Dar es Salaam. Ukiacha ajenda tatu zilizowekwa wazi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inapokwenda kwenye kikao cha Kamati Kuu kesho Ijumaa, Mei 23, 2025, yapo mambo mengine magumu yatakayohitaji mijadala na uamuzi mgumu.
Kikao hicho kinafanyika katikati ya misukosuko ambayo chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kinapitia, kubwa ikiwa ni utitiri wa viongozi na wanachama wake kujiuzulu na kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Miongoni mwa mambo hayo ni kuhusu hatima ya baadhi ya mali za chama katika ofisi hasa za mikoa na kanda, ambazo viongozi wake wamejiondoa Chadema. Pia, akaunti za mitandao ya kijamii za chama hicho zinazodaiwa kuendelea kushikiliwa na viongozi hao waliokihama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa na kuendelea hadi Mei 24, 2025, huku hali ya kisiasa nchini, oparesheni ya No Reforms No Election, uvunjaji wa haki za binadamu, na ukandamizaji wa demokrasia zikiwa ajenda zilizowekwa wazi.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, imeeleza kuwa kikao hicho kitafuatiwa na hotuba ya Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, atakayoitoa kwa Taifa.
Kikao hicho kimeitishwa kipindi ambacho chama hicho kimepoteza mamia ya wanachama, wakiwemo viongozi wa kanda, mikoa, wilaya, majimbo hadi matawi, na waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya uongozi uliopita ambao sasa ni viongozi wa Chaumma.
Kadhalika, Kamati Kuu inakutana katikati ya nyakati zilizoacha ombwe la uongozi katika baadhi ya mikoa na kanda, baada ya wengi wao kujiondoa Chadema na kuhamia Chaumma kinachoongozwa na Mwenyekiti, Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa.
Ni zaidi ya ajenda
Kikao hicho kitakachoongozwa na Heche, akiwa mbadala wa Tundu Lissu aliyeko mahabusu kwa kesi za tuhuma za uhaini kwa zaidi ya mwezi sasa, kitakuwa cha kwanza kufanyika bila ushiriki wa mwenyekiti wake.
Itakumbukwa hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa barua ya kutowatambua viongozi wa sekretarieti ya chama hicho kwa madai walipatikana kinyume na misingi ya Katiba na kanuni za Chadema, ni hoja nyingine inayotajwa kujadiliwa.
Masuala mengine ni kesi ya Lissu na ile ya madai inayohusiana na mgawanyo wa rasilimali za chama, pamoja na kushikiliwa kwa muda Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa, akiwa safarini kwenda Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU).
Kujivua uanachama
Pia suala la kujivua uanachama huenda likatawala katika kikao hicho. Tangu kuanzishwa kwa chama hicho, haijawahi kutokea makada na viongozi waandamizi kuhama kwa maelezo yanayofanana.

Kundi la kwanza kutangaza kujivua uanachama lilikuwa la waliokuwa wajumbe wa sekretarieti likiwahusisha John Mrema, Salum Mwalimu, Benson Kigaila, Catherine Ruge na Julius Mwita waliodai kuchoshwa na uongozi wa Lissu ulivyoshindwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.
Baada ya kina Mrema na wenzake kuondoka, ndipo mfululizo wa mikutano kati ya wanahabari, makada na viongozi wa Chadema wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, Baraza Kuu, Mkutano Mkuu, wenyeviti na makamu wenyeviti wa kanda, mikoa na wilaya, pamoja na viongozi wa mabaraza ulianza.
Kwa ujumla wao, wote walioondoka wamepokelewa Chaumma na baadhi yao Halmashauri Kuu ya chama hicho kimewateua kuwa viongozi wa juu. Mwalimu amekuwa Katibu Mkuu, Devotha- Kaimu Makamu Mwenyekiti Bara na Kigaila amekuwa Naibu Katibu Mkuu – Bara.
Wimbi hilo la mamia kutimkia Chaumma na maelezo kwamba wanakwenda kukijenga, limetoa hofu kuhusu mali za Chadema kuanzia ngazi za chini. Hilo limeifanya Mwananchi kumtafuta Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama, ambaye amesema kwa kawaida kiongozi yeyote anapojiuzulu au kuondoka kwenye nafasi yake, anakabidhi mali au vifaa vyote kwa mrithi wake.
Utaratibu huo, amesema, ndio utakaofanyika kwa kiongozi yeyote aliyeacha nafasi yake kama alikuwa na mali ya chama, hivyo hakutakuwa na tatizo.
“Hakuna mali itakayopotea kwa mtu kuachia nafasi yake au kuhama chama. Kama alikuwa na mali, baada ya kuondoka atafuata utaratibu wa kuikabidhi kwa mrithi wake au muhusika,” amesema.
Hata hivyo, Dk Lwaitama hakuwa tayari kuelezea madai ya kutoweka kwa baadhi ya mali, yakiwemo magari yaliyokuwa yakitumika makao makuu ya chama hicho, kwa kile alichofafanua kuwa kwa nafasi yake yeye ni msimamizi wa sera, si shughuli za kila siku.
“Kwa nafasi yangu nasimamia masuala ya kisera, si majukumu ya utendaji wa kila siku wa chama. Kwa hiyo kuhusu sijui kitu gani hakipo na kipi kipo, kwanza ni madogo sana hayo, pili siwezi kuyajua,” ameongeza.
Katika hilo, Devotha alipoulizwa juu ya ofisi amesema,“Katika ngazi za chini ni wanachama wenyewe wanazigharamia na makao makuu zinagharamikiwa tu na makao makuu. Kwa hiyo kama viongozi na wanachama wataondoka, kuna uwezekano mkubwa wa kufunga ofisi isipokuwa kanda, lakini sisi tutaanzisha ofisi nyingine.”
Aidha, katika maelezo yake, Dk Lwaitama amegusia kuhusu suala la waliokuwa viongozi wa chama hicho kuondoka, akisema hakuna tatizo kwa kuwa ilishawahi kutokea ndani ya chama hicho bila madhara yoyote.
“Mtu akiondoka kuna tatizo gani? Si anaondoka tu. Tumeona Katibu Mkuu (Dk Vincent Mashinji), Naibu Katibu Mkuu (Zitto Kabwe) waliondoka. Hata akiondoka Mwenyekiti, si ameondoka kuna tatizo gani?” amehoji.
Amesema kuondoka kwa mwanachama yeyote sio shida kwa kuwa atapatikana mwingine kuziba nafasi aliyoiacha na kwamba suala la kuhama chama ni haki ya kikatiba ya kila mtu.
“Chama ni wanachama. Kama aliyeondoka alichaguliwa, si tutachagua wengine. Hiki chama kilikuwepo miaka yote. Watu wanaohamia kwenye chama hicho ni hiari yao kikatiba,” amesisitiza.
Barua ya Msajili
Kuhusu barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyokitaka Chadema kuitisha upya Baraza Kuu kuthibitisha upya wajumbe wanane wa Kamati Kuu na sekretarieti, chama hicho kimesema suala hilo haliko ndani ya mamlaka ya msajili, lazima lijadiliwe na kupatiwa suluhisho la ndani, kwani linaweza kwenda kukiathiri.
Agizo la Msajili lililenga kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome, akipinga akidi ya Baraza Kuu iliyowathibitisha viongozi hao walioteuliwa na Lissu.
Mchome, ambaye wiki iliyopita alivuliwa uongozi na chama chake Kanda ya Kaskazini, alikuwa akilalamikia akidi haikutimia ya kuwathibitisha viongozi hao, akisema ilihitaji asilimia 75 ya wajumbe halali. Hata hivyo, chama hicho kilisema akidi hiyo hutumika tu katika uchaguzi na kupitisha masuala ya kisera, na kuwa suala hilo lilihitaji asilimia 50 ya wajumbe, ambao walitimia.
Viongozi waliolalamikiwa ni Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara), na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu: Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh, na Dk Rugemeleza Nshala – Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Hata hivyo, kupitia mikutano yake, Heche amesisitiza hakuna watakachokibadilisha kwa kuwa bado wanawatambua Mnyika na wenzake kama viongozi halali.
Akaunti za mitandao ya kijamii
Kuhusu akaunti za mitandao ya kijamii za chama hicho ambazo zimefanya chama kuanzisha mpya, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amekiri hilo kutokea.
“Ni kweli wapo viongozi walioondoka na akaunti za mitandao ya kijamii za chama,” amejibu kwa ufupi, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo.
Kuhusu magari, Brenda hakujibu lolote, na hata hivyo hakueleza sababu ya kutojibu.
Hata hivyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano wa Chadema, idara iliyokuwa inasimamia mitandao hiyo, John Mrema amesema kinachoelezwa na chama hicho kwa sasa ni uongo.
Ameeleza mitandao hiyo haipo chini ya miliki ya chama hicho kwa sababu aliyepewa kuiendesha anakidai fedha chama hicho.
“Uongo, nilishajibu kwenye akaunti yangu ya X kwa kirefu sana. Wanadaiwa (Chadema) na aliyekuwa anaendesha,” amesema Mrema.
Akizungumzia hatari ya kutoweka kwa mitandao ya kijamii uliyomiliki kwa miaka kadhaa, mtaalamu wa mitandao, Dennis Mnyambe amesema inarudisha nyuma wafuasi na kufuatiliwa.
“Unapokuwa na akaunti uliyoitumia kwa muda mrefu, kama ulikuwa active, maana yake utakuwa na wafuatiliaji wengi. Ukiacha, utalazimika kuanza upya na pengine usipate uungwaji mkono kama wa akaunti ya awali,” amesema Dennis.
Kesi za Lissu
Suala la kesi za Lissu litajadiliwa kwa kina katika kikao hicho, ili kuweka mikakati ya kisheria na mingine kuhakikisha mwenyekiti huyo anarejea uraiani. Kesi hizo zimeahirishwa hadi Juni 2, 2025, ambapo kesi ya uhaini itatajwa, huku ile ya kuchapisha taarifa za uongo ikianza kusikilizwa.
Pia kuna wanachama waliojeruhiwa na polisi baada ya kukamatwa mahakamani, nao watakuwa sehemu ya mjadala kuhusu namna ya kuwasaidia.
Vilevile, kama alivyodokeza Heche, watajadili hali ya mwenendo wa operesheni ya No Reforms No Election, ambayo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa Kanda ya Nyasa na kuendelea kanda nyingine. Kuanzia Mei 28, 2025, itaendelea Kanda ya Kaskazini.