
Dar es Salaam. Wakati viongozi wa Chadema wakiendelea kuinadi kampeni ya ‘No Reforms No Election’ katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, chama hicho kimewaita walioomba (watia nia) wa nafasi mbalimbali kwenye kikao maalumu cha kujadili hali ya kisiasa.
Kikao hicho kitakachofanyika Aprili 3, 2025 katika ofisi za makao Makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam, kitawahusu pia wanachama wote ambao walikuwa wagombea wa nafasi za ubunge katika Uchaguzi Mkuu 2020.
Kwa mujibu wa waraka wa wito uliondikwa Machi 24, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa ambao Mwananchi imeuona, walioitwa ni waliotia nia ya kuwania ubunge kwa mujibu wa tangazo la Katibu Mkuu (John Mnyika), lilivyoelekeza kuhusu kutia nia.
Golugwa amesema kikao hicho kitawakutanisha watia nia na viongozi wakuu wote wa chama hicho, kujadili hali ya kisiasa na mwenendo wa Chadema katika kudai uchaguzi huru wenye kuaminika.
“Kikao hiki ni cha muhimu sana na wahusika wote wahudhurie,”amesisitiza Golugwa katika wito huo aliouelekeza kwa makatibu wa kanda 10 za Chadema, wakitakiwa kuushusha kwa makada wao.
Tayari makatibu wa kanda wameshusha wito huo, wakiwaelekeza wahusika kuhakikisha wanapohudhuria wanavaa sare za kombati zenye rangi ya kaki.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia alimethibitisha leo Machi 25, 2025 kuhusu uwepo wa kikao hicho, akisema kitahusisha pia watia nia wa udiwani.
“Lengo ni kuzungumzia na kuwafundisha No Reforms No Election, tutaanza na watia nia ya ubunge na baadaye udiwani,” amesema Rupia.
Wito huo unakuja kukiwa na sintofahamu miongoni mwa makada wa chama hicho juu ya ama wanaendeleaje na maandalizi yao ya kugombea katikakati ya kampeni ya “hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi”.
Hali hiyo inakolezwa na ukweli kwamba baadhi ya makada wa chama hicho, walishajipanga na kuwekeza kwa ajili ya kuwania ubunge na udiwani, lakini kutokana na msimamo ajenda hiyo mpya ya chama, wamejikuta wakibaki njiapanda.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa, waliozungumza na Mwananchi wamebashiri kuwa huenda kikao hicho kikawa njia ya kuwataka watia nia hao waendelee kujiandaa na mchakato wa uchaguzi kabla ya kipenga hakijapulizwa.
Mwananchi inazo taarifa kwamba baadhi ya watia nia wa chama hicho, wanafikiria kusaka vyama mbadala, ili kutimiza ndoto zao, baada ya kuona chama hicho, kikishikilia msimamo wa ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’, ingawa mara zote kimesisitiza hakitasusia uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba bali kitauzuia.
Mmoja wa viongozi wa Chadema aliyezungumza na Mwananchi (jina linahifadhiwa kwa kuwa si msemaji) amesema, wapo watia nia wengi wanatafuta vyama vya kugombea ili kutimiza malengo yao ya kisiasa kwa sababu walishajiandaa.
“Kwa hiyo tunawawahi kuongea nao, ili kuwaambia wasijali na kwamba watagombea na wasikimbie chama,” amesema kiongozi huyo.
Kwa sasa Chadema inaendelea kunadi kwa wananchi ajenda yake ya No Reforms No Election ambapo viongozi wakuu wapo Kanda ya Nyasa yenye mikoa ya Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe na Songwe.
Lengo la ajenda hiyo ni kuushawishi umma kuishinikiza Serikali ifanye mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili haki sawa itende kwa vyama vyote.
Mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza amesema chama cha siasa hufanya siasa kwa mikakati, hakiwezi kusema hakishiriki uchaguzi wakati hakina mgombea.
“Ninachokiona hapa, kaulimbiu ya No Reforms No Election haizuii chama kufanya maandalizi ya uchaguzi, watakuwa na wagombea udiwani na ubunge, wakati huo wanashinikiza mabadiliko.
“Watu wanaowaunga mkono wagombea hatua ya mwisho ni kupiga kura kwa wagombea wanaotaka mabadiliko. Wanacheza na pande mbili huku wanashinikiza huku wanaandaa wagombea, ndivyo siasa zinavyofanyika,” amesema Kaiza.
Kaiza amesema hatua ya mwisho ni watu wanaotaka mabadiliko kuwapigia kura wagombea wenye sera hiyo, ili kuwaondoa walioko madarakani.
“Huenda katika kikao hicho, watia nia hao wakaambiwa waanze maandalizi, wajiandae na kuendelea kutafuta uungwaji mkono ili ikifika mwisho kama Serikali haijafanya mabadiliko, basi wapigiwe kura nyingi zitakazowawezesha kushinda ubunge na udiwani ili kuleta mabadiliko,”amesema.
Naye, mchambuzi mwingine Ali Makame Issa, amesema, “Huenda kuwaita watia nia hao ni hofu iliyopo kwamba wakiendelea na msimamo wa No Reforms No Election, basi watia nia watakwenda kutafuta vyama vingine ili kushiriki uchaguzi,”
“Ninachofikiria Chadema watapata mawazo ya wagombea wao kuhusu No Reforms No Election na kusikiliza watakachokisema watia nia wao. Ikitokea wakawalazimisha kuendana na msimamo huo, kuna wengine watakimbia na kuhamia vyama vingine,” amesema Issa.