Hii ni baada ya aliyekuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Said Issa Mohamed, na wenzake, kufungua kesi ya msingi wakilalamikia hatua ya chama hicho kuibagua Zanzibar katika shughuli zake, zikiwemo rasilimali za kifedha.
Kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama, katika kipindi cha siku 14, safu nzima ya uongozi wa Chadema haitaruhusiwa kufanya shughuli zozote za kisiasa.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, na wenzake wawili, wakilalamikia kuwa Chadema inaitenga Zanzibar katika mipango yake ya kisiasa, hasa upande wa usambazaji wa rasilimali fedha.
Chama tawala kuukandamiza upinzani
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, amesema uamuzi huo ni sehemu ya kile alichokiita sarakasi za Chama Tawala, CCM, katika juhudi za kuikandamiza Chadema.
“Amejua lini kuna ubaguzi wa kidini, amejua lini Zanzibar inapunjwa, ama ni baada ya kushindwa uchaguzi ndo ameyaona haya, hizi ni sarakasi za CCM kutumia watu kujaribu kuzuia chama chetu kufanya shughuli zake,” alisema Heche.
Kwa mujibu wa hati ya malalamiko, walalamikaji wanadai kuna mgawanyo usio sawa wa rasilimali za kifedha kati ya Bara na Zanzibar ndani ya chama hicho.
Aidha, wamelalamikia pia kuwepo kwa ubaguzi wa kijinsia, udini, na matamko yanayodaiwa kuwa na nia ya kuvuruga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa baada ya wakili wa Chadema, Jebra Kambole, kujiondoa katika kuendelea kuisimamia kesi hiyo mapema Jumanne, akilalamikia kuwa hoja za mawakili hazikusikilizwa ipasavyo.
Juhudi za kumpata Kambole kwa maoni zaidi hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni.
Shughuli za ndani za kisiasa zasitishwa
Mwanasheria wa kujitegema Tanzania William Kahale ametoa maoni yake kuhusu mwenendo wa kesi hiyo baada ya Kambole kujiondoa.
“Inaonekana Jebra alijitoa kabla muda wa kufanya mamuzi haujafanyika, ikiwa hivyo ina maana hilo ni tatizo na linavunja haki ya mmojawapo katika kesi hiyo,” alisema Kahale.
Shughuli nyingine zilizositishwa na mahakama ni pamoja na shughuli za ndani za kisiasa, operesheni za chama, mikutano ya hadhara na vikao mbalimbali vya Chadema.