Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempa saa 72 Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura kuzungumzia mwenendo wa matukio ya utekaji nchini likiwemo la Mdude Nyagali ambaye hadi sasa hajulikani alipo.
Chama hicho kimeeleza kwamba IGP hawezi kuwa kimya wakati wote wakati kuna matukio yanayoonyesha kwamba kuna magenge uhalifu yanatumika kuteka watu majumbani mwao.
Wito huo umetolewa leo Mei 10, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Amani Golugwa wakati akizungumzia kutoonekana kwa kada wao, Dude, ambaye inadaiwa alichukuliwa Mei 2, 2025 na watu waliojitambulisha kuwa ni askari.

Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, Amani Golugwa akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chama Mikocheni, Dar es salaam leo Jumamosi Mei 10, 2025. Picha na Sunday George
“Tunakusihi sana IGP, ndani ya saa 72 uzungumze na Watanzania kuhusu hili suala la magenge ya uhalifu.
Ameeleza kushangazwa kuendelea kusikika taarifa za kuwapo watu wanaojitambulisha ni askari.
Wakati huohuo, Golugwa amesema Chadema kimeweka dau la Sh10 milioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha Mdude kupatikana, hivyo ametoa rai kwa Mtanzania yeyote mwenye kujua alipo kada huyo kutoa taarifa kwa chama.
“Tunatangaza kutoa Sh10 milioni kwa mtu yeyote atakayesaidia taarifa za uhakika za anaposhikiliwa Mdude Nyagali. Kiasi hiki cha fedha siyo kwa kumthaminisha Mdude, maisha ya Mdude yana thamani kubwa,” amesema Golugwa.

Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, Amani Golugwa akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chama Mikocheni, Dar es salaam leo Jumamosi Mei 10, 2025. Picha na Sunday George
Golugwa amelitaka Jeshi la Polisi kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na wananchi kuhusu watu waliojitambulisha kuwa ni askari wanaotuhumiwa kumchukua Mdude nyumbani kwake.
“Tunatoa wito kwa wanachama wote na wananchi na Watanzania ambao hawaridhishwi na mwenendo huu, tusaidiane kuwatafuta watu waliomchukua Mdude,” amesema kiongozi huyo wa Chadema.
Mwananchi limefanya jitihada za kumtafuta IGP Wambura kuzungumzia wito huo wa Chadema, hata hivyo hakupokea simu yake ya mkononi. Pia, Msemaji wa Polisi, David Misime hakupatikana kuzungumzia madai ya Chadema.
Wakati Chadema wakieleza hayo, huko Mbeya, wafuasi wa Chadema wameweka kambi katika ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa huku wakimtafuta Mdude katika maeneo mbalimbali tangu Mei 3, 2025.
Awali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilieleza kutojua mahali alipo Mdude huku likitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu kukamatwa kwake. Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera ametangaza dau la Sh5 milioni kwa mtu atakayetoa taarifa za alipo Mdude.