Chadema yaigomea INEC kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi

Dar es Salaam. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, (INEC), vyama vya siasa na Serikali leo Aprili 12, 2025 wakitarajiwa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Chadema kimesema hakina mpango wa kwenda kusaini kanuni hizo.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na vyombo vya habari jijini Dodoma jana Aprili 11, 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisema chama cha siasa ambacho hakitasaini maadili hayo hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi.

Aprili 4, 2025 INEC ilituma mialiko kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa na Serikali kukutana jijini Dodoma leo Aprili 12 kujadiliana na kusaini kanuni hizo za maadili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema haendi na hajatuma mwakilishi kwenda kusaini kanuni hizo.

Mnyika kupitia mtandao wa kijamii wa X na baadaye katika mazungumzo kwa simu na Mwananchi leo Aprili 12, 2025 amesema haendi na hajatuma mwakilishi kwenda Dodoma kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.

Alipoulizwa ni kwa nini hajateua mwakilishi Mnyika amesema: “Ni vyema mkaandika kwamba sijakwenda wala sijateua mtu. Habari kubwa sasa hivi ni katibu mkuu, sitakwenda kusaini wala sijateua mtu.”

Kwa upande wake, Makamu  Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ameandika ujumbe kupitia mtandao wa X akisisitiza chama hicho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa INEC maadili hayo yameandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.

Kifungu hicho kinaelekeza kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.

Kailima katika mahojiano maalumu jana Aprili 11 alisema maandalizi yote muhimu na mawasiliano yameshafanyika baina ya Tume, Serikali na vyama vya siasa na kwamba kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo.

Kailima alisema kazi hiyo itafanyika kwa siku moja tu na baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni za maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *