Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kuvutana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa kutotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria.

Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika akiwaonyesha waandishi wa habari,wanachama wa chama hicho waliokamatwa na polisi na kwenda kutelekezwa katika pori la Pande Bagamoyo.
Tangu kukamatwa kwa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu akiwa anahutubia Kampeni ya No reforms, no election, Mbinga mkoani Ruvuma na hatimaye kufunguliwa kesi ya uhani, kumeibuka matukio kadhaa yaliyosababisha mvutano baina ya viongozi wa Chadema na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Saalam.

Kesi hiyo tayari imeshatajwa mara mbili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiendeshwa kwa mtandao huku Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likitoa taarifa kwa watu kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwamo kuzuiwa kufika Mahakama ya Kisutu, likidai kwa sababu za kiusalama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 30, 2025, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amedai Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliroametoa taarifa za uwongo za watu waliowakamata Aprili 24, 2025 maeneo ya Mahakama ya Kisutu wakati wa usikilizwaji wa kesi ya Lissu.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi leo kuhusu madai ya kusema uwongo, Muliro alicheka tu, pasi kutoa majibu.
Akiendelea kuzungumza na waandishi, Mnyika amelitaka Jeshi la Polisi kumchukulia hatua za kinidhamu kamanda huyo ikiwamo ya kumwondoa kwenye nafasi hiyo.

Chadema pia wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura kutoa tamko la wazi la kukana au kuthibitisha iwapo vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanachama wao vinafanyika kwa baraka zake.
“Chama kimeshawasilisha malalamiko katika taasisi mbalimbali za haki za binadamu za kimataifa kuhusu matukio haya,” amesema Mnyika.
Aidha, ametoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la Aprili 24, 2025 ambalo analitaja kuwa, miongoni mwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Tunamwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua dhidi ya Kamanda Muliro, kwa sababu kasema uongo kuhusu matukio haya,” amedai katibu huyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo huku akionesha matukio kwa picha mjongeo waliyofanyiwa wanachama, amedai Muliro lazima achukuliwe hatua kwa kuwa aliongoza shughuli ya ukamataji huo.

Polisi wakiwa ndani ya gari lao wakiwa katika majukumu yao ya kuimarisha ulizi katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 28, 2025.
Amedai jumla ya wanachama wao 25 wamefanyiwa ukatili ambao haupaswi kufumbiwa macho huku akidai wamevunjwa miguu na mikono lakini taarifa ya jeshi la Polisi haikuwataja.
“Tunamshangaa kamanda Muliro kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo juu ya yale yaliyotokea Aprili 24, 2025, kuwa viongozi waliokamatwa ni wawili tu, John Heche na mimi Katibu Mkuu John Mnyika, kuna watu wengi walikamatwa na hawakutajwa kwenye taarifa ya jeshi la Polisi,” amedai Mnyika.
Amedai kuwa, kitendo cha mtu aliyechukuliwa na Jeshi la Polisi kushindwa kutajwa kwenye taarifa kuonesha amekamatwa ni ishara ya kuficha ukweli na kwa maana nyingine huyo ni nia ovu.
“Kwa kuwa kamanda Muliro amesema uongo tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania kama haya matendo hayana baraka zake, ajitokeze atoe taarifa kwa umma juu ya matukio ya watu kupigwa, kuteswa na kuumizwa na kutajwa idadi halisi na kuwajibika,” amesema katibu huyo.
Muliro ajibu mapigo
Akizungumzia madai kuwa, makada wa Chadema wamekamatwa, Muliro amesema hajasikia malalamiko hayo wala hajapelekewa rasmi huku akisisitiza jeshi hilo litaendelea kusimamia sheria katika kuhakikisha ulinzi unaimarishwa wakati wote ndani ya Dar es Salaam.
“Bado sijasikia lolote ila nasisitiza tutaendelea kusimamia sheria na kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa salama na kuzifanya kazi zetu zote kwa mujibu wa sheria,” amejibu Muliro.
Hata hivyo, Mnyika amesema wameamua kutangaza mikakati sita ya kupinga kile wanachokiita ukandamizwaji unaofanywa na polisi wakiongozwa na Muliro.
Mnyika ametaja hatua wanazokwenda kuchukua kuwa ni kumfungulia mashitaka binafsi kamanda Muliro.
Ratiba ya No reforms no election
Mnyika amesema pamoja na kuendelea na kesi ya Lissu mahakamani, mikutano ya kampeni ya No reforms no election itaendelea na safari hii inahamia Kanda ya Victoria.
“Ratiba mpya mikutano itaendelea kuanzia Mei 8 hadi 12, 2025 sasa tunaenda Kanda ya Victoria inayounda mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza na kuanzia Mei 13 hadi Mei 17, 2025 tutakwenda Kanda ya Serengeti mikoa ya Mara, Simiyu, na Shinyanga,” amesema.
Amesema mikutano hiyo wataifanya kama ushahidi pamoja na madhila wanayofanyiwa kamwe hawawezi kuacha kuunganisha Watanzania kupigania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
“Kampeni hii inalenga kutoa elimu kwa umma kushinikiza Serikali kuweka mifumo mizuri ya uchaguzi ili ufanyike kwa huru na haki,” amesema Mnyika.
Kampeni hiyo ilizinduliwa Machi 23 mwaka huu, Kanda ya Nyasa inayounda na mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa.

John Pambalu akisimulia namna alivyokamatwa na polisi siku ya kesi ya Mwenyekiti wa Chadema,Tundu Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Baadaye iliendelea Kanda ya Kusini inayounda na mikoa mitatu, Ruvuma, Lindi na Mtwara kisha iliingia Kanda ya Pwani yenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Kada wa Chadema, Emmanuel Sunday amesema mikutano hiyo ilikuwa na hamasa kubwa na watu wengi wanajitokeza.
“Ni wazi wanahitaji mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili wapate wawakilishi wao wazuri watakowasemea matatizo yao,” amesema Sunday.