
LICHA ya Ceasiaa Queens kupata ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Mlandizi Queens wamesema uchovu umewafanya kutokuwa na mchezo mzuri.
Ceasiaa iko nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 16 baada ya mechi 12 ikishinda mechi tano, sare moja na kupoteza sita ikifunga mabao 20 na kuruhusu 26.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya kupata matokeo hayo lakini timu hiyo ilicheza chini ya kiwango.
Aliongeza kuwa kutocheza ligi muda mrefu takribani mwezi mmoja na nusu kumechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kushuka kiwango jambo ambalo analifanyia kazi kuelekea mechi ijayo na JKT.
“Hatukuwa hata na mechi za kirafiki kujiboresha. Fitinesi ya wachezaji imepungua, sasa unapocheza na timu kama JKT unapaswa kuwa makini kwa sababu zinacheza kwa makini,” alisema na kuongeza:
“Tunacheza na JKT iko kwenye mbio za ubingwa wa ligi na sisi tunapambana kuhakikisha tunamaliza nafasi ya pili kwa hiyo sio mechi nyepesi na tunaamini tutaondoka na ushindi.”