CCM, Watanzania tunawajibika kusaidia kuujenga upinzani imara

Nimemsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu katika mahojiano ya dakika 45 na kituo cha televisheni cha ITV kuhusu falsafa yake ya ‘No Reforms No Election’ (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi).

Ingawa ana hoja za msingi, uwasilishaji wake unategemea hoja za nguvu badala ya nguvu ya hoja.

Hoja za nguvu hutokea pale mtu anapotoa hoja sahihi lakini akaitetea kwa kulazimisha, badala ya kutumia nguvu ya hoja yenyewe kuaminika hata kwa wasiokubaliana naye.

Ni muhimu kwa Lissu, Chadema na wapinzani wengine kujifunza jinsi ya kujenga hoja zenye nguvu badala ya kushinikiza kwa vitisho.

Hata katika mchezo wa ngumi, mtu wa uzito wa chini akikabiliana na mwenye uzito mkubwa ataumia.

Uchaguzi wa Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa na changamoto kubwa kwa upinzani na matokeo yake yalishuhudia Chadema ikipungua kutoka wabunge zaidi ya 100 hadi wawili. Ili kupata Bunge lenye kambi rasmi ya upinzani, ni lazima wapinzani wasaidiwe.

Madai ya Lissu kuhusu No Reforms yana msingi, kwa sababu kuna haja ya kufanyika kwa mabadiliko muhimu ya Katiba ili uchaguzi wa mwaka huu uwe huru na wa haki.

Hata hivyo, kauli ya No Election ni kauli ya kibabe inayodai kuwa bila mabadiliko hakutakuwa na uchaguzi, kana kwamba Chadema ina mamlaka ya kuamua.

Ukweli ni kwamba, hakuna chama kinachoweza kuzuia uchaguzi kufanyika, hivyo hii ni siasa ya hadaa.

Lissu akiwa ndiye Mwenyekiti wa Chadema kwa sasa, anapaswa kuachana na mbinu za uanaharakati na kufuata siasa za kimkakati. Siasa siyo kupambana tu, bali ni kujenga ushawishi wa kushinda uchaguzi.

Bila mabadiliko haya, upinzani utajikanganya na historia ya 2020 itajirudia, jambo litakalolinyima Bunge kambi rasmi ya upinzani, hali inayodhuru siyo tu Chadema, bali pia Chama cha Mapinduzi (CCM), Bunge na taifa kwa ujumla.

Kukosekana kwa kambi rasmi ya upinzani bungeni kumechangia kudhoofika kwa Bunge, kiasi cha kupitisha miswada na mikataba batili bila changamoto yoyote.

Upinzani makini ungeweza kuzuia matendo haya kwa kupangua hoja kwa hoja mbadala. Tanzania inahitaji upinzani madhubuti, kwa kuwa bila upinzani imara, hata chama tawala hukosa changamoto ya kuimarika.

Upinzani wa kweli haupingi tu kwa sababu ya kupinga, bali unatumia hoja mbadala kuonesha upungufu wa serikali.

Lengo kuu la vyama vya siasa ni kushika dola na kuongoza serikali, hivyo ni lazima wapinzani waweke mikakati imara badala ya kushiriki siasa za matukio zisizo na malengo ya muda mrefu.

Ukosefu wa upinzani imara umeifanya Tanzania kuwa na chama kimoja chenye nguvu ambacho ni CCM, na vyama vingi vya upinzani vinavyoshindwa kujijenga kama mbadala madhubuti wa uongozi.

Ili kujenga upinzani makini, ni lazima wapinzani wajifunze siasa mahiri badala ya kupiga kelele zisizo na tija.

Badala ya kutegemea siasa za matumaini hewa, wanapaswa kukumbatia siasa za ukweli, kwa kuzingatia uhalisia na kuchagua mapambano yanayowezekana.

Natoa wito kwa Watanzania wote, wakiwamo wanachama wa CCM wenye nia njema kwa taifa, kusaidia kujenga upinzani imara, makini na wenye afya.

Kama ilivyokuwa wakati wa Rais Julius Nyerere, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli waliowahi kuwateua wapinzani kushika nyadhifa mbalimbali, hakuna dhambi kusaidia upinzani kuwa na mwelekeo sahihi kwa maendeleo ya taifa.

Kazi ya chama tawala ni kuongoza serikali kwa kutumia ilani yake ya uchaguzi.

Baada ya uchaguzi, kazi ya upinzani makini duniani kote ni kupinga sera za chama tawala kwa hoja mbadala na siyo kupinga tu alimradi kupinga.

Na sisi wengine tuendelee kujitokeza kuwasaidia hawa wapinzani na vyama vyao kufanya siasa safi, siasa za maendeleo, siasa zenye tija.

Lengo la kufanya hivyo kutawasaidia kuepuka hizi siasa za kiuanaharakati usio na tija kwa maendeleo ya nchi na Watanzania kwa jumla.