Chadema itakavyomkumbuka Balozi Mwapachu, uthubutu 2015 watajwa

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitamkumbuka Balozi Juma Mwapachu kwa uthubutu wake hususani wakati wa joto la siasa la mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika kipindi hicho, Balozi Mwapachu alifanya uamuzi wa kihistoria kwa kujiengua kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akishirikiana bega kwa bega na maelfu ya Watanzania waliokuwa wakitaka mabadiliko.

Taarifa ya Chadema iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Machi 29, 2025 imesema Mwapachu alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia mahiri, ambaye moja ya kumbukumbu zake muhimu ni utumishi wake kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kati ya mwaka 2006 – 2011.

“Kwa niaba ya chama, viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema, tunatuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Balozi Juma Mwapachu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Hakika sisi ni wa Mola na hakika kwake tutarejea,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mwapachu amefariki dunia Machi 28, 2025 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu, huku mwili wake ukitarajiwa kusafirishwa kwenda Kijiji cha Pande, Kiomoni, mkoani Tanga kwa mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho Jumapili Machi 30, 2025.

Balozi Mwapachu, mwanasiasa mkongwe na kiongozi mashuhuri nchini Tanzania alihudumu kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kati ya mwaka 2006 hadi 2011, pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.

Ameshika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika sekta ya biashara na maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwa rais wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Katika uhai wake wa kisiasa, Balozi Mwapachu alikuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, mwaka 2015 alijiondoa kwa muda, kisha 2016 akaomba kurejea tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *