Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewaahidi Watanzania kuweka wagombea wanaokubalika na wananchi kwenye nafasi ya udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Pia, kimeahidi kuja na ilani itakayojibu changamoto wanazopitia wananchi na hata kampeni zitakazofanywa na chama hicho katika kuwanadi wagombea wake, zitazingatia 4R zilizoasisiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa leo Machi 7, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ambaye anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Dar es Salaam akizungumza na wanachama katika ngazi za shina, kata na wilaya.
Akiwa kwenye mkutano uliofanyika Wilaya ya Temeke katika ukumbi wa Sabasaba, Makalla amesema utekelezaji wa ilani waliyoahidi wakati wanaomba ridhaa kwa wananchi mwaka 2020 ni sababu ya kuwa na uhakika wa kushinda.
“Suala la ushindi ni uhakika, nataka niwaahidi, katika uchaguzi ujao tunaenda kuweka wagombea wenye sifa na wanaokubalika, kama tulivyofanya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, kikubwa viongozi jitokezeni kuboresha taarifa zenu kwenye daftari la kudumu la mpigakura,” amesema.
Makalla ambaye ni mlezi wa chama katika mkoa huo, amesema tayari chama hicho kimeshafanya tathimini ya kina na kubaini changamoto zinazowasumbua wananchi na ilani wanayoiandaa itakuja kujibu kilio hicho.

“Tutakuja na ilani bora na itakayokonga nyoyo za wananchi wote, timu ya kuandaa ilani ipo kazini, ina watu makini na mmoja wapo anayefanya kazi hiyo ni Profesa Kitila Mkumbo, mbunge wa Ubungo. Ni mtu makini, naamini tutakuja tofauti,” amesema Makalla.
Makalla aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa Mwanza, amesema chama hicho hakiwezi kufanya makosa ndiyo maana walifanya mabadiliko ya kuongeza wajumbe wa kupiga kura za maoni na wanaona mbali.
“Tumefanya mabadiliko madogo ya Katiba yanayoongeza na kupanua demokrasia ya watu kuchagua na safari hii hata wakijitokeza madiwani 20 kutaka kugombea kata moja, kwanza tutaanza kuteua na kupeleka majina matatu tu kupigiwa kura za maoni na kupatikana jina moja,” amesema.
Kuhusu kampeni za chama chake katika uchaguzi ujao, Makalla amesema zitakuwa za kistaarabu na hawatashambulia watu kwa kuwa wanataka kudumisha amani.
“Tutafanya kampeni za kistaarabu, si za kumshambulia mtu, tutazingatia 4R zilizoasisiwa na mwenyekiti wetu, Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Awali, katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Zena Mgaya amesema wamejipanga kuhakikisha wananchi wao wanajitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
“Baada ya kumaliza, tutafanya tathimini ya kina ili tujihakikishie orodha kubwa, jambo tunalotaka ni kuhakikisha wilaya yetu inabaki kuwa ngome ya CCM,” amesema.
Kwa upande wake, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, Ibrahim Msengi amewataka wanachama hao kudumisha umoja wanapoelekea kwenye kura za maoni ili kupata wagombea bora.