Chadema yaja na vuguvugu la mabadiliko

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanzisha vuguvugu la mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kimesema sasa kinakwenda kutekeleza kaulimbiu yake ya “Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi” kwa lengo la kushinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi nchini.

Vuguvugu hilo litahusisha mikutano ya hadhara nchi nzima na kushirikisha wadau tofauti wakiwamo viongozi wa dini, jumuiya ya kimataifa, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi wote katika maeneo yao.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Februari 12, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakati akihutubia Taifa, ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu achaguliwe mwenyekiti mpya wa chama hicho Januari 21, 2025.

Lissu amesema kwa muda mrefu, mfumo wa uchaguzi wa Tanzania umekuwa hautoi haki kwa vyama vya upinzani badala yake imekuwa inakipendelea chama tawala cha CCM. 

Lissu amesema chaguzi zilizopita zimeonyesha “uchafuzi mkubwa” katika hatua zote kuanzia wakati wa uteuzi wa wagombea, wakati wa kampeni, upigaji kura na utangazaji wa matokeo, hivyo hawaoni haja ya kuwepo kwenye uchaguzi kwa kuwa bado mazingira ni yaleyale.

“Kila mtu ajiulize, tukienda kwenye uchaguzi wa Oktoba 2025, tutegemee nini kwa Tume hii ambayo iliengua wagombea wetu katika chaguzi zilizopita? Watu walewale ndiyo tunaotarajia watutendee haki?” amehoji Lissu.

Amesema changamoto hizo zimeitafakarisha kamati kuu na kuamua kwamba; “bila mabadiliko hakuna uchaguzi” na kuwa kazi iliyo mbele yao ni kuhakikisha wanashinikiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini.

“Msimamo wetu ni kwamba ‘Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’. Hatuzungumzii kususia uchaguzi, hatutasusia uchaguzi, tutakwenda kuwaambia Watanzania, tutauambia ulimwengu kwamba CCM haitaki kufanya mabadiliko ili kuwa na uchaguzi huru na haki, hivyo uchaguzi usifanyike kabisa,” amesema Lissu.

Katika kutekeleza mkakati huo ulioridhiwa na Baraza Kuu na mkutano mkuu wa Chadema, Lissu amesema wamepanga kuzungumza na kila mmoja katika jamii kuhusu jambo hilo, ili kuunganisha nguvu na makundi mengi ya jamii.

Na amewaomba viongozi wa dini kuwa sehemu ya harakati hizo kwa kuwa kuna mifano kutoka nchi za jirani inayoonyesha viongozi wa dini walikuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao, akiitaja Kenya kama mfano, kuwa wakati wa harakati za kupigania katiba mpya, walikuwa na mchango mkubwa.

“Natoa wito kwa viongozi wetu wa dini; maaskofu wetu, masheikh wetu, wachungaji wetu, watuunge mkono katika hili, mambo yakiharibika, yataharibika kwao pia. Wasikubali kuambiwa wasijihusishe na siasa, kazi yao kuwaombea wananchi,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema vyama vya siasa navyo vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanawezesha chaguzi hizo kuwa huru na haki, hivyo amevitaka kushirikiana na Chadema katika vuguvugu hilo.

“Wale wanaosema lazima tushiriki uchaguzi kwa vyovyote vile, mjiulize, unategemea nini? Kama unataka kugombea ubunge kwenye mazingira haya, jiulize, unategemea nini?” amesema Lissu kwenye hotuba yake hiyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akilihutubia Taifa kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Lissu mwenye umri wa miaka 57 sasa, amebainisha kwamba watazishirikisha jumuiya za kimataifa katika vuguvugu hilo la mabadiliko na wataziomba nchi zenye nguvu kutumia ushawishi wao kwa Tanzania kushinikiza mabadiliko hayo.

“Natoa wito kwa marafiki wa Tanzania, jumuiya ya kimataifa, watuunge mkono. Tutatumia kila njia kufikisha ujumbe kwa kila Balozi aliyepo hapa nchini, tutazungumza na serikali zao na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa,” amesema.

Mwenyekiti huyo aliyechukua nafasi ya Freeman Mbowe, amesema watazishirikisha pia asasi za kiraia katika mapambano hayo kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika kupigania haki na demokrasia.

“Funzo ambalo tumelipata kutoka kwa jirani zetu ni kwamba asasi za kiraia na wanachama wao, zikiungana zinakuwa ni jeshi kubwa. Tunaomba waungane nasi katika harakati hizi za kudai mabadiliko,” amesema.  

Lissu hajawasahau Watanzania, amewaomba kujiunga na chama hicho ili kuongeza nguvu katika mapambano ya kudai haki katika mifumo ya uchaguzi aliyodai siyo rafiki hasa kwa vyama vya upinzani.

“Ombi langu kwa watu wote, mahali popote mlipo, mnaotaka kujiunga na hili jeshi kubwa la ukombozi, tukapiganie mabadiliko haya. Mahali popote mlipo, mnaotaka kujiunga na Chadema ili kushiriki harakati hizi, naomba niwakaribishe mjiunge na chama hiki.

“Watalaamu wetu wanasema utaratibu wa kujiunga umerahisishwa kwa kujiunga kwa mtandao kuliko ilivyokuwa siku za nyuma, wale wanaotaka kujiunga na jeshi hili, nawakaribisha ili tuwe wengi zaidi, jambo likiwa la wengi linakuwa la Mungu,” amesema Lissu.

Hata hivyo, Lissu amesema kazi ya kudai haki katika mifumo ya uchaguzi inahitaji kujitolea na kwenda kila mahali kufanya mikutano ya hadhara na ya ndani, amewaomba wadau na wanachama wa Chadema kujitolea kwa michango mbalimbali ili kufanikisha mchakato huo.

Kutokana na umuhimu wa jambo hilo, amesema viongozi wakuu wa chama watakwenda katika kanda 10 za chama hicho kuzungumza na Watanzania kuhusu kaulimbiu ya Chadema ya “bila mabadiliko hakuna uchaguzi”.

Heche amvaa Wasira

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Bara, John Heche, amemvaa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Stephen Wasira huku kikisisitiza kwamba tangu nchi ipate uhuru hakuna kilichofanyika.

Kauli hiyo ya Chadema ni muendelezo wa majibizano kati ya Chadema na Wasira ambaye hivi karibuni alijibu mashambulizi ya chama hicho akisema CCM imefanya mambo makubwa ya kimaendeleo.

Januari 18, 2025, Wasira alichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kuwa Makamu mwenyekiti amefanya ziara Geita, Dar es Salaam, Mara na jana Jumanne, alimaliza ziara yake mkoani Mwanza.

Katika maeneo hayo, Wasira amekuwa wakitupa ‘vijembe’ kwa Chadema kwamba wamemaliza uchaguzi wao wakiwa mafungu mafungu baada ya Tundu Lissu kuibuka mshindi wa uenyekiti dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea nafasi hiyo.

Januari 3, 2025, Wasira akiwa Bunda Mjini alisema kutokana na maendeleo waliyoleta ikiwemo ujenzi wa miundombinu kinajivunia na hakina mpango wa kuondoka madarakani kwa sasa.

“Nashangaa watu wanaohoji CCM imefanya nini kipindi cha miaka 60 ya uhuru, kipindi tunapata uhuru tulikuwa na barabara tatu tu zote zilikuwa zinatumiwa na wazungu kwenda mashamba ya mikonge na kahawa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, kutoka Tanga kwenda Korogwe na kutoka Moshi kwenda Arusha,” nakuongeza

“Hivi sasa Serikali ya CCM, imeunganisha nchi nzima kwa barabara za lami leo unaweza kutoka hapa kwa usafiri wa bajaji hadi mkoa wa Mtwara,” alisema.

Leo Jumatano, Februari 12, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amerejea nyumbani kwao mokoani Mara akianza kufanya mkutano Lamadi, Mkoa wa Mara kisha akaenda Bunda Mjini alipozaliwa Wasira, pamoja na Tarime Mjini.

Hoja ya CCM haijafanya chochote, imetolewa mkoani Simiyu na Heche na wanachama na viongozi wengine wakisema Wasira mwenye miaka 80 anahitaji kupumzika.

Heche katika maelezo yake amesema licha ya nchi kuwa na utajiri mkubwa wa raslimali kama madini, utalii na ardhi lakini chama kilichopo madarakani kimeshindwa kuzitumia kwa ufanisi ili kuboresha maisha ya wananchi wake.

“Leo nchi hii ina miaka 63 baada ya kupata uhuru hakuna cha maana kilichofanyika, kula ni tatizo, maji ya kunywa ni tatizo katika nchi hii, mwanamke akipata mimba na kwenda kujifungua hata mume wake anaaza kupata mimba ya mawazo,” amesema Heche.