Chadema: Serikali mbadala ndio itakayotatua hali ngumu ya maisha

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai hali ya ngumu ya maisha na changamoto za ajira zitaondoka endapo Watanzania watafanya uamuzi wa kupata Serikali mbadala kupitia uchaguzi huru na wa haki.

Kimesema ajenda ya No refomrs No election ndio njia pekee itakayowawezesha wananchi kupata viongozi bora watakaotatua na kuzisemea changamoto zao.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 23, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Chamazi wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mkutano huo ni mwendelezo wa Chadema kunadi ajenda yao ya No reforms no election kwa wananchi ili kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.

Heche ambaye ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini mkoani Mara, amesema changamto za maisha na ukosefu wa ajira haziwezi kupungua  kwa kumsubiri Mungu ashuke, bali ziitabalishwa kwa kuweka Serikali nyingine madarakani.

“Chadema tumekuja kwenu na No reforms no election ili kura yako iwe na thamani kwa mbunge au diwani awajibike kwenu wananchi, hiki ndicho chama kinachopigania.

“Mkikiweka Chadema madarakani kikishindwa kutekeleza yale kilichoahidi inakuwa rahisi kukipiga chini na kumweka mtu mwingine ili heshima iwepo. Hilo ndilo tunalolipigania lazima rasilimali zirudi kwa wananchi,” amesema Heche.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Suzan Lyimo amesema wanancgi Dar es Salaam kujitokeza katika mikutano ya hadhara ya chama hicho, akisema mwamko wa jiji umekuwa mdogo tofauti na mikoani.

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema John Pambalu amesema lazima kupigania mabadililo ya mfumo wa uchaguzi ili kupata viongozi bora wanaotokana na ridhaa ya wananchi.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Rose Mayemba amesema lengo la mikutano hiyo ni kuhakikisha ajenda ya No reforms No election inaelekeweka kwa umma.

Naibu Spika la Bunge la Wananchi la Chadema, Lumola Kahumbi amedai kwa hali ilivyo uchaguzi kuwa huru na haki haiwezekani, akitolea mfano kilichojiri katika mchakato wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka 2024.

“Kama mabadiliko hayatafanyika basi ni ngumu wapinzani kushinda, tukisema No reforms no election tunamaanisha,” amesema Kahumbi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *