Dar es Salaam. Mwaka 2025, Tanzania inakaribia tena kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa kidemokrasia, wananchi watawachagua Rais, wabunge na madiwani watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Uchaguzi huu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, huku maandalizi yakiendelea kushika kasi miongoni mwa vyama vya siasa.
Katika kipindi hiki cha maandalizi, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeimarisha juhudi zake za kujitangaza na kujijenga zaidi, hasa katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Lindi na Mtwara.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM anayesimamia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, alifanya ziara ya siku 10 katika mikoa hiyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
Ingawa malengo rasmi ya ziara yalikuwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa ilani hiyo, matokeo ya kisiasa yalikuwa makubwa.
Zaidi ya wanachama 200 kutoka vyama vya upinzani, Chadema, CUF, na ACT-Wazalendo, walitangaza kujiunga na CCM.
Miongoni mwao ni Vedasto Ngombale, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kupitia CUF, pamoja na madiwani waliokuwa wakihudumu.
Katika Wilaya ya Kilwa ambako ziara ilianza, zaidi ya wanachama 70 wa CUF na Chadema walijiunga rasmi na CCM.
Makalla alieleza kuwa baadhi ya wanachama hao walikuja na mihuri ya ofisi zao, wakionyesha kujitoa rasmi katika vyama vyao vya awali.
“Tumepokea wanachama wapya zaidi ya 70, baadhi yao wakiwa na mihuri ya ofisi zao, ishara ya dhamira yao ya kweli kuunga mkono CCM,” alisema Makalla mbele ya umati wa wanachama.
Mabadiliko haya hayakuishia Kilwa pekee, bali yalienea katika maeneo mengine ya Lindi na Mtwara, ambako pia baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa vyama vya upinzani walijiunga na CCM.
Aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Lindi Mjini, Hamis Mtanda, alitangaza rasmi kujiunga na CCM, akieleza kuvutiwa na juhudi za maendeleo za Rais Samia Suluhu Hassan. Vilevile, Imail Ally Mbelei, aliyekuwa Diwani wa Mbwemkuru kupitia ACT-Wazalendo, alieleza kuwa alichukua hatua hiyo baada ya kuona namna Rais Samia alivyo karibu na wananchi na dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo.
Makada wa zamani wa upinzani waanzisha nguvu mpya ndani ya CCM
Katika ziara hiyo, Makalla aliandamana na makada waliowahi kuwa kwenye vyama vya upinzani na sasa wako CCM – Mchungaji Peter Msigwa (aliyewahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini kwa Chadema), Abdul Kambaya (aliyekuwa Mkuu wa Mawasiliano wa CUF) na Hamidu Bobali (aliyekuwa Mbunge wa Mchinga kupitia CUF).

Makalla aliwataja kama “silaha za msaada,” kutokana na mchango wao mkubwa katika kuvutia wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani.
Abdul Kambaya aliwahimiza wananchi kutambua kuwa maendeleo hutegemea uongozi thabiti na utekelezaji wa sera bora, si kuwepo tu kwenye chama fulani.
Kwa mfano, Diwani wa Nkwedu, Hamis Suleiman, alijiunga na CCM baada ya kushawishiwa na Kambaya, akisema aliamua kwa hiari na kwamba tayari alipokea kadi zaidi ya 300 kutoka kwa wanachama wa zamani wa CUF waliotaka kuhamia CCM.
Vivyo hivyo, Mchungaji Msigwa alisaidia kuvutia wanachama kutoka Chadema, wakiwemo Katibu wa Kanda ya Kusini, Pascal Mmuni, na Diwani wa Kuledi wilayani Masasi, Hamza Kalembo. Msigwa alieleza kuwa uamuzi wake wa kutoka Chadema ni sawa na kufuta historia ya chama hicho katika Kanda ya Kusini.
Ujumbe kwa wanachama wa Chadema
Katika Wilaya ya Nachingwea, Makalla aliwahimiza wanachama wa Chadema waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura kuelekeza kura zao kwa CCM, baada ya Chadema kutoshiriki uchaguzi kutokana na kutosaini makubaliano ya uchaguzi.
Alisisitiza kuwa CCM itaendesha kampeni zake kwa amani na kwa kuzingatia mwongozo wa 4R: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Ujenzi upya.
Chadema yakabiliwa na changamoto za ndani
Ziara hiyo ya Makalla na mafanikio yaliyopatikana yameongeza shinikizo kwa Chadema, ambacho tayari kinakabiliwa na mgawanyiko ndani ya chama.
Kundi la G55 linaendelea kushinikiza chama kishiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kinyume na msimamo wa viongozi wa juu waliotangaza sera ya “Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.”
Mafanikio ya CCM Kusini yanaonekana kuwa uthibitisho wa kukubalika kwa chama hicho kutokana na miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.
Makalla ajibu hoja za upinzani
Katika mikutano yake, Makalla alijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na viongozi wa upinzani, akisisitiza kuwa maboresho katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia ushirikiano na kampuni ya DP World yameongeza mapato ya serikali, kupunguza muda wa meli bandarini, na kuongeza idadi ya makasha.
Alikanusha madai ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, aliyedai kuwa serikali imeuza bandari.

Makalla alisema mapato yanayotokana na bandari yamewezesha serikali kugharamia miradi ya maendeleo kama shule, barabara, na huduma za maji.
Pia alizungumzia sekta ya makaa ya mawe, akieleza kuwa imeleta ajira na mapato ya ndani na nje ya nchi.
Katika mkutano wa hadhara Newala, Makalla alielezea mafanikio ya mfumo wa stakabadhi ghalani katika kuongeza bei ya korosho hadi kufikia Sh4,000 kwa kilo.
“Wanaodai wakulima wananyonywa hawajawahi kulima. Serikali imetoa ruzuku, pembejeo, na kuimarisha ushirika. Ushirika ndio sera ya CCM,” alisema Makalla.
Alisisitiza kuwa mageuzi yanayoongozwa na Rais Samia yamewanufaisha hata waliokuwa wapinzani, na kuwa mifumo hiyo imetengeneza mazingira yenye tija kwa wakulima.