Chadema, Msajili bado kaa la moto

Dar/mikoani. Ni mvutano. Hoja ya uhalali wa wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeibua hali ya kutunishiana misuli kati ya chama hicho na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, huku kila upande ukitoa hoja za kisheria kuhalalisha hatua ulizochukua.

Chadema kupitia uongozi wake inakosoa uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kuitaka iwasilishe maelezo kuhusu malalamiko ya mchakato wa uthibitishaji wa wajumbe hao, ikirejea kifungu cha 5B cha Sheria ya Vyama vya Siasa, huku Msajili naye akikosoa hilo kwa kurejea sheria na kanuni mbalimbali.

Mzizi wa yote hayo ni barua ya malalamiko iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome akikichongea chama hicho kwa kukiuka katiba yake katika mchakato wa uthibitishwaji wa wajumbe hao.

Hadi Mchome anafikisha barua hiyo kwa Msajili alikiandikia chama chake na kabla ya kujibiwa aliwasilisha malalamiko hayo katika Ofisi ya Msajili.

Mchome alikuwa akilalamikia kwamba akidi ya Baraza Kuu haikutimia wakati wa kuwathibitisha viongozi hao ambao walikuwa wameteuliwa na mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu, katika Kikao chake cha januari 22, 2025 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, chama hicho kilitetea uamuzi wake, kikisema akidi iliyokuwa inahitajika ni asilimia 50 ambayo ilitimia na si asilimia 75 inayohitajika ikiwa suala linaloamuliwa ni uchaguzi au mabadiliko ya sera.

Viongozi waliokuwa wanaolalamikiwa na msajili ameamua kuwaweka kando hadi Baraza kuu jingine liitishwe ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Wengine ni wajumbe wa kamati huu Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh pamoja na Dk Rugemeleza Nshala, ambaye pia aliteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa chama hicho.

Kufuatia malalamiko hayo, Mei 12, 2025, Msajili wa Vyama vya Siasa, alichokiandikia barua chama hicho na nakala kwenda kwa Mchome, akikitaka kiitishe upya kikao cha Baraza Kuu ili kujaza nafasi za wajumbe hao.

Katika maelezo yake, msajili anaeleza amefanyia kazi malalamiko ya Mchome kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungo 4 (5) (a) na (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 na Kanuni ya 31(2)(3) ya Kanuni za Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa za Mwaka 2019.

Msajili anaeleza kutokana na sheria na kanuni hizom malalamiko ya Mchome yana ukweli kwamba Kikao cha Baraza Kuu  cha Januari 22, 2025 kilikuwa batili kwa sababu kilikuwa hakina akidi inayotakiwa kwa mujibu wa katiba ya Chadema ya mwaka 2006 toleo la 2019.

Katika maelezo yake, msajili anasema kwa mujibu wa kifungu cha 31(3) cha Kanuni za Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa za Mwaka 2019, Msajili wa vyama ameielekeza Chadema kuitisha kikao kingine cha Baraza Kuu kujaza nafasi za viongozi zilizokuwa wazi kwa mujibu wa Sheria vya Vyama vya Siasa, katiba na kanuni za Chadema.

Majibu ya Chadema

Jana Jumatano, Mei 14, 2025, Chadema imetoa majibu kwenda kwa Msajili, ambayo waliyatuma Machi 27, 2025 kujibu kile ambacho msajili aliwataka kufanya.

Katika majibu hayo ya kurasa mbili, yakiwa yamesainiwa na Naibu Katibu Mkuu-Bara, Aman Golugwa kwa niaba ya Katibu Mkuu wake, John Mnyika, chama hicho kinamweleza Msajili kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 4(5)(b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, ofisi yake ina wajibu wa kusimamia chaguzi za ndani ya vyama vya siasa.

Chadema kilimweleza msajili kwamba wanachokijua kwa mujibu wa barua ya Mchome, amekata rufaa kwa Msajili na si kuwa alimtaka afanye uchuguzi bali ameleta rufaa kwako.

“Tunapenda kusema kwa uelewa wetu wa sheria ya vyama vya siasa na kifungo hicho cha 5B, ambacho unadai kinakupa madaraka ya kupewa unachokitaka, ni kuwa ofisi ya msajili wa vyama vyama vya siasa haina mamlaka ya rufaa kwa mwanachama ambaye hajaridhika na uamuzi wa chama,” inaeleza Chadema.

“Aidha, sheria ya vyama vya siasa haiipi ofisi yako madaraka ya kusimamia uchaguzi bali kuangalia uchaguzi. Hivyo kwa kuwa ofisi yako si mamlaka ya rufaa, Chadema inasema takwa lako kwetu ni kinyume cha katiba ya Chadema na kinyume kabisa na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Katika msisitizo wake Chadema ikaongeza: “Chadema itakuwa tayari kabisa kukupa taarifa unazozitaka kama utatueleza kwa kina na wazi kabisa kuwa kwa taarifa hizo zitakuwezesha kutekeleza kifungu kipi cha sheria ya vyama vya siasa, kinachoipa ofisi yako madaraka ya kupokea na kuamua rufaa za wanachama wa vyama vya siasa kwa upande mmoja au taarifa hizo zinaiwezesha ofisi yako kutekeleza jukumu lipi la kisheria juu ya taarifa za vikao vya kawaida vya chama cha siasa.”

Vilevile, leo Jumatano, Mei 14, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-bara, John Heche ametumia mikutano ya operesheni No reforms, no election mkoani Mara kutoa msisitizo wa suala hulo.

Heche amesema Msajili hapaswi kuwapangia cha kufanya: “Kama anataka kuifuta Chadema na aifute lakini asitulazimishe. Sisi tunaendelea kumtambua Mnyika kama katibu mkuu na viongozi wengine. Hiki chama ni kikubwa sana na kitasonga mbele licha ya hila tunazofanyiwa.

Wanatokaje?

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Mei 14, 2025, Wakili Frank Chundu amesema kifungu cha 4(5) cha Sheria ya Vya Siasa, kimeweka majukumu ya ofisi ya Msajili, ikiwamo wajibu wa kutazama mchakato wa chaguzi za vyama vya siasa.

“Haijampa Msajili kusimama kama mrufani, ndio maana katiba za vyama vya siasa zinatoa nafasi kwa makada wake, kama hawajiridhika na utaratibu uliotumika, kufuata utaratibu fulani ambao hadi mwisho unawapeleka mahakamani,” amesema.

Chundu amesema si jukumu la Msajili kuwa sehemu ya rufaa katika vyama vya siasa, anawajibika kuangalia uchaguzi kama taratibu za chama zimefuatwa.

“Ndio maana akiona taratibu zimekiukwa wajibu wake ni kuvielekeza vyama kufuata katiba na kanuni,” amesema Chundu.

Kwa mujibu wa Chundu, miongozo iliyowekwa inazihusu pande zote mbili za vyama vya siasa na ofisi ya msajili, hivyo inapaswa kufuatwa.

“Tuwe katika nafasi ya kusimamia miongozo iliyowekwa, kama Msajili hana mamlaka ya kusimamia rufaa kwa nini asimamie? Akisimamia rufaa anakwenda nje ya mamlaka yake kisheria.

“Turudi chini, tukae pamoja (Msajili na vyama vya siasa) tuelekezane kisheria kuhusu utaratibu ulivyo na kila mtu asimamie wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Tukitoka nje ya utaratibu wa kisheria ndio maana tunaingia kwenye migogoro kama hii,” amesema Chundu.

…wengine wahama

Wakati vumbi likiwa halijatulia, bado hamahama ya wanachama ndani ya chama hicho imeendelea kushika kasi, baada ya makada wengine kujiondoa, wakidai wanasaka jukwaa lingine la kufanya siasa zao.

Wanachama waliojiengua jana Jumatano, ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa kichama Kinondoni, Henry Kilewo na Mhazini wa chama hicho Kanda ya Pwani, Patrick Assenga ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Segerea.

Wengine ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Moza Ally na miongoni mwa waasisi wa Chadema Digital, Glory Tausi na Asha Abubakari ambaye alikuwa Katibu wa Chadema wilaya ya kichama Segerea.

Katika maelezo yao, Kilewo na wenzake wamesema wanakwenda kugombea ubunge kwenye maeneo yao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Mkoani Shinyanga kuna viongozi na makada kadhaa ambao nao wametangaza kujiondoa akiwamo katibu wa baraza la wanawake (Bawacha) mkoa wa Shinyanga Furahisha Wambura walitangaza kujiondoa.

Uamuzi wa kujiondoa ndani ya chama hicho ni mwendelezo wa kufanya hivyo kuanzia Mei 7, 2025 kwa waliokuwa wajumbe wa sekretarieti iliyokuwa chini ya utawala wa uenyekiti wa chama, Freeman Mbowe,  huku tetesi zikieleza huenda Mei, 18, 2025 watatangaza kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Nyongeza na Tuzo Mapunda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *