
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uwezeshwaji wa wanawake katika nyanja mbalimbali, ikiwemo masuala ya uongozi, utasaidia kuongeza na kuimarisha nguvukazi ya nchi kwa kuwa wao ni wabeba maono ya Taifa.
Chalamila anasema hatua hiyo ni muhimu kwani idadi yao (wanawake) ni kubwa kuliko wanaume na pia uwezo wanaouonyesha wanapopata nafasi mbalimbali ni mkubwa.
Amebainisha hayo leo, Februari 21, 2025, wakati wa hafla ya miaka 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi inayoendeshwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa ushirikiano na Serikali ya Norway na wadau wengine.
Hafla hiyo pia imehusisha mahafali ya 10 ya wahitimu takribani 110 waliopatiwa mafunzo hayo ya uongozi.
Programu hiyo ya Mwanamke Kiongozi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuwaongezea ujuzi wanawake katika uongozi katika sekta mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila amesema wanawake ni watu waliobeba maono makubwa ya taifa, hivyo uwepo wa programu zinazowawezesha unasaidia kutafsiri maono hayo.
“Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, asilimia tatu ya wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam ni wajane, hivyo kuwepo kwa programu kama hizi kunasaidia kuwainua na kuweza kutunza familia zao vizuri,” amesema.
Pia amegusia changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake, akisema uwezeshwaji wa idadi kubwa ya wanawake, utasaidia kupunguza matendo hayo katika jamii.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba, amesema katika muongo mmoja wa programu hiyo, washiriki 493 kutoka sekta ya umma na binafsi wamepata mafunzo ya uongozi.
Amesema miongoni mwa waliofikiwa na programu hiyo ni wabunge takribani 150 kutoka Bara na Visiwani, na hivyo kufanya idadi ya watu waliopata mafunzo hayo kufikia 643.
“Kati ya waliohitimu mafunzo, 102 wamepata nafasi za uongozi na kuongezewa majukumu, 56 wamepata nafasi katika bodi, na 16 kupata fursa ya kuongoza taasisi mbalimbali.”
Ameelezea mpango wao wa kupanua wigo wa mafunzo hayo ili kuwafikia wanawake zaidi, na sasa mazungumzo yanaendelea ili kuwafikia maofisa wa jeshi wanawake.
“Tunaomba wadau mbalimbali kuendelea kutuunga mkono ili programu hii iweze kuwafikia wanawake wa kada mbalimbali,” anaeleza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Uongozi cha Esami, Dk Peter Kiuluku, amewapongeza wahitimu hao 110 kwa kufaulu vizuri licha ya majukumu mbalimbali yanayowakabili.
“Hongereni sana kwa kuweza kuyamudu yote—kuhudumia familia, majukumu ya kazi, na bado mkatenga muda kwa ajili ya kusoma na kufanya vizuri masomo yenu,” amesema.
Pia amewataka wahitimu hao kutumia maarifa waliyoyapata kuongeza ufanisi katika shughuli zao za uongozi.