
BAADA ya jana kupigwa michezo mitatu ya Ligi ya Championship katika viwanja mbalimbali, leo mechi moja nyingine itapigwa kati ya wenyeji Geita Gold dhidi ya Cosmopolitan, huku macho yakielekezwa zaidi kesho kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Geita Gold iliyotoka kuchapwa mabao 2-0 na Bigman FC mchezo uliopita ugenini, inarudi kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita kuikaribisha Cosmopolitan, yenye kumbukumbu mbaya pia ya kupoteza kwa mabao 2-0, kutoka kwa TMA ya Arusha.
Baada ya hapo, utamu unahamia kesho saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na Mbeya City inayopambana kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Stand United.
Mchezo huo unavuta hisia za mashabiki wengi kutokana na viwango vyao, kwani Mbeya City inashika nafasi ya pili na pointi zake 52, sambamba na ‘Chama la Wana’, Stand United iliyopo ya tatu, ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa tu.
Stand United inapambana pia kurejea Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa Mbeya City baada ya kushuka msimu wa 2018-2019, jambo linaloongeza mvuto wa mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki kuona kitakachojiri huko kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, zilitoka sare ya kufungana kwa mabao 3-3, Novemba 24, 2024, hivyo huenda na huu pia ukashuhudia mabao mengi yakifungwa, kutokana na ubora wa timu zote mbili.
Mbali na mchezo huo, kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbeya Kwanza iliyoichapa Polisi Tanzania bao 1-0, itaikaribisha maafande wa Transit Camp, yenye kumbukumbu mbaya ya kuchapwa mechi ya mwisho na Mbeya City kwa mabao 3-2.
Keshokutwa, Jumatatu utapigwa mchezo mmoja na Kiluvya United iliyochapwa mabao 2-1, dhidi ya Songea United, itasalia kwenye Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani kuikaribisha Bigman FC, yenye kumbukumbu ya kuichapa Geita Gold mechi ya mwisho 2-0.