
Mbeya. Mkutano wa Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche uliokuwa ufanyike Kata ya Mabadaga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya umeshindwa kufanyika baada ya kudaiwa kuzuiwa na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo Jeshi hilo limefafanua kuwa mkutano na vikao vya chama hicho havikuwatolewa taarifa kama taratibu zinavyoelekeza.
Heche pamoja na viongozi wengine chini ya Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu wapo Kanda ya Nyasa kwa ajili ya mikutano ya hadhara na kuzungumza na wafuasi wao.
Machi 23 chama hicho kilizindua operesheni zake za ‘No Reforms No Election’ ‘Stronger Together’ na ‘Tone Tone’ ambapo baada ya uzinduzi huo, vigogo hao waligawanyika mikoa tofauti.
Mwenyekiti Lissu ameelekea mkoani Rukwa kisha Songwe, huku Heche akianzia Mbeya wilaya za Kyela na Mbarali kisha kutua Njombe kabla ya kuhitimishia ziara zao mkoani Iringa kwa mkutano wa hadhara.
Leo Machi 25, mkutano wa hadhara uliokuwa ufanyike Mabadaga chini Heche, umeshindwa kufanyika baada ya Jeshi la Polisi kuzuia.
Katibu wa chama hicho mkoani Mbeya, Hamad Mbeyale ameliambia Mwananchi Digital kuwa wameshindwa kufanya mkutano huo na kusalimiana na wananchi na wafuasi wao baada ya kuzuiliwa na Polisi.
“Makamu Mwenyekiti alikuwa asalimiane na wananchi na kufanya mkutano, lakini Polisi wamezuia, tukaandaa kikao cha ndani nacho tumezuiwa, ishu siyo kibali cha Polisi kwani tulitoa taarifa.
“Baada ya kuzuiwa kufanya mkutano, tunatarajia kurudi hapa Mbarali Aprili Mosi kusalimiana na wananchi kwa kuwa walikuja kwa wingi kumuona kiongozi wao, kuna Katibu wa Bawacha Mkoa tumesikia alishikiliwa hatujapata taarifa zaidi kama kaachiwa,” amesema Mbeyale.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema hawajazuia mkutano wa chama hicho na kuahidi kulitoa ufafanuzi baada ya kufika ofisini.
Hata hivyo amesema, “eneo la Mabadaga ambalo walitaka kufanya mkutano sio salama ni barabarani ambayo mara kadhaa hutokea ajali, tuombe tu vyama vya siasa katika kipindi hiki kutumia busara zaidi,” amesema Kuzaga.
Endelea kufuatilia mitandao ya mwananchi kujua kinachoendelea…