Chalamanda: Yanga? Tutajuana huko huko!

KIPA wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda amesema pamoja na ugumu wa mechi dhidi ya Yanga, lakini kutokana na uhitaji wa pointi tatu ’watakufa na mtu’ hadi kieleweke.

Kagera Sugar haina matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi 11 katika msimamo wa Ligi Kuu, ambapo Jumamosi itakuwa kibaruani kuikabili Yanga.

Yanga ambayo imetoka kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya mwisho ilishinda mabao 5-0 dhidi ya Copco FC kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, Kagera Sugar inakutana na bingwa huyo mtetezi ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ya duru la kwanza kwa mabao 2-0 walipokutana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Chalamanda aliliambia Mwanaspoti kuwa, hawana matokeo mazuri hivyo mechi yoyote kwao ni vita ya pointi tatu na Yanga lazima kieleweke katika kupambania timu kubaki Ligi Kuu.

Alisema wanafahamu mechi hiyo itakuwa ngumu na upinzani mkali, lakini watakuwa makini na kila mchezaji kuhakikisha wanafikia malengo yao akiwaomba wenzake kukaza dakika zote 90.

“Hatumkabi mmoja, tutaangalia watakaoanza ndio tutakomaa nao, itakuwa ni mtu na mtu, hatuko salama na ndio tunaianza raundi ya pili hivyo juhudi zetu ndizo zitatuacha salama,”  alisema Kipa huyo.

Nyota huyo aliongeza kuwa, pamoja na kutoanza msimu vyema, lakini wanayo matumaini makubwa kwa wachezaji wapya waliojiunga na timu hiyo dirisha dogo kuweza kuongeza nguvu kikosini.