Dar es Salaam. Wakati joto la uchaguzi mkuu 2025 likiendelea kupanda ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla ametoa maelekezo kwa watendaji kuwadhibiti viongozi wanaowapangua mabalozi wa nyumba kumi na kuwaweka wapya.
Inadaiwa kuwa, mbio hizo zimeibuka ikiwa imebakia miezi mitatu kabla ya kuingia kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama kusaka wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wameshatoa kauli za onyo na kuwatahadharisha wanaotaka kuwania nafasi katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, wasubiri muda ufike waanze kujinadi.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi ni miongoni mwa viongozi waandamizi waliowahi kutoa angalizo hilo.
Machi mosi 2025, Katibu wa NEC, Organaizesheni ya Taifa, Issa Gavu akiwa mkoani Mtwara alitumia jukwaa la uzinduzi wa ofisi ya Wilaya ya Newala kuonya mwanachama yeyote atakayeonekana anajipitisha jimboni au kwenye kata kwa lengo la kujinadi, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Leo Jumanne, Machi 4, 2025, Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla amerejea tena kutoa maelekezo hayo ya onyo katika ziara yake aliyoianza leo jijini Dar es Salaam itakayokamilika Machi 8, 2025.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa ndani na viongozi wa jumuiya zote kuanzia ngazi ya shina, tawi, mitaa na kata, Wilaya ya Kinondoni uliofanyika ukumbi wa Kiramuu Mbezi Shule, Makalla ametoa maelekezo kwa watendaji wa chama hicho kuwadhibiti wote wanaofanya mchezo huo.
Amesema chama kimeshapokea malalamiko kutoka kwenye wilaya moja (hakutaka kuitaja).
“Kutokana na hilo, natoa maelekezo kwa makatibu ngazi zote kuweka rekodi zao na wawakemee viongozi wanaowapangua mabalozi wa nyumba kumi na kuwaweka wapya, kumbukeni hawa walishachaguliwa, halafu mtu anapita kupangua nakusema tuweke tunaoendana nao, haiwezekani,” amesema Makalla ambaye ni mlezi pia wa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla leo Machi 4, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa Viongozi wa Chama na Jumuiya ngazi ya Shina, Tawi, Kata na Wilaya katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano katika mkoa huo.
Makalla amesema mabalozi hao ndiyo waliowasaidia kushinda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
“Baada ya kupata taarifa hiyo, tuliwaandikia barua kali ya onyo kuwaonya, lazima mjue chama chetu kimeamua kuongeza watu wa kushiriki kupiga kura za maoni kwa lengo la kukuza demokrasia, lakini kuondoa mianya ya rushwa,” amesema kiongozi huyo.
Amesema CCM haitaki kuona jambo hilo likifanyika na wanajua wanacheza rafu hizo kwa sababu ya utashi wa baadhi ya watu wenye uchu wa madaraka, wakitaka kupanga safu kwa ajili ya uchaguzi ujao.
“Mabalozi wakati nawatetea, na ninyi mchangamke, msiniangushe baada ya tamko hili, msikubali kutenguliwa, haiwezekani suala la uteuzi na utenguzi liendelee kufanyika, nawakemea watendaji, lakini na ninyi nawaomba msiwakane watu wenu, endeleeni kushirikiana nao,” amesema Makalla.
Katika mkutano huo, ameonya pia makada wanaoendelea kujipitisha kwenye majimbo.
Amesema ni vema wakaacha huku akiwaagiza watendaji wakiwabaini watunze kumbukumbu zao, ili wakati wa mchujo ukifika, watatumia kigezo hicho kuwaengua.
Akizungumzia lengo lingine la ziara hiyo, amesema ni kuwahamasisha viongozi hao waendelee kuwahimiza wanachama na umma kwa jumla, kujitokeza kwa wingi katika uboreshaji wa taarifa zao kwenye daftari la mpigakura ambalo kwa Mkoa wa Dar es Salaam utaanza Machi 17 mpaka 23, mwaka huu.
“Wanaojipitisha pitisha rekodi zenu zinatunzwa, naagiza makatibu na watendaji wote muwabaini tutazitumia orodha hizo kwenye kufanya mchujo wa wagombea, Waliopo sasa ni wabunge madiwani wetu waachwe wafanye kazi hadi muda wao utakapofika,” amesema.
Amesema wabunge wanaojiandaa kwenye Bunge la bajeti ni lazima wawalinde kwa sababu wanabeba maono ya wananchi, haiwezekani wanaendelea na shughuli hiyo lakini jimboni kuna mwingine anakazana kwenye eneo lake kujiuza.
“Kumekuwa na fitina fitina na fitina mtu anakuja gia ya kwanza mbunge wenu mara ya mwisho mlimuona lini huku unajua kabisa kuna kamati za maendeleo, inakuwaje wewe unauliza swali la namna hiyo ni fitina ya bure,” amesema.
Makalla amesema baada kuona mtindo huo unakuja kwa kasi aliwaelekeza watendaji na kamati za siasa ngazi zote, kuweka rekodi za watu wote wanaojipitisha na kufanya kampeni kwa kuwa, watawarahisishia kwenye mchujo ili wasipigiwe kura za maoni.
” Nafasi zipo mtaomba, lakini kwa sasa naelekeza muache kuwasumbua wabunge na madiwani wafanye kazi zao,” amesema.
Pia, amesema ni muhimu wakaa kimya waendelee kuusoma mchezo huku akisema mara nyingi samaki anayeangaika muda wote ndiye ananaswa kwenye ndoana.
“Kuna watu wamejiweka weka kukamatwa na ndoana sasa hatutakuwa na huruma kwenye mchujo wa kura za maoni,” amesema.
Kutokana na maagizo hayo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam,(UDSM) Dk Richard Mbunda amesema msingi wa vurugu zinazoendelea kushuhudiwa sehemu mbalimbali, zimesababishwa na makada wengi kuvurugwa chanzo kikiwa ni mkutano uliofanyika Dodoma.
Amesema kumpitisha mgombea mmoja kwenye nafasi ya urais wa Jamhuri ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wengi hawakupendezwa nacho, jambo linalofanya kila mmoja kutaka kutumia ubabe ule ule kupanga safu.
“Siamini kama wataweza kuwaengua wagombea ni jambo ambalo hawataweza na nakuambia uchaguzi ujao naona kabisa rushwa kubwa itatumika mara mbili ya kile kilichofanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa,” amesema Dk Mbunda.
Amesema maneno wanayoongea watendaji wa chama hicho ni kama danganya toto huku akieleza iwapo watasimama kwenye kanuni labda haki itatendeka.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla leo Machi 4, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa Viongozi wa Chama na Jumuiya ngazi ya Shina, Tawi, Kata na Wilaya katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano katika mkoa huo.
Mtazamo huo wa Dk Mbunda, umetofautiana na Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, Dk Ponsian Ntui akisema haoni tatizo kwa baadhi ya watu kuanza kujipitisha kwa kuwa, hawawezi kuwa kikwazo kwa walipo madarakani.
“Wanazuiaje utekelezaji wa majukumu kwa waliopo madarakani? Kuendelea kufanya kazi, kikubwa watu wafanye kazi na utendaji wako kwa wananchi utakubeba, na kinachoendelea ni hofu ya bure,”amesema.
Dk Ntui amesema madiwani na wabunge wengi walijisahau katika kipindi chote, hawakufanya kazi waliyotumwa na wananchi na wanahisi watu wakijitokeza wanaweza kuwanyang’anya viti.
“Nafikiri jambo hili alipaswi kuongelewa na chama au Serikali kwani wanaofanya uamuzi ni wananchi na kwa kuwa demokrasia inakua waachwe wafanye wapime wenyewe,”amesema Dk Ntui.
Katika hatua nyingine, Makalla alihoji mikakati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kudai ajenda yao ya ‘No reform no election’ haina hoja.
Hata hivyo, ajenda ya mabadiliko ya kushinikiza mifumo huru ya uchaguzi ndani ya Chadema ilipitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 21 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.
“Tunawaambia mabadiliko yameshafanyika na uchaguzi unaenda kufanyika, wasiposhiriki uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kinaenda kufa; ule ukubwa wa chama kikubwa cha upinzani utakuwa umepotea na watapoteza ndoto za wenye nia ya kugombea,”amesema Makalla.
Amesema mpango huo unaolenga kuishinikiza Serikali kufanya maboresho ya mifumo huru, uchaguzi hauwezi kufanikiwa huku akieleza wanachojua wao mabadiliko yalishafanyika.