Shinyanga. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehitimisha operesheni ya No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ katika kanda za Victoria na Serengeti kikiwahimiza wananchi kukikataa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti bara, John heche walifanya mikutano mbalimbali kwenye mikoa hiyo ya kanda ya ziwa ambayo ilikuwa na mwitikio mkubwa.

Operesheni hiyo ilianza Mei 8, 2025 kanda ya Victoria yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita na kumalizika jana Jumamosi Mei 17,2025 kwenye kanda ya Serengeti iliyojumlisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walijigawa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza lililowajumuisha katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Deogratius Mahinyila, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (Bazecha), Suzan Lyimo na kiongozi wao alikuwa Heche.
Kundi la pili lilikuwa likiongozwa na Katibu Mkuu, John Mnyika pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema. Aidha, viongozi mbalimbali wa kanda hizo nao walikuwa wakijigawa kwenye makundi hayo na mikutano ilikuwa ikifanyika kuanzia asubuhi.
Pamoja na kunadi sera zake viongozi hao walitumia mikutano yao ya hadhara kutoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa chama hicho kutoingia kwenye uchaguzi, bila mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaoweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.

Katika maeneo mbalimbali aliyopita Heche, aliwasihi wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa kuikataa CCM akidai imewapuuza ndio maana wanaishi katika lindi la umaskini licha ya wingi na utajiri wa maliasili ikiwemo madini yanayopatika kanda hiyo.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu za pato la kila mtu kwa kila mkoa kwa mwaka 2023, mikoa ya Simiyu na Kagera ambayo ipo kanda ya ziwa zinashika nafasi ya kwanza na ya pili kwa kuwa na watu wenye umaskini wa kipato nchini.
Hii ni kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwenye chapisho lao la Tanzania in Figures 2023 unaonyesha kuwa kipato cha Mtanzania kwa mwaka (Per Capital Income) ni Sh3.055 milioni ingawa kuna takriban mikoa 15 ambayo watu wake wana wastani wa kipato cha chini kuliko wastani wa kitaifa wa Sh3 milioni.
Wastani wa kipato cha mtu inapatikana kwa kuchukua jumla ya pato la mkoa na kuigawanya kwa idadi ya wakazi wa mkoa husika.

Kukamilika kwa ziara hiyo ya Chadema kumefungia milango kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla kupita pale walipopita Chadema ili kuweka mambo sawa.
Mei 15, 2025, Makalla akizungumza katika mkutano wa hadhara Uwanja wa Kilosa Town mkoani Morogoro alisema wenzao Chadema wamekwenda Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga na wao wanajipanga kwenda huko.
“Popote walipopita tutapita kwa sababu tunayo mambo ya kujivunia, ukweli na uongo ni sawa na mafuta na maji, lazima vijitenge.
Niseme tu WanaCCM tuendelee kukipigania chama kuna mambo makubwa yamefanyika na tuendelee kuyalinda mafanikio yaliyopatikana kwa wivu,” alisema Makalla. Tayari msafara wa Makalla umekwishaingia mkoani Kagera kuanza ziara hiyo.

