
Dar/Dodoma. Mjadala wa kuitaka ukomo wa udiwani na ubunge wa viti maalumu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) umepata majibu baada ya chama hicho kuridhia vipindi visivyozidi viwili (miaka 10).
Kumekuwa na sauti za makada ndani ya nje ya chama hicho, zitaka uwekwe ukomo kwenye nafasi hizo ili kuondoa tabia ya wachache kung’ang’ania nafasi hizo na kutoa fursa kwa wanawake wengi kupata uzoefu huo.
Mathalani, kuna wabunge wa viti maalumu walioshikilia nafasi hizo kwa miaka 15, 20 na wengine 25, jambo linalodaiwa kwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa nafasi hizo, ya kuwainua wanawake wengi zaidi.
Uamuzi huo wa CCM ambao hata hiyo unaotarajia kuanza mwaka 2030, umefikiwa Jumatatu, Machi 10, 2025 katika kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyikia jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Taarifa ya Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Haji Ussi aliyoitoa leo Jumanne, Machi 11, 2025 imesema katika kikao hicho ilipokea na kujadili agenda mbili ikiwemo mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola la toleo la 2022 na Rasimu ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025-2030.
Kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imeridhia mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni hizo.
Gavu amebainisha maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi wa majimbo na udiwani wa kata/wadi.
Pia, mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge,
uwakilishi na udiwani wa viti maalum wanawake.
Kuhusu ukomo wa viti maalumu, Gavu amesema: “Kuweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kwa nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani wa viti maalum wanawake. Ukomo huo utaanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.”
Vilevile, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imepitisha Kauli Mbiurasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 isemayo, ‘Kazi na utu, tunasonga mbele.’
“Kauli mbiu hiyo inaakisi dhamira ya Chama ya kuendeleza juhudi za ujenzi wa Taifa Ienye maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa na ustawi wa watu wenye kujali UTU,” amesema
Ilivyokuwa
Kabla ya taarifa hiyo, Mwananchi lilikuwa limezngumz na wajumbe mbalimbali kujua kilichojadiliwa ambapo kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe hao, utaratibu huo unatarajiwa kuanza mwaka 2030 ukitanguliwa na mabadiliko ya kanuni za jumuiya zote za chama hicho, yaani Wazazi, Vijana-UVCCM na Wanawake-UWT.
“Mabadiliko hayo yatafanywa kwenye kanuni za jumuiya za chama si kwenye Katiba ya CCM, kwa sababu Katiba haijafafanua kuhusu viti maalumu, imeishia kutaja tu kwamba kutakuwa na viti maalumu,” amesema mjumbe huyo.
Uchambuzi wa kina kuhusu nafasi za viti maalumu, mjumbe huyo amesema umefanywa ndani ya kanuni za jumuiya ndiyo maana zenyewe ndizo zitakazofanyika maboresho ili kuendana na matakwa hayo.
“Mchakato huo utaanza mwaka 2030, hawa wabunge wa viti maalumu waliopo sasa wote watalazimika kuachia ngazi, kama watataka ubunge waende majimboni. Hao wapya watakaoingia wataruhusiwa kugombea viti maalumu kwa vipindi viwili pekee (miaka 10),” amesema.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, anakiri kuwa jambo hilo lilidokezwa, ingawa hakueleza kwa undani zaidi lilidokezwa kwa namna ipi na nini maazimio yapi yaliyofikiwa na wajumbe.
“Ni kweli jambo hilo lilidokezwa lakini siwezi kusema zaidi mambo ya vikao vya ndani, mtafute Makala anaweza kukufafanulia, lakini kwangu itakuwa viguvu, si unajua nami huenda nitakuwemo,” amesema.
Mjumbe mwingine amesema kikao hicho pia, kimepitisha kaulimbiu rasmi ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 itakayokuwa ‘Kazi na utu, tunasonga mbele.’
