CEO Mbeya City atuliza presha

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mbeya City (CEO), Ally Nnunduma amesema licha ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa FC, ila mashabiki wa kikosi hicho waendelee kutarajia mambo makubwa msimu huu.

Ally amezungumza hayo baada ya Mayanga kujiunga na Mashujaa FC kuziba nafasi ya Abdallah Mohamed ‘Baresi’, aliyetimuliwa rasmi Februari 26, mwaka huu kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya kikosi hicho, tangu msimu umeanza.

“Mayanga alikuwa kocha mzuri na tunaheshimu na kuthamini kazi kubwa aliyoifanya hadi sasa, niwatoe hofu tu kwa mashabiki zetu, licha ya kuondoka kwake ila malengo yetu ni yaleyale ya kuhakikisha msimu ujao tunaicheza Ligi Kuu Bara,” alisema.

Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Stand United, Mbeya City imecheza michezo 24, ikishinda 15, sare saba na kupoteza miwili, ikiwa nafasi ya pili na pointi 52, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 48 na kuruhusu 21.

Kikosi hicho kinachosaka tiketi ya kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, kwa sasa kiko chini Kocha Msaidizi, Patrick Mwangata anayekipambania kwa michezo iliyosalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *