
Dar/Rukwa. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema wanaopanga kuwapigia kura ya hapana wagombea wa chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika Novemba Jumatano 27, 2024 watasubiri sana.
Makalla amefananisha hatua hiyo ni sawa na mtu anayesubiri meli katika uwanja wa ndege, akimaanisha jambo hilo halitawekana.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2024, hakuna utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa badala yake atapigiwa kura ya hapana na wananchi.
Kwa nyakati tofauti, ACT – Wazalendo imesema itashirikiana na vyama vingine kupiga kura ya hapana kwa maeneo ambayo hawana wagombea, vivyo hivyo kwa Chadema ambayo imewataka wananchi kupiga kura ya hapana kwa CCM.
Makalla ameeleza hayo jana Jumatano Novemba 20, 2024 akizindua kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa Mkoa wa Dar es Salaam zilizofanyika Uwanja wa Bulyaga wilayani Temeke jijini hapa.
Katika maelezo yake, Makalla amesema,”Hujasimamisha wagombea halafu unapanga jitihada na nguvu ambazo hukuweka mgombea au maarifa ambayo hukuweka mgombea halafu unasubiri kumuangusha mtu wa CCM.”
“Huyu ni sawa na mtu anayesubiri meli uwanja wa ndege, niwaombe WanaCCM maeneo yote ambayo tuna mgombea peke yetu kampeni ziendelee kuhakikisha wagombea wanapata kura zote za ndio,” amesema Makalla.
CCM ndio chama kilichofanikiwa kuweka wagombea katika vijiji, mitaa na vitongoji vyote, huku upinzani ukishindwa kufikia lengo hilo kwa sababu mbalimbali zikiwemo za wagombea wao kuenguliwa na rasilimali fedha.
Sababu za wagombea CCM kuchaguliwa
Katika mkutano huo, Makalla metaja sababu tatu kwa nini Watanzania wanapaswa kuwachagua wagombea wa chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Sababu hizo ni CCM ndio inayotekeleza ilani ya uchaguzi 2020/25, mafanikio ya utelelezaji wa miradi mbalimbali ambayo ni matokeo ya wa ushirikiano na viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji, madiwani na wabunge.
Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, amesema sababu nyingine ni tamko kuhusu uchaguzi huo na mambo ya kuzingatia pamoja na chama hicho kuwa na dhamana na wajibu kuwatumikia Watanzania.
“Licha ya changamoto ndogondogo zilizopo lakini mafanikio yapo hakuna miradi iliyotekelezwa ya ujenzi wa madarasa, pasipo ushirikiano wa serikali za mitaa.
“Kama tulifanikiwa kufanya kazi na watu hawa (viongozi wanaomaliza muda wao) basi CCM imewaletea tena watu sahihi, tunaomba muamini wabunge na madiwani watafanya nao kazi vizuri,” amesema Makalla.
Makalla amesema wagombea wa CCM watakaochaguliwa wataungana na madiwani, wabunge na Rais (Samia Suluhu Hassan), katika kuteleleza majukumu ya kuwaletea maendeleo Watanzania tofauti na vyama vingine.
“Wagombea wetu watakuwa wanajinadi, lakini wana tamko la Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo mnaweza mkapima wagombea wa vyama vingine. Nawaomba chagueni wagombea wa CCM,” amesema Makalla.
Makalla amesisitiza CCM itafanya kampeni pasipo matusi wala kejeli kwa sababu wana hoja za msingi za kuwashawishi Watanzania kukipigia kura kwa mara nyingine.
“Tunaamini mtu asiyekuwa na hoja atafanya kampeni za vitisho, kejeli na kutukana, lakini CCM itawajibu kwa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuwashawishi wananchi kwa hoja ili wapime,” amesema Makalla.
Kwa mujibu wa Makalla, CCM ndio chama chenye dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo kupitia madiwani wao watakaoshirikia na wenyeviti wa serikali za mitaa katika kutumikia makundi mbalimbali.
Umuhimu wa serikali za mitaa
Makalla amesema viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji ni muhimu kwa sababu wanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja ikiwemo kutoa huduma za barua za utambulisho, ndio viongozi wanaojua changamoto za kaya.
“Viongozi tunaoenda kuwachagua ndio kimbilio letu la kutupa barua za utambulisho, watatuelekeza maeneo ya kujenga, ikiwemo miradi ya maendeleo, ndio wanaotusaidia kutupa barua kwenda benki,” amesema Makalla.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi amewaomba wananchi wa mkoa wa huo kuwachagua wagombea wa chama hicho ili kuwaletea maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amewahakikishia wananchi wa Temeke kwamba ulinzi utaimarishwa kuanzia kampeni, kupiga kura hadi kutangaza matokeo ya washindi wa mchakato huo.
Alichokisema Nape
Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa, Nape Nnauye akiwa mkoani Rukwa aliwaagiza wagombea kufanya kampeni za kistaarabu zenye kuchochea maendeleo ya wananchi.
Nape ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni hizo mkoani humo amesema CCM wamejipanga kuhakikisha wanashika dola kwa kishindo kwa kufanya kampeni kwa lengo la kunadi sera zao.
Nape amewataka kusikiliza kampeni na kupima kama wanaweza na tarehe 27 kufanya uamuzi wa kupiga kura.
Amesema watahakikisha uchaguzi unafanyika kwa huru na haki na CCM kinashinda kwa kura nyingi.
“Tunajiamini tumesimama imara kuhakikisha tunashinda, yapo mambo tunayojivunia yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Awali akimkaribisha Nape, Mbunge Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly amesema kila mwananchi ana wajibu na haki ya kumchagua kiongozi anayemtaka.
Katika mitaa yote 165, vijiji 339 na votongoji 1,816 chama hicho kimewasimamisha wagombea wote pamoja na wajumbe wake.
Mwenyekiti CCM Mkoa wa Rukwa, Silaf Maufi amesema chama kipo imara na wana imani kubwa watashinda kwa kishindo.
Maufi amevitaka vyama vya upinzani kufanya kampeni zenye kuleta tija na maslahi kwa jamii na sio kutumia nguvu kubwa kufanya vurugu.