“Kaulimbiu hii inaakisi dhamira ya chama katika kuendeleza juhudi za kujenga Taifa lenye maendeleo jumuishi, ustawi wa watu na mshikamano wa kitaifa,” amesema.
Aidha, kikao hicho pamoja na masuala mengine, kimejadili na kupitia rasimu ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambayo pia itawasilishwa kwenye mkutano mkuu wa CCM.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya CCM (jina lake limehifadhiwa), amekiri masuala hayo kujadiliwa na kupitishwa, akisema taarifa rasmi itatolewa hivi karibuni.
“Taarifa rasmi itatolewa hivi karibuni, kwa sasa Mwenezi (Amos Makalla) amesafiri kikazi, bila shaka taarifa itatolewa, lakini la viti maalumu litaanza mwaka 2030,” amesema mjumbe huyo.
Februari 28, mwaka huu hoja ya ukomo wa viti maalumu iliibuka katika maadhimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo) jijini Dar es Salaam miaka 30 baada ya azimio la Beijing kuhusu haki za wanawake.
Katika maadhimisho hayo, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Sophia Simba alisema ifike mahali uwepo ukomo wa viti maalumu ili wanawake wengine wakalie nafasi hizo.
Sophia alisema UWT katika mikutano yake ilishapitisha viti maalumu viwe na ukomo wa miaka 10, lakini utekelezaji umekuwa mgumu.
Kufuatia kauli hiyo, Mwanasiasa mkongwe na mbunge za zamani CCM, Kate Kamba akizungumza na Mwananchi juu ya hoja hiyo alisema lengo la kuanzishwa viti maalumu lilikuwa kama shule ya mafunzo ya siasa kwa wanawake kabla hawajiangia kwenye mchakato wa kuwania majimbo.
Kamba ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema shule hiyo inapaswa kuwa na muda maalumu ili kutoa nafasi kwa wanawake wengine kujifunza na kuwa na ushiriki mkubwa katika siasa na uongozi.
“Watu wanapaswa kujua mambo ya siasa ni magumu, lazima uwe imara, ukubali kuna kushinda na kushindwa, usihofie wala kuweka kinyongo ukipata matokeo usiyoyataka. Ni vyema ukawepo muda maalumu,” alisema Kate Kamba.
Vilevile, hoja ya ukomo wa ubunge na udiwani wa viti maalumu ilijadiliwa Machi 5, mwaka huu katika mjadala wa Mwananchi X Space unaoratibiwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) uliohoji ni muhimu kuwepo ukomo wa ubunge, udiwani viti maalumu?
Katika mjadala huo, Mratibu wa Kitaifa wa Ulingo, Dk Ave-Maria Semakafu alisisitiza umuhimu wa ukomo wa nafasi hizo, huku akitaka hilo litanguliwe na kuongeza hadhi yake.
Sambamba na hilo, katika mjadala huo Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Devotha Minja aliunga mkono hoja ya kuwekwa ukomo wa ubunge huo, akitaka wanawake wengine wapewe nafasi nao ili wainuke.
Hata Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Lailah Burhan Ngozi alisema si vibaya kuwepo ukomo huo na aliwasihi wanawake wasiogope, kwa kuwa ni utaratibu utakaokwenda kuwainua wengi zaidi.
Hoja ya ukomo haikuanza leo wala jana na ilikuwa moja ya ajenda za Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Tundu Lissu katika kampeni za kuwania nafasi hiyo Desemba mwaka jana.
Lissu ambaye baadaye alishinda uenyekiti dhidi ya Freeman Mbowe, alisema nafasi hizo ziliingizwa katika siasa kuwapatia wanawake uwezo na uzoefu wa kuwa katika nafasi za uwakilishi wa wananchi, lakini wengine wamezifanya kuwa nafasi zao za kudumu.
“Tuweke ukomo ili tutoe nafasi kwa watu wengi kujifunza, kupata uwezo na uzoefu wa kushiriki kwenye siasa ili kutekeleza azma ya kuanzishwa kwa viti hivyo,”