CCM yajibu aliko Wasira

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema kutoonekana kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Stephen Wasira ni suala la ratiba na si vinginevyo kama inavyoelezwa.

Ufafanuzi wa Makalla unajibu kauli mbalimbali zinazoibuliwa katika mitandao ya kijamii kutoka kwa baadhi ya wadau wakihoji, yuko wapi Wasira ambaye hakuonekana kwa siku kadhaa hadharani.

Baadhi wamekwenda mbali zaidi na kusema, pamoja na kutoonekana majukwaani, hakuonekana hata katika msiba wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.

Msuya (94) alifariki dunia Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo ambayo yalimsumbua kwa kipindi kirefu.

Kwa mara ya mwisho, Wasira alionekana hadharani alipofanya ziara yake katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma na baada ya hapo hakuonekana tena.

Makalla amejibu swali hilo leo, Jumamosi Mei 17, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu Mei 29 na 30, 2025.

Amesema ni kawaida kwa kiongozi kupumzika baada ya ziara na shughuli mbalimbali za kiofisi kama ambavyo mwingine yeyote angefanya.

“Ni Mzee hana jambo lolote kwa hiyo ni ratiba kwamba bwana nitafanya hapa, nikikamilisha nitapumzika kuna jambo la familia, kuona watoto, hata mimi mwenyewe lazima nijiwekee hilo,” amesema Makalla.

Akifafanua zaidi, amesema hata yeye amekuwa akipumzika baada ya ziara, anafanya kazi nyingine za kiofisi na vikao vya kawaida.

“Kwa hiyo hata mimi nikipotea wiki moja mtasema mwenezi amekata moto au amekata pumzi hapana bwana ni suala la ratiba,” amesema.

Mwananchi limemtafuta Wasira kwa simu haikuwa hewani na hata alipopigiwa kwa njia ya WhatsApp iliita bila majibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *