Mbeya. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimevunja rasmi kambi iliyokuwa imewekwa kushinikiza kupatikana kwa kada wao, Mdude Nyagali, huku kikieleza msimamo wao katika ushiriki wa uchaguzi mkuu na uzinduzi wa kampeni ya ‘No reforms, no election’ mkoani Mbeya.
Pia kimewataka wananchi na wafuasi wao kupuuza taarifa za baadhi ya waliojivua uanachama wa chama hicho, wanaoeleza kuwa uongozi wa sasa hauna ushirikiano.
Mdude anadaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake mtaa wa Iwambi jijini Mbeya tangu Mei 2, 2025 hajapatikana huku Chadema ikitumia njia tofauti kumtafuta mwanaharakati huyo bila mafanikio.

Hali ilivyo kwa sasa katika Ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa jijini Mbeya ilipokuwa kambi ya wafuasi wa Chama hicho kushinikiza kupatikana kwa kada na mwanaharakati, Mdude Nyagali.
Chadema ikiongozwa na viongozi mbalimbali, wafuasi na baadhi ya wananchi walikuwa na kambi ya zaidi ya siku 14 katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa, wakishinikiza kupatikana kwa Mdude.
Akizungumza leo Mei 21, 2025 Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli amesema baada ya kupata vitisho ikiwamo kumwagiwa vitu vinavyodhaniwa kuwa ni sumu, wameona harakati za kumpigania Mdude zihamie nyumbani ili kuokoa maisha ya wengine.
Amesema zipo njia nyingi za kuendelea kupambania kila mwananchi na mfuasi wa chama hicho na Mbeya itaendelea kuwa mfano kupitia tukio la Mdude. Masaga pia aliiomba Serikali na vyombo vya dola kusaidia kupatikana kwa mwanaharakati huyo.
“Tumeona kuendelea kuwa hapa ilihali tunapitia vitisho vyenye nia ovu bora tutumie njia nyingine kudai haki ya Mtanzania huyu, hadi sasa tunaomba Serikali na mamlaka nyingine zisaidie kupatikana kwa Mdude, sisi tutatoa aina yoyote ya ushirikiano kwa yeyote” amesema Masaga.
Masaga ameongeza kuwa baada ya kuligawa Jimbo la Mbeya Mjini kupatikana Jimbo jipya la Uyole, wanaenda kukaa kamati ya chama mkoani humo kuchagua viongozi kwa ajili ya kusimamia Jimbo jipya ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2025.
“Wakati tukiendelea kudai mabadiliko na maridhiano, Chadema Mkoa wa Mbeya tutakaa kuanza mchakato wa kufanya uchaguzi kwa ajili ya Jimbo jipya la Uyole, ambapo kama kutakuwa na mabadiliko ambayo chama inayataka kupitia ajenda ya No reforms, no election sisi hata kesho tupo tayari kwa uchaguzi.”

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli akizungumza kuhusu kuvunjwa kwa kambi ya Chama hicho kushinikiza kupatikana kwa kada wao Mdude Nyagali na muelekeo mpya wa Chama hicho.
Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa wao wapo tayari kusubiri hadi 2030 kushiriki uchaguzi baada ya kujiridhisha usawa, haki, uhuru na uwazi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kuthamini kura ya wananchi.
“Mapema Juni tunatarajia kuzindua kampeni ya ‘No reforms, no election’ mkoani Mbeya ikiwa ni kuwapa elimu wananchi kuhusu kutoshiriki uchaguzi iwapo hakutakuwapo mabadiliko ya mfumo yanayotakiwa.
Amesema wanaohama chama hicho kwa sasa wakitoa kauli zisizo na ukweli, wananchi wanapaswa kupuuza akieleza kuwa Chadema itabaki kuwa imara wakati wote.
“Mimi mwenyewe nilikuwa timu Mbowe (Freeman) lakini baada ya uchaguzi mkuu tulipongezana, hata wote walioondoka hakuna aliyekuwa mkereketwa wa Mbowe kama mimi, lakini bado naamini Chadema iko imara na hao pengine walihitaji nafasi.”
“Nashukuru hadi sasa Mbeya iko salama na waliotarajia ning’atuke wamekwama, mimi sifuati mtu bali nabaki na chama kama wosia wa aliyekuwa Mwenyekiti wetu Taifa Freeman Mbowe” amesema Masaga.