Zanzibar. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema chama kitawasimamisha kazi na wengine kuwapeleka katika kamati za usalama na maadili watendaji na viongozi wake watakaojihusisha na vitendo vya kuhujumu mchakato wa uchaguzi wa ndani wa kura za maoni.
Kura hizo za maoni zinalenga kuwapata wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani watakowakilisha chama katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Amesema CCM itaanza kwa kile alichokiita usafi wa ndani, kwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watendaji wake wanaofanya udalali wa kisiasa kwa masilahi yao binafsi na wengine kutumiwa na baadhi ya watia nia kuvunja taratibu na miongozo ya CCM kwa ajili ya maslahi binafsi.
“Kwa uwazi, fagio hilo litakuwa ni maandalizi ya kuhakikisha tunapata viongozi bora wasiokuwa na chembechembe za rushwa, udalali wa kisiasa ndani ya chama na jumuiya zake na viongozi wenye utu na uzalendo wa kusimamia na kuleta maendeleo ya wananchi wote,” amesema.

Dk Dimwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 29, 2025 wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za matawi, wadi, majimbo ya Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba katika mwendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk Dimwa, anatumia ziara hiyo kutoa onyo kwa wote walioanza kupitia wagombea na kubeba mikoba yao kabla ya chama kutoa ruhusa ya kuanza kwa kampeni, kuhakikisha wanaacha tabia hizo na kuheshimu utaratibu uliowekwa.
Amesema kupitia kikao cha Mkutano Mkuu maalum wa CCM uliofanyika Januari 18 na19, 2025 kimefanya mabadiliko ya katiba yake ya 1977 toleo la 2022 kwa kuongeza idadi ya wapiga kura katika mchakato wa ndani wa kura za maoni ili kuongeza upana wa uwazi, uhuru na demokrasia ndani ya chama.
“Natumia ziara hii kutoa onyo kwa watendaji wote na viongozi waliopo katika usimamizi wa chama kuacha tabia ya kutumiwa na watu kuharibu utaratibu na kanuni za chama, hatuwezi kuacha vitendo hivi viendelee tunataka kupata wagombea safi watakaouzika na kukubalika uchaguzi ujao,” ameongeza.
Amesema: “Lazima Chama kirudi kwa wanachama wenyewe, hiki sio chama cha wapiga ‘deal’ (wababaishaji) bali ni chama cha kijamaa yaani wakwezi, wakulima na wafanyakazi, ni lazima tulinde misingi ya ASP (Afro-Shirazi Party) na TANU (Tanganyika African National Union).”
Katika hatua nyingine amesema CCM kimejipanga kushinda majimbo yote ya Pemba kwa kile alichodai wananchi wamekiamini baada ya kuisimamia Serikali vizuri kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

“Kingine kinachotupa imani hiyo ni baada ya makada wengi waliokuwa wanachama cha ACT-Wazalendo wakiwemo vigogo, makada na wanachama wa miaka mingi wameendelea kujiunga na CCM huku wakieleza kuridhishwa na sera za CCM,” amesema.
Hata hivyo, amesema ushindi huo utapatikana kupitia uchaguzi huru, haki na wa demokrasia na kwamba utang’oa mizizi yote ya upinzani iliyojikita kwa muda mrefu kisiwani humo.
Dk Dimwa ambaye pia Mwenyekiti wa Sekretarieti hiyo, amefafanu kwamba miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika sekta na Serikali ya awamu ya nane ni suluhu ya kumaliza changamoto za wananchi.
Amesema mbali na wanachama wa chama hicho kujiandikisha kwa wingi, lakini kinajivunia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi uliomaliza changamoto za wananchi wa mijini na vijijini kwa zaidi ya asilimia 98.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa UV-CCM Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, amesema kundi la vijana wa Chama hicho wanatakiwa kuwa mfano bora wa kukipigania.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Oganaizesheni CCM Zanzibar, Ibrahim Omar Kilupi aliwasihi wajumbe hao kufanya maamuzi sahihi ya kuhakikisha wagombea wote wanaowateua katika kura za maoni wanakuwa ni wazuri na watakaouzika na kuchaguliwa.
Kilupi, amesema CCM imejipanga vizuri kuendelea kufanya siasa za kistaarabu zinazozingatia ushindani huru unaozingatia matakwa ya Demokrasia.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar, Yahya Abdalla Rashid amesema kazi kubwa aliyobaki kwa sasa ni kuendelea kuhamasishana baina ya wanachama na wananchi kutumia haki yao kikatiba katika uchaguzi huo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Zanzibar, Tunu Juma Kondo amewasihi wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea katika kura za maoni za uchaguzi wa ndani kwa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili waweze kushika uongozi katika vyombo vya maamuzi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma amesema mkoa huo umeendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na juhudi kubwa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.
Amesema kuna maendeleo makubwa yameshuhudiwa katika mkoa huo na Pemba kwa ujumla amabyo hayakuwahi kutokea kipindi cha nyuma.