
Dar es Salaam. Wakati vuguvugu kuhusu ukomo wa kusainiwa kwa kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu likishika kasi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema suala la kutosaini kanuni hizo haliwapi ‘stresi’ wala hofu, badala yake wataendelea kukomalia ajenda ya No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’.
Mbali na hilo, kimedai hatua ya Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima kuutangazia umma kuwa Chadema hakitashiriki uchaguzi kwa kutosaini kanuni hizo, kulilenga kuhamisha mjadala wa ajenda hiyo na kamwe hawataingia kwenye mtego huo.
Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa INEC, Kailima alitangaza kuwa Chadema wamejiengua wenyewe kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, jana Aprili 15, 2025 aliwataka watendaji wa INEC wajitathimini kama wanaweza kutekeleza majukumu yao baada ya kueleza kuwa, Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na kugomea kusaini kanuni za maadili.
Akijibu kauli iliyotolewa na Dk Nshala, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama.
Leo Jumatano Aprili 16, 2025 Naibu Katibu Mkuu Chadema (Bara), Aman Golugwa ameliambia Mwananchi kuwa hawana presha kuhusu msimamo wao wa kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
“Hatuna ‘stresi’ wala hatuwashwi kukimbilia kusaini kanuni za maadili, isipokuwa tutaendelea kuonyesha changamoto zilizopo katika kanuni, sheria za uchaguzi na Katiba zinazotengeneza dosari za uchaguzi.
“Tutaeleza dosari hizo pamoja na kuwahamasisha Watanzania kupaza sauti kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili watawala wazifanyie kazi,” amesema Golugwa.
Amesema Serikali imekuwa ikiunda tume mbalimbali tangu mwaka 1992 ili kuzifanyia kazi changamoto za uchaguzi, lakini zikishamaliza kazi utekelezaji wa mapendekezo yake umekuwa wa kusuasua.
“Serikali imeshindwa kuzifanyia kazi changamoto kupitia nyaraka za tume ilizoziunda yenyewe na mazungumzo ya mezani na wadau wa siasa, hivyo tunaamini Watanzania wakipiga kelele watawala watasikia.
“Tunachokifanya ni haki yetu ya msingi ili watawala wasikie kwa kelele. Niwaambie wana-Chadema na Watanzania, alichokisema Kailima si bahati mbaya bali anataka kuhamisha mjadala wa No reforms, no election na kuzua sintofahamu kwa umma, lakini hatutaingia kwenye mtego huo,” amesema Golugwa.
Amesisitiza kuwa alichokifanya Kailima ni kuhamisha goli ili Watanzania wajadili hatua ya Chadema kutoshiriki uchaguzi mkuu, badala ya kunadi ajenda ya No reforms, no election.
Mjadala uliopo kwa sasa nchini ni kuhusu uamuzi wa Chadema kususia kusaini kanuni hizo na adhabu ya kutoshiriki uchaguzi, huku wadau wakitofautiana kuhusu kifungu cha ukomo.
Hoja kubwa ya wadau ni kutaka kuona kifungu kinachoeleza ukomo wa kusaini kanuni hizo, ambapo baadhi wanaeleza kuwa si kanuni wala sheria inayoeleza ukomo huo.
Hata hivyo, kinachoeleza ni kuwa, INEC imepewa mamlaka kisheria ya kuendesha mchakato wa kusainiwa kwa kanuni hizo kwa kushirikiana na wadau kwa hatua nyingine zaidi.