Chama la Wana yashtuka, yasuka pacha ya mabao

KOCHA wa Stand United ‘Chama la Wana’, Juma Masoud amesema kwa sasa anatengeneza safu kali ya ushambuliaji katika timu hiyo itakayozungukwa na nyota, Msenda Amri Msenda na Omary Issa ‘Berbatov’, kutokana na kiwango bora wanachokionyesha.

Nyota hao wawili kwa pamoja wamefunga mabao 10 kati ya 29, yaliyofungwa na timu nzima na Msenda Msenda amefunga sita huku kwa upande wa Omary Issa ‘Berbatov’, akifunga manne na kuendelea kuweka hai matumaini ya kuirejesha Ligi Kuu Bara.

“Nimekaa nao kwa muda mfupi na kwa hakika wanafanya kazi nzuri sana katika eneo la ushambuliaji, ukiangalia mwenendo wao unaridhisha ila nahitaji kuwatengeneza wawe pacha bora kikosini kwetu, kwani ndio tunaowategemea hadi sasa,” alisema.

Masoud alisema licha ya wachezaji wengi kusajiliwa bila ya mapendekezo yake ila ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wao, huku akiweka wazi uzoefu na ushirikiano anaoupata kutoka kwao na viongozi utatimiza malengo ya kuirejesha Ligi Kuu.

Kocha huyo wa zamani wa FGA Talents kwa sasa Fountain Gate, amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliyejiunga na Songea United, huku akiipambania kuirejesha Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2018-2019.