CCM Moshi mjini kwa moto, ni mtifuano kwa kwenda mbele

Moshi. Waswahili wanasema panapofuka Moshi chini kuna moto, ndivyo unaweza kuelezea kile kinachoendelea katika jimbo la Moshi mjini kufuatia mtifuano baina ya makada wa CCM kutokana na baadhi yao kuanza kampeni za ubunge mapema.

Katika kuthibitisha hilo, baadhi ya makada wanadaiwa kuanzisha makundi mawili ya Whatsapp mahsusi kwa lengo la kumshambulia mbunge aliyepo madarakani, Priscus Tarimo na baadhi ya viongozi wa CCM wasiounga mkono harakati zao.

Licha ya Viongozi wa CCM ngazi ya Taifa na Mkoa kuwaonya makada wa chama hicho kuacha kampeni za mapema na fitina na badala yake wawaache wabunge walioko madarakani watekeleze majukumu yao ipasavyo, hali Moshi ni tofauti.

Jimbo la Moshi Mjini linachukuliwa kama moja ya ngome ya vyama vya upinzani kwa sababu kwa miaka 25 (1995-2020) lilikuwa chini ya upinzania hadi katika uchaguzi mkuu wa 2020 ndipo CCM kwa mara ya kwanza ikashinda kwenye jimbo hilo.

Alipotafutwa na gazeti hili jana, Tarimo anayemaliza kipindi chake cha ubunge 2020-2025, amesema hali ya kisiasa katika jimbo lake ni shwari isipokuwa wapo makada (hakuwataja) wanavunja kanuni na kufanya kampeni kabla ya muda.

“Hali ya kisiasa kama hali ya kisiasa ni shwari isipokuwa wapo watu (makada) wanaovunja kanuni wazi wazi lakini mamlaka zinashindwa kuchukua hatua stahiki. Wengine wanaenda mbali na kudai wametumwa na viongozi wa juu,”amedai mbunge huyo.

Ametolea mfano wa kada mmoja ambaye katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo misiba, amekuwa akijitangaza ndiye mbunge wa Moshi mjini 2025 na wakati mwingine akionyesha mawasiliano ya simu na watu aliodai ni wazito.

Mwenyekiti wa CCM afunguka

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusiana na hili sambamba na kinachoendelea jimboni humo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai licha ya kusema hali ya kisiasa ni shwari, amesema joto la uchaguzi limepanda na kuonya wale wanaovunja kanuni.

“Hali ni shwari, tunaingia kwenye uchaguzi, lakini sasa hivi kuna viongozi ambao bado wako madarakani. Lakini joto la uchaguzi limepanda, maneno ya kawaida, watu wanazungumza siasa kwenye vijiwe wanabadilishana mawazo,” amesema na kuongeza;

“Yapo mawazo ya watu pia huko mitaani wanayazungumza lakini kiujumla hali ya kisiasa (Jimbo la Moshi mjini) ni shwari.”

Akizungumzia mtifuano unaoendelea kwenye makundi ya Whatsapp, mwenyekiti huyo amesema zipo kanuni na taratibu zitakazofuatwa katika kuchukua hatua kwa makada ambao wanavunja kanuni zilizopo.

“Tunapokuja kwenye suala la uchaguzi zipo kanuni na taratibu zinafuatwa, kwa hiyo kwa sasa hivi huko, watu wana uhuru wa kutoa mawazo yao, lakini mtu anapovuka mipaka lamba ya kukashifu mwenzako, hilo tena siyo jambo zuri, ikithibitika, hatua zitachukuliwa,” amesema Swai.

Amesema kwa wale ambao wanajijua ni wana CCM wasijiingize kwenye mkumbo wa malumbano yasiyokuwa na maana kwenye mitandao.

“Kwa sababu ziko hatua za kuwachukulia watu ambao watakuwa wanavunja kanuni na taribu zetu za chama,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema watawachukulia hatua wale ambao watabainika kufanya mambo ya kipuuzi bila kuweka wazi kama chama kilishachukua hatua ingawa taarifa zinadai mmoja alishapewa onyo na Kamati ya siasa wilaya.

Hali ilivyo

Wakati mwenyekiti huyo wa CCM Moshi mjini akieleza hayo, hali mtaani ni tofauti, baadhi ya makada wanadaiwa kutumia nguvu ya fedha kujenga mitandao na ‘kuwashika’ wajumbe kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Habari kutoka ndani ya CCM zinadai baadhi ya makada wanaosaka ubunge, wanafanya kampeni za wazi na wengine kwa kuwatumia baadhi ya makatibu kata wa chama hicho na wengine wakidaiwa kutumia nguvu ya fedha na udini.

Mbali na hilo, baadhi ya makada wanaojipitisha katika jimbo hilo, wanadaiwa kutafuta ushawishi wakitumia majina ya baadhi ya viongozi wa kitaifa wa CCM kuwa wamewapa baraka zote.

Taarifa nyingine ambazo Mwananchi imezipata zinadai kuna kada amehifadhi namba za viongozi wa juu wa chama na Serikali na huwaonyesha wana CCM wenzake kuwa anazungumza nao mara kwa mara na ndiye wanamtaka agombee jimbo hilo katika uchaguzi huu.

Licha ya joto la uchaguzi kudaiwa kupanda katika majimbo yote ya Mkoani Kilimanjaro, lakini inaelezwa Jimbo la Moshi Mjini lina msuguano mkubwa zaidi hali ambayo inatajwa isipodhibitiwa itaweza kukiathiri chama na kutoa fursa kwa wapinzani kushinda.

Na inadaiwa kuna kada mmoja aliyegombea katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2020, ni miongoni mwa walioanza kampeni kwa zaidi ya miaka miwili ni miongoni mwa wanaoongeza kasi ya joto la uchaguzi huo.

Mbali na hilo, Moshi Mjini pia inadaiwa kuenezwa siasa za makundi, chuki, uhasama na na uadui na hata kuchafuana kupitia makundi ya Whatsapp.

Walichokisema Makada wa CCM 

Wakati mwenyekiti wa CCM wilaya akidai kuwa hali ya kisiasa wilayani humo ni shwari, baadhi ya makada wa CCM Moshi mjini, wamedai si  nzuri na kuwataka viongozi kuwachukulia hatua wale wote ambao wanavunja kanuni waziwazi kwa kufanya kampeni ikiwamo vikao visivyo rasmi na kugawa rushwa.

Robert Malivishe amesema kwa sasa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi, hivyo wale wanaohitaji kugombea ubunge na udiwani, wanapaswa kusubiri wakati ufike na si muda wa malumbano na kukashifu viongozi walioko madarakani.

“Hali ilipofikia sasa siyo nzuri kwenye chama chetu, kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi, na tukianza malumbano sasa hivi, tunaweza kujitengenezea ajali wenyewe. Tusubiri muda ufike watu wajitokeze kuchukua fomu,”amesema na kuongeza;-

“Kwa sababu unavyoanza kujitangaza sasa hivi unamfanya hata yule ambaye yuko madarakani kama mbunge au diwani, ataacha kusimamia kazi za maendeleo, sasa itakuwa kazi yake ni kushughulika na yule ambaye anajipitisha kujitangaza.”

Hivyo, kada huyo amekitaka chama kuchukua hatua kali hasa kwa wale wanaojitangaza mapema kinyume na kanuni za CCM sambamba na wale wanaowachafua wenzao.

“Kutoa siri za mwenzio, kurushiana maneno kwenye makundi ya WhatsApp, kumkashifu mtu kwenye misiba au sherehe na hata kusema mbunge fulani hafai si jambo sahihi,” amesisitiza mmoja wa makada hao.

Kwa upande wake, kada wa CCM, Joyce Ndosi amesema tabia ya kuchafuana imezoeleka kipindi cha uchaguzi, lakini akatahadharisha viongozi dhidi ya kujiingiza kwenye makundi ya wanaowania ubunge.

“Watu wanachafuana, lakini mwisho wa siku ni mmoja tu atakayeshinda. Wabunge waliopo madarakani bado wana nafasi ya kutekeleza majukumu yao na wanapaswa kuachwa wafanye kazi zao muda wa kampeni bado,” amesema Ndosi.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali ya CCM imefanya kazi kubwa za maendeleo zinazoonekana, hivyo ni jukumu la viongozi kudhibiti migawanyiko inayoweza kukiathiri chama katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Makundi haya yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa. Viongozi wanaojihusisha nayo wanatupa wakati mgumu,” ameongeza kusisitiza kada huyo.

Hata hivyo ametoa rai kwa CCM kuanza kuchukue hatua ya kutoa elimu kwa wanachama wake kuhusu umuhimu wa kusema ukweli wakati wa kampeni na kuepuka uzushi.

“Viongozi wanapaswa kuchukua hatua, kwani hali inazidi kuwa mbaya. Wasome kanuni na katiba ya chama ili kuzuia uvunjifu wa nidhamu. Ikiwa kuna mtu anayevuruga jimbo, hatua zichukuliwe bila upendeleo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *