Shinyanga. Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amelaani vitendo vya utekaji wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema katika Kanda ya Serengeti.
Akizungumza leo Machi 29, 2025, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya Kanda Maalum ya Chadema, Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, ameeleza kuwa vitendo vya utekaji vinavyoendelea vimezua hofu kubwa miongoni mwa wananchi. Kanda ya Serengeti inayounganisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga.
Mnyawami amesema kuwa hali hii imesababisha wasiwasi, huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha usalama na utulivu katika kanda hiyo.
Akizungumza leo Machi 29, 2025 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya kanda maalum ya Chadema, Mnyawami amesema vitendo vya utekeji vinavyoendelea vimeleta hofu na wasiwasi kwa wananchi. Kanda hii inahusisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga.
“Matukio hayo mawili yalihusisha kiongozi wa hamasa katika Jimbo la Tarime Vijijini, Mussa Juma (Tall) na mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Daniel Chonchorio ambaye ni mtia nia jimbo la Tarime Mjini, utekaji huu unaweka wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi,” amesema Mnyawami.
Mnyawami amesema, “Pamoja na Jeshi la polisi kukanusha katika taarifa zao… kujua watu hao walipo, tunaamini wanapaswa kuwajibika kutokana na jukumu la kisheria waliopewa kuhakikisha upatikana wa watu hao”

Mnyawami ameendelea kwa kusema kuwa anaelekeza Mkoa wa Mara kuanza kuratibu maandamano ya amani kwa madhumuni ya kupinga ukatili wa haki za binadamu, yatakayo hudhuriwa na viongozi wote pamoja na wanaCCM wanaalikwa kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu,
“Tunaelekeza Mkoa wa Mara kuanza kuratibu maandamano ya amani ambayo yatahudhuriwa na viongozi wa kanda, pia waanze kutoa taarifa polisi na lengo kubwa ni kupinga utekaji unaoendelea mkoani Mara na tunawakaribiasha wanaCCM wote ambao ni waathiriwa wa utekaji kupaza sauti zao” amesema Mnyawami.
Amesisitiza kuwa Chadema Kanda ya Serengeti inataka kurejesha amani ambayo imetoweka kwa wananchi, pamoja na kurejesha imani ya wananchi ambayo imetoweka kwa Jeshi la Polisi.
“Tunaomba Jeshi la Polisi kuwajibika kwa kushindwa kulinda usalama wa raia, Rais Samia Suluhu Hassan aunde tume ya kijaji kuchunguza matukio ya utekaji na kuharakisha utekelezaji wa ripoti ya haki jinai ambayo ilionesha vyombo vya ulinzi na usalama kuvunja kwa haki za binadamu” amesema Mnyawami.
Amewasihi wadau wa haki za binadamu na wananchi kupaza sauti dhidi ya vitendo viovu, ikiwamo kukutana na viongozi wa dini kuwaeleza umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na idadi ya wananchi waliouwawa.