
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelaani kitendo cha polisi kumshikilia mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu aliyekamatwa jana Jumatano, Aprili 9, 2025 mkoani Ruvuma.
Chadema imedai hatua ya kumshikilia Lissu na viongozi wengine ni njama za kuzuia chama hicho, kuwaeleza Watanzania kuhusu mwenendo wa uchaguzi. Hata hivyo, kimesema licha ya Lissu kushikiliwa na polisi, kampeni ya ‘No Reforms, No Election’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) haitasimama.
Lissu anayedaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma muda mchache baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mbinga.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Aprili 10, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani Songea mkoani Ruvuma, akisema Lissu na viongozi wakuu wa chama hicho, wamejikita kuelimisha umma kuhusu No Reforms, No Election .
Katika mkutano huo, Heche amedai polisi ilitumika nguvu kubwa kumkamata Lissu badala ya kutumia taratibu za kawaida, kwa sababu mwenyekiti huyo ni kiongozi mkubwa wa chama hicho.
“Lissu ni kiongozi ambaye wangemwita kwa muda ambao wangekubaliana, lakini kwenda kumkamata kwa kupiga mabomu kwa mtu mmoja ambaye hali yake inajulikana sio sawa,” amesema Heche.
Katika purukushani za kumkata Lissu, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wanazuia utekelezaji wa majukumu yao.
Mkutano wakatishwa
Wakati Heche akiendelea na mkutano huo, polisi walizingira ofisi hiyo na kuingia katika chumba cha mkutano, wakimtaka kiongozi aache kuzungumza na wanahabari afuatane nao kuelekea kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema:“Mkutano wa Heche haukumalizika baada ya kutakiwa kwenda kwa RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa), jambo ambalo makamu mwenyekiti amelitii,” amesema Rupia.
Hadi sasa bado haijafahamika chanzo cha Lissu kushikiliwa na polisi, ingawa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya aliliambia Mwananchi yupo katika ufuatiliaji kuthibitisha kuwepo kwa taarifa hizo, akiahidi leo kuuelezea umma kuhusu tukio hilo.
Kauli ya TLS
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi ametumia ukurasa wake wa kijamii wa X kuzungumzia tukio hilo. Akiandika, “tunafuatilia kujua nini kimejiri na kwa nini nguvu kubwa kiasi kile ikatumika eneo ambalo Chadema na wananchi walikuwa wakitumia haki yao ya kujumuika kwa kufuata sheria.
Nguvu iliyotumiwa na Polisi dhidi ya raia wasiokuwa na silaha yeyote siyo tu matumizi mabaya ya sheria, bali ni hali inayoashiria kutokuwajibika na kukosekana kwa ustahimilivu wa kisiasa katika Taifa letu.
Amefafanua zaidi katika andiko hilo kuwa, “kulikuwa na namna nyingi za kiueledi ambazo zingeweza kufanyika bila rabsha wala risasi au mabomu ya machozi. Tundu Lissu siyo tu kwamba ni mwanachama na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani huyu pia ni mwanachama hai wa TLS, na ana haki ya kutendewa kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la Polisi litoke na kutueleza sababu za kutumia nguvu ile dhidi ya raia na kwamba Tundu Lissu anashikiliwa kwa kosa gani. Tunafuatilia na kutafakari kuhusu jambo hili.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi