
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amesema Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wanapaswa kujitathimini kama wanaweza kutekeleza majukumu yao baada ya kusema Chadema hakitashiriki uchaguzi kwa kuwa hakijasaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Amesema sababu za chama au mgombea kutoshiriki uchaguzi mkuu zimetajwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo, na kilichofanywa na Tume hiyo ni propaganda ya kutaka kukidhoofisha Chadema.
Mwanasheria huyo ametoa kauli hiyo kujibu kauli iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima kwamba Chadema kimejiondoa kwenye mchakato huo, baada ya kushindwa kusaini kanuni hizo kama ilivyofanyika kwa vyama vingine 18 vya siasa.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jumanne, Aprili 15,2025, Dk Nshala amesema pamoja na kwamba msimamo wa chama hicho wa bila mabadiliko hakuna uchaguzi, amesema kilichofanywa na INEC kinapaswa kusahihishwa huku akidai kuwa nayo imeisigina Katiba.
“Walichokifanya ni upotoshaji mkubwa wa sheria na kanuni zenyewe wanazosema wamesaini na Kikubwa zaidi katiba ya sasa. Sifa za Chama kugombea au kushiriki zimeainishwa na Katiba na sifa za wagombea kugombea zimeainishwa na Katiba,” amesema.
Hata hivyo, itakumbukwa Aprili 4, 2025 INEC ilituma mialiko kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa na Serikali kukutana jijini Dodoma Aprili 12 kujadiliana na kusaini kanuni za maadili.
Vyama vilivyoitika wito na makatibu wakuu wake kusaini ni ADC, Demokrasia Makini, DP, NRA, NLD, SAU, UDPD, ADA- Tadea, AAFP, CCM, CUF, ACT-Wazalendo, Chaumma, UMD, TLP, NCCR-Mageuzi, CCK na UDP.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema hataenda na hajatuma mwakilishi kwenda kusaini kanuni hizo.
Mnyika kupitia mtandao wa kijamii wa X na baadaye katika mazungumzo kwa simu na Mwananchi, Aprili 12 alisema: “Ni vema mkaandika kwamba sijakwenda wala sijateua mtu. Habari kubwa sasa hivi ni katibu mkuu sitakwenda kusaini wala sijateua mtu.”
Msimamo huo, ulisisitizwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ambaye naye aliandika ujumbe kupitia mtandao wa X kuwa chama hicho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Msimamo wa viongozi hao unaendana na ajenda ya Chadema ya No reforms, no election ambayo chama hicho kimeshaweka wazi kwamba, kama hakutakuwa na mabadiliko ya mifumo na sheria za uchaguzi, hakutakuwa na uchaguzi.
Lakini leo Jumanne, Dk Nshala amesema kutokusaini kanuni hizo za maadili ya uchaguzi si miongoni mwa sababu iliyotajwa na Katiba iliyopitishwa na kupewa mamlaka na Bunge kwa kuitungia sheria na kwa maana hiyo, inapoka haki ya vyama vya siasa, wanachama na wagombea wao kushiriki.
“Tuliona ni upotoshaji na propaganda lakini bahati mbaya imefanywa na Tume na ilikuwa inalenga kutudhoofisha na kunyong’onyesha wanachama wa Chadema pamoja na washabiki na wapenzi wao wanaoamini katika chama hiki,” amesema Dk Nshala.
Amesema kwa kusema hivyo haimaanishi Chadema imebadili msimamo, bado wanadai mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi na kilichofanywa na mkurugenzi wa INEC ilikuwa propaganda chafu.
Amesema kama dhamira ya INEC ni njema, viongozi wake watoke hadharani wasahihishe kauli yao kuwa Chadema kimejiweka kando na hakitaruhusiwa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu, kwa kuwa hakijasaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
“Iwapo mtu anaelewa kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani, kinaipa INEC haki ya kuchapisha kanuni za uchaguzi, lakini haiipi tume mamlaka ya kuzuia mtu au chama chochote cha siasa kushiriki katika siasa au chaguzi,” amesema Dk Nshala.
Aidha, amesema ni upotoshaji na kinyume cha katiba kutaka vyama vya siasa vipitishe kanuni ambayo inatumika katika kipindi ambacho hakijaanza kisheria.
Lakini wakati Nshala akiyasema hayo, itakumbukwa Aprili 12 wakati vyama vinasaini kanuni hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisema: “Chama cha Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2025, hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.”
Alisema utaratibu wa kusaini kanuni hizo ulipangwa kuwa siku hiyo tu na hakutakuwa na siku nyingine.
“Kwa maana hiyo, chama ambacho hakikusaini hakitaweza kushiriki uchaguzi na chaguzi nyingine ndogo zitakazofuata katika kipindi cha miaka mitano, kwa sababu kanuni hizi uhai wake ni ndani ya miaka mitano kuanzia uchaguzi mkuu huu,” alifafanua Kailima.
Hata hivyo, Wakili Nshala alirejea hukumu ya kihistoria iliyotolewa na Mahakama ya Rufani Januari 31, 1995, katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Radio Tanzania Dar es Salaam na kesi nyingine dhidi ya Dk Amani Kaburu.