Alichokisema Heche
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Kahama jana Jumamosi, Mei 17, 2025, Heche amesema mikoa yote sita inayounda kanda ya ziwa imejaaliwa utajiri wa madini ya dhahabu achilia mbali madini ya vito ya almasi na nickel, lakini jamii haijanufaika vya kutosha kwa uwepo wa rasilimali hiyo katika maeneo yao.
“Mgodi wa dhahabu mkubwa kuliko yote nchini ni Bulyanhulu na unapatikana Wilaya ya Kahama, Geita Gold Mining na Barick Gold yote iko kanda ya ziwa; sisemi hili kwa ubaguzi, lakini maisha ya wananchi kanda ya ziwa yanastahili kuwa bora zaidi,” amesema.
Amesema badala ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata mitaji ya kuchimba madini hayo, Serikali imegawa maeneo mengi ya migodi yenye kiwango kikubwa cha dhahabu kwa wawekezaji kutoka nje, ambao wanahamishia nchini mwao faida inayopatikana kwa kazi ya uchimbaji inayofanywa na Watanzania wanaoambuliwa ajira na ujira usiolingana na kazi wanayofanya.
“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini matumizi yasiyo ya tija ya zaidi ya Sh500 milioni, fedha hizi zingetosha kuwakopesha mitaji ya kuchimba madini vijana ambao mapato na fedha zao zote zingebaki nchini kuendeleza na kusisimua uchumi wetu, tofauti na sasa ambapo fedha ya sekta ya madini inafaidisha raia wa nchi nyingine huku sisi tukiachiwa mashimo,” amesema Heche.
“Kwa ziara yangu ya siku 10, nimefika kwenye mikoa, wilaya na halmashauri zenye utajiri wa madini ya dhahabu, almasi na nickel; umaskini wa wananchi ni wa kutisha kiasi kwamba wapo watu hawamudu kupata milo miwili kwa siku. Hii haikubaliki kuona Watanzania wanaoishi jirani na migodi wanakosa hata huduma ya uhakika wa majisafi na salama,” amedai Heche.

Amedai hali ya barabara katika wilaya na halmashauri zenye migodi ni mbaya akitolea mfano wa msafara wake kutumia zaidi ya saa tatu kusafiri umbali wa kilomita 100 kutoka Kijiji cha Solwa Wilaya ya Shinyanga hadi Kijiji cha Kakola wilayani Kahama.
Katika mkutano wake wa kuhitimisha ziara mjini Kahama, Heche ambaye pia anakaimu nafasi ya uenyekiti wa Chadema kutokana na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kuwa mahabusu kwa kesi ya uhaini isiyo na dhamana, ametaja Ziwa Victoria kuwa rasilimali nyingine inayopatikana kanda ya ziwa ambayo haijawanufaisha wananchi.
“Watu wanaolima mpunga kwenye mashamba yaliyo umbali usiozidi kilomita moja kutoka Ziwa Victoria wanavina mara moja kwa mwaka kwa sababu wanategemea msimu wa mvua za masika.
Serikali makini inayojali watu wake ingewekeza katika skimu za umwagiliaji kuwezesha wakulima wa mpunga unaovunwa kila baada ya miezi mitatu, hivyo kuwezesha kulima na kuvuna zao hilo mara nne kwa mwaka,” amesema.
Amesema wananchi wa nchi ya Misri wanalima kilimo cha umwagiliaji kwa kutegemea maji ya mto Nile unaotoa maji yake Ziwa Victoria huku Watanzania ambao ziwa hilo liko nchini mwao, wanalima kwa kutegemea misimu ya mvua.
“Watanzania wanaoishi hatua chache kutoka Ziwa Victoria hawana uhakika wa huduma ya majisafi na salama, wakati wananchi wa nchi ya Misri ambayo ni jangwa wanapata huduma ya uhakika wa majisafi na salama yanayotoka Ziwa Victoria kupitia mto Nile. Serikali ya CCM imewapuuza vya kutosha wakazi wa Kanda ya Ziwa,” amedai Heche.
Mwenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo amewaomba wazee wenye mapenzi mema na ustawi wa jamii ijayo ya Tanzania kuunga mkono mapambano ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaohakikisha viongozi wanapatikana kwa ridhaa ya wananchi, ambao pia watakuwa na mamlaka ya kuwawajibisha wasipotekeleza wajibu.
Ombi kama hilo pia limetolewa na Mwenyekiti wa Bavicha, Deogratius Mahinyila ambapo aliwataka vijana kote nchini kupigania mabadiliko bila kujali jinsia, itikadi wala maeneo yao ya kijiografia.
“Vijana ndio chachu ya mabadiliko duniani kote kwa sababu ya kupigania maisha bora zaidi kwa ajili yao na watoto wao; vijana wa Tanzania tuamke tudai mabadiliko ambayo yatatuhakikishia maisha bora zaidi,” amesema Mahinyila.