Cha kujifunza kiuchumi kwenye miradi inayofadhiliwa

Uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya Marekani kusitisha ufadhili wa programu zote za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) umetia wasiwasi wa namna yake kwa wadau wa maendeleo.

Hatua hii, ambayo tunaweza kusema ni kuzuia utoaji wa mabilioni ya dola za misaada, imefichua kwamba kuna utegemezi mkubwa wa nchi za Kiafrika kwa ruzuku za kigeni katika kuendeleza sekta muhimu za kiuchumi na kijamii.

Swali kubwa tunapaswa kujiuliza, kujitafutia majibu sisi wenyewe ni kuwa, nini kitatokea pale ambapo chanzo cha maji kitakauka kabisa? Muhimu zaidi, tunawezaje kubuni vyanzo vipya vya maji bila kusubiri kutaabika na kiu au ukame? Nadhani, kuna umuhimu wa kubadili mifumo yetu ya ufadhili wa maendeleo ili kuendana na mabadiliko haya ya kidunia.

Kwa miongo kadhaa, miradi inayofadhiliwa na wafadhili imekuwa mhimili wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuanzia miradi mikubwa ya miundombinu hadi mipango ya afya ya kijamii, ruzuku za kigeni zimekuwa zikiendesha sekta mbalimbali muhimu.

Hali ni hiyohiyo kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ambayo naweza kusema programu zao nyingi au zote zinategemea ufadhili wa nje kwa kiwango kikubwa.

Uamuzi wa Wamarekani unazusha fikra mpya, kwamba hali kama hii ya usitishaji ruzuku za ufadhili inaweza kujitokeza mbeleni kwa wafadhili wengine kufuata uelekeo huo.

Changamoto iko wazi, kupungua kwa mabilioni ya fedha yaliyokuwa yanasaidia kuendesha miradi mbalimbali bila shaka kutaathiri utoaji huduma hizo, mfano afya, elimu, juhudi za kupunguza umasikini na mengineyo, ikiwa hakutakuwa na mbadala.

Na fursa yake ni kwamba inatusukuma sisi Waafrika, tukiwamo na Tanzania, kufikiria upya namna ya kuendesha mambo yetu ya kimaendeleo. Chachu ya kuanza kujitafakari mapema.

Kwa mfano, kufanyia kazi uboreshaji wa mifumo ya kodi, iwe rahisi kutabirika na kutanua wigo wa kapu la kodi, wengi walipe kiasi kuliko wachache kuwatwika zigo, pamoja na kuboresha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kidijitali na kudhibiti rushwa ili kupata fedha zitakazopunguza mwanya utakaoachwa.

Pili, ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPs) ni njia mwafaka.

 Kuanzia miradi ya miundombinu, afya na mengine, watu binafsi wenye fedha na mitaji ya kutosha wawekeze. Serikali ishiriki ikiweza, si lazima ifanye yenyewe kila kitu.

Uchumi ni kama nyumba, haujengwi kwa nguzo moja. Jukumu lake tu iunde na kuhakikisha mazingira mazuri ya biashara yanayowahakikishia wawekezaji usalama wa mitaji yao huku maendeleo yakiendelea.

Tatu, kubuni filantropia na utamaduni wa wenye nacho kuchangia maendeleo. Ni ukweli kwamba fedha nyingine zinazoletwa kwa hisani kufadhili miradi yetu si za Serikali, ni matajiri na watu wenye uwezo wamechangia.

Afrika ina tabaka la kati linalokua na idadi inayoongezeka ya wajasiriamali waliofanikiwa ambao wanaweza kuchangia kwa maendeleo ya jamii zao.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kutumia njia hii, kubuni jambo fulani la kibunifu, kwa mtindo huo wanaweza kupata sehemu ya ufadhili kuendesha programu zao na isiwe ni njia ya “kutembeza kapu.”

Nne, ujasiriamali wa kijamii ni mbadala unaoleta matumaini.  Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi katika sekta kama kilimo, elimu na afya, sekta zinazoweza kuendeshwa kwa mifumo inayojitegemea kibiashara.

Au kuwekeza sehemu ya fedha wanazopata kwenye mifuko ya uwekezaji ya pamoja, masoko ya fedha na mbinu nyingine ambazo zitawasaidia wakati wanaendeleza harakati zao za kijamii.

Tusiendelee kuishi bila mipango

Tano, programu za kurejesha kwa jamii zinazofanywa na kampuni ziwekewe uelekeo maalumu kistratejia kufadhili sekta mbalimbali za maendeleo kwa awamu.

Kwa mfano, ilivyo sasa makampuni yanachagua wapi wapeleke fedha zao kwa kulingana na masilahi yao ya kibiashara au kwa namna wanavyoona.

Vilevile, sehemu ya CSR inaweza kupewa NGOs za ndani ambazo zina uwezo wa kutekeleza miradi ya kijamii kwa ufanisi mkubwa.