Kulingana naye, mahakama iliamua kwamba msingi wa Katiba ya Tanzania lazima uhakikishe uchaguzi huru na wa haki na ukiukaji wowote wa kanuni hiyo unafanya mchakato wa uchaguzi kuwa haramu.
“Uamuzi ulikuwa wazi: Tume ya Uchaguzi haiwezi kukingwa dhidi ya kuchunguzwa kisheria kama inakiuka masharti ya kikatiba au sheria za kitaifa,” Dk Nshala ameelezea, akiongeza kuwa INEC lazima ifanye kazi kikamilifu ndani ya mifumo ya kisheria na kikatiba.
Dk Nshala amesema chombo cha sasa cha uchaguzi kinachoongozwa na majaji akiwemo Mwenyekiti Jacob Mwambegele, Makamu Mwenyekiti Jaji Mbarouk (mstaafu) na Jaji Asina wa Mahakama Kuu, kingezingatia uamuzi wa mahakama unaolinda misingi ya demokrasia.
Amepinga sababu za kulazimisha vyama vya siasa kusaini kanuni za maadili kabla ya muda wake, akitolea mfano wa Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima, Aprili 12, 2025, alipotangaza kuwa toleo la mwisho wa kanuni hizo lilitumwa kwa vyama vya siasa Machi kwa ajili ya kupata maoni, na marekebisho ya mwisho yaliwasilishwa Aprili 4, kabla ya kutiwa saini Aprili 12, mwaka huu mjini Dodoma.
“Chadema haikutia saini, na kwa sababu za msingi. Sheria za uchaguzi zimevurugika, haziendani na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na haziakisi kanuni za msingi za mchakato wa uchaguzi huru na wa haki,” amesema.
Amesisitiza kuwa kushiriki katika mchakato huo wa uchaguzi wenye dosari ni sawa na usaliti wa kikatiba.
Akilizungumzia hilo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama.
“Mahakama ni mtafsiri wa mwisho inaweza kusema kipi sahihi, ni suala la kutafsiri tu Katiba imesema hivi na sheria zinasema hivi na Kanuni zinasema hivi kwa hiyo msimamo ni upi. Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi tulitoa tafsiri yetu maana yake wewe usipo saini hutashiriki kwenye uchaguzi,”amesema
Kulingana na Jaji Mwambegele taasisi hiyo haitaki kubishana na Chadema kwenye mitandao ya kijamii huku akieleza kwanza wameshatoa msimamo hawana nia ya kushiriki uchaguzi.
“Sasa mbona wanataka tuanze kubishana kwenye tafsiri, ni sawa uko na jirani yako unasema utanunua mbuzi nitakuwa namfunga na kumlishia sehemu hii halafu mnaanza kubishana tena na jirani huwezi kulishia hapa hii si sehemu yako, na kuanza kugombana wakati mbuzi mwenyewe hajanunuliwa,” amesema
Amesema amekuwa akisoma kwenye mitandano ya kijamii wakidai hawatashiriki uchaguzi huo na hawana mpango wa kusaini kanuni hizo na sababu wanazitoa kwa nini wasifanye hivyo.
Wakati huohuo, baada ya ajenda ya No reforms, no election ya Chadema kukabiliana na vikwazo katika Kanda ya Kusini, hatimaye viongozi wa chama hicho wameibukia Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Ajenda ya No reforms, no election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) yenye lengo la kuelimisha umma kuhusu hatua ya chama hicho ya kuishinikiza Serikali kubadilisha mfumo wa uchaguzi ili kuwepo kwa haki sawa kwa vyama vyote ilianza Machi 23 hadi 29, 2025 katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe na Njombe.
Baada ya mikoa hiyo, ziara za viongozi wakuu wa chama hicho, ilihamia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kuanzia Aprili 4 hadi 10, 2025 ambapo ilikumbana na kikwazo katika mkutano wa kuhitimisha ziara hiyo baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kusitisha vibali vya mikutano yote mkoani humo.
Baada ya misukosuko hiyo, hatimaye chama hicho, kimetangaza kuanza kwa kampeni hiyo katika Kanda ya Pwani kesho Aprili 16, 2025 itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche, Naibu Katibu Chadema (Bara), Aman Golugwa na viongozi wengine wa mabaraza ya chama hicho.
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu, akiwemo Boniface Jacob ambaye pia ni mwenyekiti wa kanda hiyo.
Kuendelea kwa kampeni hiyo kunakuja katika kipindi ambacho mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu yupo rumande akisubiri kukamilika kwa upelelezi wa shitaka la uhaini lililofunguliwa na Jamhuri dhidi yake.
Kampeni hiyo inaibuka tena katika nyakati ambazo chama hicho kimepigwa rungu la kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, baada ya kususia kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, zilizosainiwa jijini Dodoma Aprili 12, 2025.
Taarifa ya INEC imeibua mjadala wa wadau wa siasa na sheria, wakihoji inawezekanaje chama kilazimishwe kusaini siku iliyopangwa na tume, ilhali sheria haikuweka ukomo wa siku kwa wanaotakiwa kutia saini.