
Dar es Salaam. Kesi dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwashirikisha watoto katika siasa imerudishwa tena mahakamani, mara hii ikipelekwa Mahakama ya Rufani baada ya Mahakama Kuu kujivua mamlaka ya kuisikiliza.
Awali kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam (wakati huo, sasa Masjala Ndogo) na mwanaharakati, Kumbusho Dawson Kagine dhidi ya Baraza la wadhamini wa CCM, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo yenye maombi mchanganyiko namba 1222/2024, Kagine anayejitambulisha kuwa mtetezi wa haki za binadamu na watoto alidai hatua ya CCM kuwahusisha watoto katika shughuli za kisiasa, ni ukiukwaji wa katiba, sheria na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama.
Pia alihoji kitendo cha msajili na AG kushindwa kutekeleza wajibu wao wa usimamizi kwa kuruhusu ukiukwaji uliofanywa na wadhamini wa CCM bila kuhoji kinyume na mamlaka yake ya udhibiti vyama vya siasa na shughuli za kisiasa nchini.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Angelo Rumisha Oktoba 3, 2024 ilisema suala hilo lipo katika mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye anapaswa kuombwa kwanza kuyashuhilikia kabla ya kwenda mahakamani.
Hata hivyo, Kagine hakukubaliana na uamuzi huo, badala yake amerudi tena mahakamani, sasa akibisha hodi katika milango ya Mahakama ya Rufani ambako amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Wakili wa Kagine, John Seka amelieleza Mwananchi leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 kuwa tayari wameshawasilisha notisi ya rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.
Wakili Seka amesema wameamua kwenda Mahakama ya Rufani kwa kuwa wanaamini Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Akizungumzia maelekezo ya mahakama hiyo kuwa malalamiko hayo yalipaswa yawasilishwe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwanza ambaye ana mamlaka ya awali ya kuchukua hatua, Wakili Seka amesema hilo halitekelezeki.
“Katika mazingira ambayo mlalamikaji si mwanchama wa chama cha siasa, si rahisi kumpelekea Msajili wa Vyama vya Siasa malalamiko kama haya na akayafanyia kazi. Ndio maana sisi tuliamua kuja mahakamani moja kwa moja, maana mahakama ina mamlaka mapana,” amesema Wakili Seka na kuongeza;
“Kwa hiyo tumerudi tena mahakamani, tumekata rufaa Mahakama ya Rufani, na tayari tumeshawasilisha notisi tangu juma lililopita maana tunaamini kwa mazingira ya shauri hili, mahakama ndiko jukwaa sahihi la kuliamua.”
Kagine alifungua kesi hiyo baada ya uchaguzi wa viongozi wa Chipukizi wa CCM uliofanyika Desemba 2023, ambao picha jongefu (video) zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikiwaonesha baadhi ya watoto waliokuwa wakigombea nafasi hizo wakitoa sera na kuomba kura.
Chipukizi ni kundi la watoto wenye umri wa chini ya miaka 18, ambao wako kwenye Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji chini ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na limekuwepo kwa miaka mingi.
Hata hivyo, uchaguzi huo uliibua mjadala mkali mitandaoni, huku makundi mawili yakisigana kimtazamo, wengine wakipinga hatua hiyo kuwa ni kinyume cha sheria na kwamba watoto hao wanapaswa waachwe wajielekeze kwenye masomo na wengine wakiunga mkono.
Katika kesi hiyo, Kagine alidai kuwa kwa mtizamo wake ni kinyume na sheria kuwahusisha watoto wenye umri chini ya miaka 18 katika shughuli za kisiasa na za chama kikamilifu.
Alidai CCM wanakiuka vifungu vya 6C (1) (b) na 10A (a) vya Sheria ya Vyama vya Siasa, Ibara ya 7 ya katiba yake na maslahi ya watoto chini ya kifungu cha 4(2) cha sheria ya mtoto na chini ya sheria ya kimataifa.
Hivyo, aliiomba mahakama itoe amri kumwelekeza msajili wa vyama kusimamia kutokuhusishwa kwa watoto chini ya miaka 18 katika shughuli za kisiasa na za CCM, na imwelekeze msajili kukichukulia hatua za kiutawala CCM kwa vitendo hivyo.
CCM katika majibu yake ilidai kuwa kulingana na Ibara ya 7 ya Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto na kifungu cha 11 cha Sheria ya Mtoto, kama ilivyorekebishwa mwaka 2019, mtoto ana haki ya kueleza maoni yake na kusikilizwa.
Walichokisema mawakili
Wakili wa Kagine, Seka alieleza sheria inazuia mtu wa umri wa chini ya miaka 21 kugombea uongozi isipokuwa kuanzia umri huo na kuendelea.
Alidai kuwa CCM inakinzana na sheria inayosimamia vyama vya siasa, hasa masharti ya vifungu vya 6C (1) (b) na 10A (a), ambayo Ibara ya 3(2) ya Katiba ya Nchi inaelekeza izingatiwe, na kwamba msajili pia alipuuza ukiukwaji huo.
Kwa upande wake, wakili wa CCM, Fabian Donatus alidai watoto chini ya miaka 18 wameunda jumuiya inayoitwa Chipukizi ambayo imekuwepo tangu miaka ya 1970 na kwamba watoto hao wanashiriki matukio ya kitaifa kama Siku ya Uhuru na ya Muungano kuonyesha uzalendo wao.
Alidai kuwa ushiriki wao huo katika matukio hayo unaendana na Ibara ya 29(c) na (d) ya Mkataba wa Haki na Ustawi wa Mtoto, ambayo inahimiza Serikali (za Nchi wanachama) kuwaelimisha watoto kuhusu utambulisho wa utamaduni wake na maadili.
Hata hivyo, Wakili Donatus alidai watoto hao si wanachama wa CCM, kwa kuwa uanachama hautambuliwi kwa kuvaa mavazi ya chama, bali kwa kumbukumbu zinazohofadhiwa na msajili.
Alidai sheria ikiwemo Katiba ya Tanzania na mikataba ya kimataifa inaruhusu watoto kuunda jumuiya, hivyo akaiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo.
Wakili wa Serikali, Daniel Nyakiha alidai kuwa kuwa mwelekeo wa madai ya Kagine ni vitendo vya CCM kuwashirikisha watoto katika siasa kukiuka sheria na si sheria yenyewe inakiuka katiba, basi madai yake yako nje ya mamlaka ya Mahakama ya Kikatiba.
Alichokisema Jaji Rumisha
Jaji Rumisha akirejea msimamo wa mahakama hiyo katika mashauri mbalimbali, alisema utaratibu wa mashauri ya kikatiba haupaswi kutimika kama kuna njia mbadala ambazo zinapaswa zitumike kwanza.
Alisema msimamo huo unalenga kulinda utakatifu wa asili wa katiba na kupeleka mahakamani mashauri ambayo yana umuhimu mkubwa na kwamba inapaswa kutumika kuomba nafuu pale tu ambapo hakuna tiba ya kutosha katika sheria ya kawaida.
Alifafanua sheria ya vyama vya siasa inatoa utaratibu wa udhibiti na utekelezaji wa sheria na kwamba kifungu cha 19 cha sheria hiyo kinampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka mapana, yakiwemo kusimamisha au kukiondolea usajili chama cha siasa kilichovunja sheria.
Jaji Rumisha alisema ingawa Kagine anamlalamikia msajili kutoichukulia hatua CCM kwa ukiukaji huo wa sheria anaodai, lakini hakuna ushahidi kama aliwahi kumuomba achukue hatua kabla ya kuomba nafuu za Kikatiba.