
LICHA ya Stand United ‘Chama la Wana’, kuchapwa kwa mabao 8-1, dhidi ya Yanga katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), kocha wa kikosi hicho, Juma Masoud amesema kichapo hicho hakijawaharibia malengo yao ya msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Masoud alisema licha ya kuruhusu mabao mengi alikaa na wachezaji na kuwataka kusahau yote yaliyotokea, kisha wawekeze nguvu katika michezo yao mitatu ya Ligi ya Championship iliyobakia ili kutimiza malengo yao.
“Hatuwezi kuangalia matokeo ya nyuma kwa sababu tayari mchezo ule ulishapita, tulicheza na timu yenye wachezaji bora na licha ya kupoteza kuna vitu vingi kimbinu vimetusaidia na tunavifanyia kazi kwa michezo iliyobakia,” alisema Masoud.
Masoud alisema gepu la pointi moja na Mbeya City iliyopo nafasi ya pili sio kubwa, japo anachopambana nacho ni kuongeza umakini katika safu ya ulinzi ya timu hiyo, licha ya kukiri ugumu wa kuwania pointi tisa kwa michezo mitatu iliyobakia.
Baada ya kushinda 5-1 dhidi ya Green Warriors, Stand inashika nafasi ya tatu na pointi 58, baada ya kucheza michezo yake 27, ikishinda 18, sare minne na kupoteza mitano, nyuma ya Mbeya City yenye pointi 59 na vinara wa ligi, Mtibwa Sugar yenye 66.