Chad: Chama tawala chashinda uchaguzi wa maseneta, kulingana na matokeo ya muda

Madiwani wa manispaa na mikoa ya Chad wameitwa kwenye uchaguzi siku ya Jumanne, Februari 25, 2025, ili kuwachagua maseneta wao. Kulingana na matokeo ya muda ya Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi (ANGE), chama tawala kimeshinda kwa kura nyingi, na kupata viti 45 kati ya 46.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Na mwanahabari wetu huko N’Djamena, Olivier Monodji

Baraza la Katiba linatarajia kuidhinisha matokeo ya ANGE. Patriotic Salvation Movement (MPS), chama tawala, kimeshinda viti 45 kati ya 46. Kitawakilishwa kwa wingi katika taasisi hii mpya, Seneti. Chama pekee cha upinzani kilichowakilishwa kilikuwa chama cha Kitaifa cha Wanademokrasia wa Chad – Uamsho (RTDN-le Réveil), kinachoongozwa na Albert Pahimi, ambacho kimepata kiti kimoja katika jimbola Mayo Kebbi Magharibi, anakotoka kiongozi wa chama hicho. Wafuasi wa chama chake pia wanashtumu ukiukwaji wa sheria katika mji wa Moundou, kusini mwa nchi hiyo, ambapo wanadai kura zihesabiwe upya. Maseneta 23 waliosalia watateuliwa na Rais wa Jamhuri. Maseneta hao amabo wamechaguliwa kwa muda wa miaka sita, watawakilisha jamii zinazojitegemea.

Uchaguzi huu unafanyika bila kuwepo chama cha Transformateurs cha Waziri Mkuu wa zamani Succès Masra na kikundi cha mashauriano cha wadau wa kisiasa (Gcap) ambao waliamua kususia uchaguzi wa wabunge, mikoa na serikali za mitaa.

Akiwa na umri wa miaka 40, Rais Mahamat Idriss Déby ana njia wazi ya kutawala. Rais huyo ambaye alichaguliwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais wa Mei 2024 kwa 61% ya kura, pia ana kura nyingi katika Bunge la taifa. Chama chake cha MPS, kinashikilia viti 124 kati ya 188 bungeni.

Baada ya kuanza majukumu yao mwanzoni mwa mwezi wa Februari, wabunge hao hao mara moja watafuatiwa na madiwani wa manispaa na mikoa ambao watachukua wataanza majukumu yao leo Jumatano, na hivyo kumaliza kipindi cha mpito cha kisiasa cha miaka miwili.