Geita. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema Tanzania ni nchi huru yenye mamlaka kamili, hivyo ina uwezo wa kuamuru mgeni gani aingie nchini na nani asiingie.
“Nimeona kwenye mitandao ya kijamii, oooh oooh… mara wanaharakati mara kina Martha Karua na wenzake wamezuiwa uwanja wa ndege walikuwa wanakuja kwenye kesi ya Tundu Lissu…, niseme Tanzania ni Dola iliyokamilika yenye mamlaka kamili,” amesema Makalla.
Amesema Tanzania ina uwezo wa kuruhusu au kutoruhusu mgeni yeyote kuingia kwa sababu ni nchi huru haishinikizwi kufanya chochote katika hilo.
Makalla ameyasema hayo leo Jumanne Mei 20, 2025 alipokuwa akiwasalimia wananchi wa Katoro na Ludete mkoani Geita anakoendelea na ziara yake ya kikazi mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Jana Jumatatu Rais Samia Suluhu Hassan alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kutotoa nafasi kwa wanaharakati kutoka mataifa mengine kuja kuingilia mambo ya ndani ya nchi na kuchochea vurugu.
“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku. Sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije kutuharibia huku.
“Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika ni hii (Tanzania), watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,” alisisitiza Rais Samia na kuongeza;
“Niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na Wizara ya Mambo ya Nje, kutotoa nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kufanya vurugu hapa. Hapana.”

Rais Samia alieleza hayo wakati mwanasiasa wa Kenya, Martha Karua na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga wakidaiwa kuzuiliwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Wakenya hao waliingia nchini juzi kwa lengo a kuja kusikiliza kesi ya uhaini na kuchapisha taarifa za uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Kesi hiyo ilisikilizwa jana na kuahirishwa hadi Juni 2, 2025.
Makalla amesema hakuna sheria yoyote duniani inayoweza kulishinikiza Taifa huru likiwemo Tanzania kwamba lazima mtu fulani apokelewe.
Amesema idara ya uhamiaji nchini ina mamlaka ya kuruhusu au kutomruhusu raia wa kigeni kuingia nchini, hivyo taasisi haiwezi kushinikizwa kuruhusu watu kuingia.
“Huyu Martha Karua ni kiongozi wa upinzani wa chama cha ukombozi kule Kenya, sasa Tanzania tumeshakombolewa tupo huru, yeye ni mwanaharakati, nimuulize Karua hivi kule Kenya ilivyotokea kina Miguna Miguna kuzuiliwa alienda kumtetea?
“Uwakili wake una maana sana akija Tanzania au kwenda Uganda, uhisani unaanzia nyumbani, mbona wengine wakipata matatizo kule Kenya hawatetei, anakuja kuja Tanzania. Tumeshitukia yeye ni mwanaharakati ana rekodi ambazo hazijafutwa huko Kenya,” amesema Makalla.
Mwenezi huyo, amesema Tanzania na Kenya ni mataifa yenye undugu na ushirikiano bora na yataendelea kuwa hivyo.
“Uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ni mzuri kuliko wakati wowote, tunategemeana katika biashara, sisi ni ndugu na wanaosema oooh…huu ndio mwanzo wa Afrika Mashariki kufa, haifi ng’o kwa sababu hiyo,”
“Nimelisema hili ili kumpa nguvu Rais wetu Samia Suluhu Hassan, aliyeapa kuilinda Tanzania, mipaka na kudumisha amani. Niwahakikishie Watanzania nchi yetu ni salama, itakwenda katika uchaguzi ikiwa salama zaidi,” amesema Makalla.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela
Chama hicho tawala si mara kwanza kumshukia Karua, Aprili 24, 2025 Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (bara), Stephen Wasira alimjia juu mwanasheria na mwanasiasa huyo, akimataka kuacha kujipima uzito na CCM, kutokana kauli yake kuishauri Serikali kufanya mazungumzo kuhusu mifumo ya uchaguzi.
‘Geita imepiga hatua za maendeleo’
Katika mkutano huo, Makalla amesema baadhi ya watu (bila kuwataja majina) waliopita Geita hasa eneo la Katoro wanasema hakuna maendeleo yaliyofanyika jambo ambalo si kweli.
Kwa mujibu wa Makalla kuna maendeleo makubwa yanayonekana katika mkoa huo, kuanzia sekta za afya, madini, barabara, elimu, akiwataka wakazi wa mkoa huo kuwapuuza wanaosema hakuna kitu kilichofanyika.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema eneo la Katoro lilikuwa na changamoto ya taa za barabarani, lakini Serikali imeitatua na kuwezesha wananchi kufanya biashara nyakati za usiku.
Mbali na hilo, Serikali inaendelea na mradi wa barabara za lami za ndani ili kuboresha miundombinu hiyo na kuondokana na njia za vumbi.
Magesa kugombea Katoro
Mbunge wa Busanda, Tumain Magesa ametumia nafasi ya kuwasalimia wananchi wa Katoro na kutangaza mbele ya Makalla kwamba katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, atawania tena ubunge katika jimbo hilo jipya.