
Chama tawala nchini Senegal, PASTEF, kimeshinda karibu robo tatu ya viti vya Bunge katika uchaguzi uliofanyika wikendi iliyopita, matokeo yanayomaanisha kuwa sasa sera za Serikali mpya zitapitishwa kirahisi.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali, chama cha rais Bassirou Faye kimepata wabunge 130 kati ya 165 wanaotakiwa katika bunge la kitaifa, matokeo yaliyothibitisha na maofisa wa chama tawala.
Matokeo haya hata hivyo yatasalia kuwa ya awali hadi pale yatakapothibitishwa na mahakama ya kikatiba ndani ya siku 5 zijazo.
Ikiwa ushindi huu wa chama cha Pastef utathibitishwa na mahakama, utakuwa ushindi mkubwa zaidi katika historia ya chaguzi za taifa hilo kwa chama kimoja kufikisha wabunge zaidi ya 120.
Mrengo wa upinzani uliokuwa ukiongozwa na rais wa zamani Macky Sall, umeambulia wabunge 16, huku chama cha waziri mkuu wa zamani Amadou Ba kikipata viti 7 na viti vitatu vikienda kwa aliyekuwa meya wa Dakar Barthelemy Dias.
Septemba mwaka huu Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye alivunja bunge la nchi hiyo linaloongozwa na upinzani na kuitisha uchaguzi wa mapema ili kumaliza mvutano kati ya bunge na serikali.