2025-2026.
Wakati raundi hizo zikibakia, Mwanaspoti linakuletea tathimini ya kinachoendelea na kile kinachotarajiwa kutokea mwisho wa msimu huu.

‘TOP FOUR’ PAMECHANGAMKA
Wakati timu mbili zitakazomaliza nafasi ya kwanza na ya pili zikipanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja huku zitakazomaliza ya tatu na nne zikicheza ‘Play-Off’, ushindani umekuwa ni mkubwa kwao kutokana na kutopishana pointi nyingi hadi sasa.
Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, inaongoza ikiwa na pointi 51, ikifuatiwa na Geita Gold zilizoshuka zote pamoja, iliyokusanya pointi zake 45, huku Mbeya City iliyoshuka msimu wa 2022-2023, ikishika nafasi ya tatu na pointi 43.
‘Chama la Wana’ Stand United inayopambana kurejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2018-2019, inashika nafasi ya nne na pointi 43, huku Mbeya Kwanza iliyoshuka pia msimu wa 2021-2022, ikishika nafasi ya tano na pointi zake 38.
BIASHARA KATIKA MTEGO
Vita nyingine ni ya nafasi ya kubaki Ligi ya Championship na hadi sasa ‘Wanajeshi wa Mpakani’, Biashara United ndiyo timu pekee yenye kazi kubwa ya kujinasua, kutokana na kukusanya pointi nne tu katika michezo 21 msimu huu.
Hali ya timu hiyo ilianza kuonekana tangu mwanzoni baada ya kuandamwa na ukata ulioifanya kushindwa kufika katika mchezo wa ugenini dhidi ya Mbeya City uliotakiwa kuchezwa Desemba 3, 2024, hivyo kukatwa pointi 15 na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).
Ili ijinasue na janga la kushuka daraja, Biashara inabidi ishinde michezo yote tisa iliyobakia ili kufikisha pointi 31, ingawa itategemea pia na matokeo ya wapinzani wao, hali inayoonyesha wazi kikosi hicho kiko kwenye hatari ya kushuka.

MTIBWA SUGAR HAIKAMATIKI
Ushindi wa mabao 5-0, ilioupata Mtibwa Sugar dhidi ya Geita Gold Februari 26, 2025, umeifanya kuweka rekodi ya kibabe kwani tangu msimu umeanza, haijawahi kupoteza au kutoka sare mchezo wowote iliocheza kwenye uwanja wa nyumbani.
Mtibwa iliyoshuka daraja msimu uliopita, imecheza michezo 11, kwenye Uwanja wa Manungu Complex kati ya 21 na imeshinda yote, huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 28 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Kwa upande wa Geita Gold, inafuatia baada ya kucheza 11, nyumbani kati ya 21, imeshinda 10 na kutoka sare mmoja, ikifunga jumla ya mabao 27 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.

HAT-TRICK TATU
Msimu huu umekuwa mgumu kwani hadi sasa zimefungwa ‘Hat-Trick’ tatu, akianza mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mchezo dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda mabao 4-0, Desemba 13, 2024.
Andrew Simchimba wa Geita Gold alifunga pia wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akihitimisha katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Biashara United, Februari 23, 2025.
Msimu uliopita, zilifungwa ‘Hat-Trick’ tano huku nyota wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa akifunga mbili, wakati Kika Salum (Pan Africans), Abdulaziz Shahame (TMA FC) na Oscar Mwajanga aliyekuwa Mbeya Kwanza wakifunga moja.

VITA YA UFUNGAJI
Sehemu nyingine yenye msisimko ni katika vita ya ufungaji na hadi sasa anayeongoza ni mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh mwenye mabao 14, akifuatiwa na Abdulaziz Shahame wa TMA na Andrew Simchimba wa Geita Gold wenye 13, kila mmoja.
Wengine ni Naku James (Mbuni) mwenye 11, Yusuph Mhilu (Geita Gold) aliyefunga manane, Boniphace Maganga wa Mbeya Kwanza na Andrew Chamungu (Songea United) wakifunga saba, huku Ramadhan Kapera (TMA FC) na Eliud Ambokile (Mbeya City) wakiwa na sita.
Wengine wenye sita ni Seif Adam (Mbeya Kwanza), Msenda Msenda (Stand United) na Kilaza Mazoea wa Mbeya City, ambao wana kazi ya kuifikia au kuivunja rekodi ya Edgar William aliyekuwa mfungaji bora, wakati akiwa na KenGold aliyoifungia mabao 21.
MAKOCHA WATATU TU
Ni timu tatu tu ambazo hazijabadilisha benchi la ufundi, ikiwa haina tofauti na Ligi Kuu Bara kwani hadi sasa ni Salum Mayanga wa Mbeya City, Leonard Budeba (Mbuni FC) na Kessy Abdallah wa African Sports waliosalia na vikosi hivyo.
Kiluvya United iliyopanda ligi ya msimu huu, Cosmopolitan na Transit Camp zinaongoza kwa kufundishwa na makocha wengi hadi sasa ambao wanafika watatu, huku zingine zote zilizosalia zikifundishwa na wawili.
MSIKIE KESSY
Kocha wa African Sports, Kessy Abdallah anasema michezo iliyosalia ni migumu zaidi tofauti na mwanzoni kwa sababu kila timu inaangalia nafasi iliyopo ili ipiganie malengo iliyoweka, jambo linaloongeza ushindani kutokana na mahitaji hayo.
“Michezo ya mwishoni huwa ni ya hesabu zaidi kwa sababu ukizubaa unajikuta unatoka nje ya malengo yako, kwa mfano sisi African Sports tunachopambania ni kuhakikisha timu inabaki Ligi ya Championship, ili msimu ujao tujipange tena upya.”