
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, kimemwandikia barua Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Mwanga, Lembruce Mchome kikimtaka ajieleze ndani ya siku 14 kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu.
Mchome ameingia kwenye mgogoro na chama chake baada ya kuhoji uhalali wa akidi ya kikao cha Baraza Kuu ambacho kilichothibitisha uteuzi wa viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Februari 18, 2025, Mchome aliandika barua ya malalamiko kwa katibu mkuu akipinga uteuzi uliofanywa na mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, wa viongozi wa juu wa chama na wajumbe wa kamati kuu kwenye mkutano wa Baraza Kuu Taifa uliofanyika Januari 22, 2025.
Kada huyo ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu alipeleka nakala ya barua hiyo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na baada ya ukimya wa siku kadhaa, alikwenda kulalamika kwa Msajili, akitaka majibu ya barua yake na Msajili aliielekeza Chadema imjibu ndani ya wiki moja, kabla ya Machi 31, 2025.
Baada ya tamko la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alizungumzia sakata hilo, akisema kikao husika kilizingatia akidi ya asilimia 50 inayotakiwa kwa ajenda za kawaida, ambazo hazihusiani na uchaguzi.
Leo, Machi 26, 2025, Ofisi ya Katibu wa Chadema Kilimanjaro imemwandikia barua Mchome kwa mujibu wa katiba ya chama ya mwaka 2006 toleo la 2019, Maadili ya Viongozi 10.1(vi), 10.2 (ix) na Maadili ya Wanachama 10.3 (iii) ikimtaka maelezo.
Mchome amekiri kuipokea barua hiyo iliyosainiwa na Basil Lema, katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro ambayo licha ya kudai ni ya vitisho, amesema ni mapema kuizungumzia kwa sasa, bali anahitaji muda wa kutafakari zaidi nini cha kufanya kwa kushauriana na wakili wake.
“Ni kweli nimepokea barua kutoka kwa katibu wa mkoa pamoja na ujumbe wake wa vitisho dhidi yangu na yote haya nimepokea kwa njia ya WhatsApp na kwamba ananipa siku 14 nitoe maelezo yangu.
“Bado ni mapema kusema lolote kwa kuwa ndio nimepokea leo, nitatafakari nini cha kufanya kwa kupitia katiba yetu ya chama lakini pia naamini wakili wangu atanishauri vema,” amesema Mchome.
Katika barua hiyo ambayo Mwananchi imeiona, Lema amemweleza Mchome kwamba akiwa kiongozi katika chama anatakiwa aonyeshe mwenendo unaoakisi taswira ya chama kwa kuwa mkweli, mtiifu na imara katika kutekeleza wajibu wake na ulinzi imara wa Katiba ya chama.
“Katika siku za karibuni, umenukuliwa ukitoa maneno yenye kuogofya na ukakasi mwingi katika chama. Mathalan, barua yako ya kulalamikia akidi ya kikao cha Baraza Kuu cha Januari 22, 2025 ilivujisha shutuma hizo kwa maadui wa chama (Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ulimpa nakala).
“Unajua wazi kuwa watu hawa ni mahasimu wa chama na ya kwamba kila wakati wanatutafutia makosa ili kukidhuru chama chetu. Lakini wewe kwa makusudi mazima umempasia mpira, tena ndani ya 18 dhidi yetu,” amesema Lema katika barua hiyo.
Lema amemtaka Mchome kutoa utetezi wake ndani ya siku 14 akieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu ikiwemo kuvuliwa uongozi na uanachama.
Katika barua hiyo, Lema amemuonya Mchome kwamba kutopeleka majibu kwa wakati hakutazuia Baraza kutumia mamlaka yake dhidi yake.
“Kwa barua hii ninakutaka ulete utetezi wako kwangu ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya barua hii, ukitoa sababu ni kwa nini Baraza la Uongozi la Mkoa lisikuchukulie hatua kali za kinidhamu, ikiwepo kuondolewa kwenye nafasi zako za uongozi na pia kukufutia uanachama.
“Kumbuka kwamba kitendo cha kutoleta majibu yako kwa wakati uliopewa katika barua hii hakitalizuia Baraza la Uongozi kuendelea na kutumia mamlaka yake kikatiba dhidi yako,” imesema barua hiyo.