
Mbeya. Wakati Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitarajia kuzindua kampeni yake ya ‘No Reforms No Election’ kwa kufanya mikutano ya nchi nzima, jijini Mbeya, viongozi wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu na John Heche wamegawanywa mikoa tofauti ya Kanda ya Nyasa kuhakikisha wanawafikia wananchi na wafuasi wake.
Lengo la kampeni hiyo ni kupeleka elimu kwa wananchi ya kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, vinginevyo uchaguzi usifanyike.
Uamuzi huo ulipitishwa Desemba 2024 na Kamati Kuu ya chama hicho, kabla ya msimamo huo kuthibitishwa na Mkutano Mkuu Januari 21, 2025.
Kanda ya Nyasa ina mikoa mitano, ambapo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu amekabidhiwa Rukwa na Songwe.
Makamu wake-Bara, John Heche akielekea Mbeya na Njombe huku vigogo hao wakikutana mkoani Iringa kufunga kampeni hiyo, Machi 29, 2025.
Jana Jumatano, Naibu Katibu Mkuu wa cha chama hicho Bara, Aman alisema kampeni hiyo Inakwenda nzima kwa siku 48 kuanzia Machi 23 hadi Mei 10, 2025 ikianzia kanda ya nyanza.
Amesema kwenye ziara hiyo wataelimisha Watanzania kuhusu mabadiliko yanayohitajika kuanzia kwenye Katiba hadi kwenye muundo na utendaji kazi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 20, 2025 Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu amesema katika ziara hiyo ya kitaifa chini ya Mwenyekiti, Lissu, wataanza na uzinduzi wa operesheni za ‘No Reforms No Election’, ‘Stronger Together’ ya kukiweka chama imara na Tone Tone ya kukichangia chama fedha kwa ajili ya uendeshaji.
Amesema baada ya uzinduzi huo Machi 23 mwaka huu katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, Lissu ataelekea mkoani Rukwa atakapofanya mikutano ya ndani na hadhara hadi Machi 27 kisha kutua mkoani Songwe kwa siku mbili.
“Heche ataanzia Mbeya Wilaya za Kyela, Busokelo na Rungwe, kisha kusalimiana na wananchi Mbarali kuelekea Njombe Machi 26, kisha kuingia Iringa kwa siku mbili, ambapo Machi 29 viongozi hao watakutana kwenye hitimisho mjini Iringa kufunga ziara hiyo kwa mkutano wa hadhara” amesema Sugu.
Kuhusu maandalizi ya mapokezi, Sugu amesema hadi sasa hawajapata changamoto yoyote kutoka vyombo vya dola akieleza kuwa matarajio yao ni kufanikisha matukio yote kama walivyojiandaa.
Amesema kwa sasa hofu ya wafuasi wao kuhusu msimamo wa ushiriki wao katika uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, baada ya ziara ya viongozi wa chama Taifa watapata kujua msimamo na uelekeo wa Chadema.
“Ndio maana tunahamasisha wananchi kujiandikisha kwa kuwa haya tunayopigania iwapo yatatekelezwa uchaguzi utafanyika, kwa hiyo kujua msimamo tusubiri hii operesheni tuone matokeo yake na mwelekeo utapatikana.”
“Hadi sasa maandalizi ni mazuri na tunaendelea kujipanga, bado hatujapata hujuma yoyote na bahati nzuri sisi Chadema hatuna tatizo badala yake sisi ndio huwa tunafanyiwa vurugu,” amesema Sugu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha), Elizabeth Mwakimomo amesema wanachoshinikiza Serikali ni kuondoa mifumo kandamizi katika uchaguzi akieleza baadhi ya wananchi wanakatishwa tamaa na matokeo yanavyotoka.
Amesema kuelekea katika operesheni hiyo, maandalizi upande wa wanawake ni makubwa katika kuunga juhudi za chama hicho kuhakikisha haki inapatikana tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
“Ile tuliyoshuhudia ya uchaguzi uliopita ilikuwa ni kukatisha tamaa, tunahitaji mwaka huu kuona zile mifumo kandamizi zinaondoka, tulikata tamaa na uchaguzi wa awamu ya tano kuwapitisha watu ambao hawakushinda,” amesema Elizabeth.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama hicho mkoani Mbeya, Elisha Chonya amesema tangu kutangazwa kwa operesheni hiyo, Desemba mwaka jana, vijana waliipokea vyema na kwamba hadi sasa wamejipanga kudai haki kabla na wakati wa uchaguzi.